Na Hassan Hamad ,
OMKR
Zanzibar inahitaji kujengewa uwezo zaidi katika
kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake na watoto zikiwemo unyanyasaji
wa kijinsia na ajira kwa watoto.
Makamu Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akibadilisha mawazo na mwakilishi wa
UNICEF Tanzania Jama Gulaid ofisini kwake Migombani. Kulia ni Mkuu wa UNICEF
Zanzibar Francesca Morandini
Hayo yameelezwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani, alipokuwa na
mazungumzo na ujumbe wa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa
(UNICEF).
Amesema vitendo vya unyanyasaji vimekuwa
vikiendelea dhidi ya wanawake na watoto jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa
maslahi ya taifa na kukuza ustawi wa jamii.
Amesema serikali imekuwa ikichukua juhudi
kuwaelimisha wananchi juu ya athari ya vitendo hivyo kwa jamii, na kwamba
jitihada zaidi zinahitajika kuweza kuvitokomeza vitendo hivyo.
Makamu Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na mwakilishi wa UNICEF
Tanzania Jama Gulaid, ofisini kwake Migombani (Picha na Salmin Said,
OMKR)
Amefahamisha kuwa serikali imeweka msisitizo katika elimu kwa watoto, ndio maana imefikia hatua ya kuweza kuwaandikisha watoto wote waliotimiza umri wa kwenda skuli.
Amefahamisha kuwa serikali imeweka msisitizo katika elimu kwa watoto, ndio maana imefikia hatua ya kuweza kuwaandikisha watoto wote waliotimiza umri wa kwenda skuli.
Sambamba na hilo amesema serikali imekuwa
ikifanya jitihada za kuwarejesha skuli watoto walioacha skuli kwa sababu mbali
mbali zikiwemo umaskini na ajira, hatua ambayo inaonesha kuleta mafanikio.
Hata hivyo amesema sekta ya elimu bado
inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhaba wa madarasa, walimu wa sayansi
na mitaala isiyotoa uhakika wa ajira kwa vijana baada ya kuhitimu masomo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UNICEF Tanzania
Jama Gulaid, amesema Zanzibar imepiga hatua nzuri katika kukabiliana na vitendo
vya unyanyasaji wa wanawake na watoto ikilinganishwa na nchi nyengine za Afrika,
hasa katika kuzipitia na kurekebisha sheria zinazowahusu watoto.
Gulaid amesisitiza haja ya kulinda afya ya mama
na watoto wachanga, kwa kuwashauri akinamama kuwanyonyesha watoto miezi sita
mfululizo bila ya kuwapa chakula chengine.
Amefahamisha kuwa hatua hiyo inasaidia kwa
kiasi kikubwa kutunza afya ya mtoto na kumlinda dhidi ya maradhi mbali mbali,
sambamba na kuimarisha afya ya mama.
Ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea
kushirikiana na Zanzibar kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa kwa maslahi
yao na Taifa kwa jumla.
Katika mazungumzo hayo Gulaid aliambatana na
mkuu mpya wa UNICEF Zanzibar, Francesca Morandini.
Chanzo - zanzinews.com
Post a Comment