WAKATI taasisi ya Kijerumani ikitoa ripoti iliyoainisha ‘madudu’
mengi yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania, Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kimeanika matukio yote mabaya yaliyofanywa na Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kikitumia kikundi cha vijana wake wa Green Guard.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
CHADEMA, John Mnyika, amekitaja kikundi cha Green Guard kuwa cha hatari
kutokana na kuhusika na matukio mengi ya kigaidi.
Mnyika amesema matukio hayo yana baraka zote za CCM na serikali
kutokana na ukweli kwamba kikundi hicho hakiguswi wala kuchukuliwa hatua
na vyombo vya dola, pamoja na kuhusishwa kwa ushahidi mwingi na
matukio
mengi.
“Hawa wameshiriki matendo mabaya ya utekaji, upigaji, kujeruhi na yapo
ya vifo. Lakini kwa sababu kinafanya haya kwa baraka za CCM na serikali
yake, hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya yeyote.
“Tumetoa taarifa nyingi tu na zenye ushahidi wa waziwazi wa kuhusika
kwa kikundi hicho, ambacho sasa kinasimamiwa na Mwigulu Nchemba, lakini
polisi hao hao wanaotusakama leo kwa vile tumeamua kusema ukweli,
hawajachukua hatua zozote dhidi ya yeyote yule,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa CHADEMA imesema sana kuhusu ukatili huo, lakini katika
hali ya kusikitisha viongozi wa siasa wanaojitokeza kulaani hatua ya
chama hicho kuamua kutoa mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake, wamegeuka
mabubu kuikemea CCM na serikali yake.
Malalamiko hayo ya CHADEMA yanafanana pia na yale yaliyotolewa juzi
katika ripoti ya Shirika la Konrad Adenauer Stiftung la Ujerumani
linalojihusisha na utafiti wa masuala ya siasa nchini.
Shirika hilo katika ripoti yake ambayo inadaiwa kusambazwa ndani na
nje ya nchi, imeshutumu vikali matukio hayo, huku ikisukuma lawama kwa
vyombo vya dola kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watu
wanaodaiwa kuhusika na ukatili huo.
Pia shirika hilo limetahadharisha kuwepo kwa uwezekano mkubwa zaidi wa
vitendo vya kikatili kwa viongozi wa vyama vya upinzani, wanaharakati
na wakosoaji wa serikali kadiri chaguzi zinavyokaribia.
Ripoti hiyo iliyoandikwa na Danja Bergman na Stefan Reith, iliyotolewa
tangu mwezi uliopita, inazungumzia matukio mbalimbali yaliyolikumba
taifa kwa siku za karibuni, yakiwemo ya mabomu yaliyolipuliwa katika
mkutano wa CHADEMA na Kanisa Katoliki la Olasiti jijini Arusha.
Hata hivyo, wachunguzi hao wana maoni kuwa ongezeko la matumizi ya
mabavu kutoka kwa vyombo vya dola dhidi ya maandamano halali na
ukosoaji, ni dalili tu ya mambo makubwa zaidi yanayoweza kutokea katika
kipindi cha miaka miwili ijayo, ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa na
uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika.
Ripoti hiyo pia inasema katika hali hiyo, kwa kadiri ya hali ilivyo
kila aina ya vitisho, udanganyifu na matumizi ya mabavu vitakuwa
vikibadilishwa badilishwa na kutokea katika sura tofauti ikiwemo vurugu
ili kupotosha umma, huku watuhumiwa wakishindwa kutambuliwa, na wale
wanaotambuliwa watafichwa au kutochukuliwa hatua zozote za kisheria na
mamlaka husika.
Ripoti hiyo imeenda mbali zaidi na kusema kuwa hata pale vyombo vya
dola vinapohusishwa na mauaji, kwa ushahidi wa wazi, watuhumiwa wamekuwa
wakilindwa na kuendelea kutesa mitaani bila kuchukuliwa hatua zozote za
kisheria, badala yake wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakishitakiwa
kwa kesi mbalimbali za kubambikiza, zikiwemo uchochezi, ugaidi na
kuhamasisha chuki kati ya wananchi na serikali yao.
CHADEMA imeorodhesha matukio yanayodaiwa kutendwa na vijana wa CCM kama ifuatavyo:
Juni 16 na Julai 14 katika uchaguzi wa kata nne za Arusha vurugu
nyingi ziliripotiwa zikiwahusu wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi kuteka,
kujeruhi na kupewa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kusimamia shughuli za
ulinzi katika chama hicho kikongwe nchini.
Vijana CHADEMA watekwa
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Bunda, Joshua Mirumbe, aliyekaimu nafasi hiyo
pia Wilaya ya Serengeti alituhumiwa kuwateka vijana kadhaa wafuasi wa
CHADEMA akitumia magari STK 8430, T 286 BFB, T 245 BFE, yanayomilikiwa
na CCM pamoja na gari T 352 AHD, T 573 BEW akisaidiwa na askari magereza
na kuwapeleka kwenye jengo moja la chama tawala.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mkuu wa wilaya huyo alitaka kuwatumia
polisi, lakini Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo alimkatalia, hali
iliyomlazimu kwenda kuwachukua askari magereza kwa ajili ya kutekeleza
operesheni hiyo iliyodumu usiku kucha kabla ya kuwapeleka vijana hao
polisi baada ya kubanwa na CHADEMA.
Katika Kata ya Iyela, gari la CCM lenye namba T 704 BEU, likiwa na
watu wawili wanaotambulika kwa majina ya Moris na Nosy, waliwateka
vijana wa CHADEMA ambapo mmoja wao Meshack Bernad alichomwa kisu.
Pikipiki yapigwa moto
Pikipiki ya CHADEMA ilichomwa moto na vijana wa CCM (Green Guard) na
Katibu wa CHADEMA wilaya ndugu, Lucas Daniel amepigwa na kuumizwa, huku
mwenyekiti wa jimbo hilo, Kibam Ally Mohamedi akijeruhiwa na katibu
Mwenezi Severine Matanila kukatwa vidole.
Risasi za moto
Watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
waliwafyatulia risasi za moto viongozi na makada wa CHADEMA katika
uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Sengerema wakati wafuasi wa CCM na
CHADEMA walipokutana kufuatilia hali ya mambo katika vituo vya kupigia
kura Kata ya Nyampulukano.
Katika tukio hilo, milio ya risasi zaidi ya nne ilisikika kutokea
upande wa pili wa CCM, ambapo magari matatu yalilizunguka gari moja la
CHADEMA Kanda ya Magharibi likiwa na kiongozi wa Kikosi cha Movement for
Change (M4C), Kanda ya Ziwa Magharibi, Alfonce Mawazo, Hussina Amri na
makada kadhaa.
Green Guard waitwa Janjaweed Zanzibar
Kundi hilo lililoasisiwa mwaka 2005 limewahi kuvitingisha visiwa vya Zanzibar wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005.
Wakati wa kampeni za uchaguzi huo vijana wa kundi hilo walipelekwa
visiwani humo kwa lengo la kudhibiti nguvu za Chama cha Wananchi (CUF)
kwa kuwapiga na kuwatesa viongozi na wanachama wa chama hicho kikuu cha
upinzani visiwani humo.
Kutokana na vitendo vyake vya vurugu na ghasia za kupiga na kutesa
watu, kundi hilo lilipachikwa jina la Janjaweed, likilinganishwa na
wanamgambo wa Kiarabu waliotekeleza mauaji ya zaidi ya watu 300,000 huko
Darfur, nchini Sudan.
Wabunge wa CHADEMA wakiona cha moto
Juni 17, mwaka huu, vijana wa Green Guard walimshambulia na
kumuumiza vibaya mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, wakati wa
uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli.
Machi, 2012, wabunge wawili wa CHADEMA mkoani Mwanza, Highness Kiwia
wa Ilemela na Salvatory Machemuli wa Ukerewe walivamiwa na kushambuliwa
vikali kwa mapanga na nondo na vijana wa Green Guard wa CCM wakiongozwa
na mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Ahmed Mkilindi.
Shambulio hilo lilitokea wakati wabunge hao wakiratibu kampeni za
uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kirumba, mkoani humo, ambapo
CHADEMA kilishinda.
Wamteka kada
Septemba 28, 2011, Green Guard walimshambulia kada wa CHADEMA Odero
Odero wakati mwenyekiti huyo akielekea kwenye kampeni za uchaguzi wa
udiwani huko Engototo ambao ulitarajiwa kufanyika Oktoba 2, 2011.
Kada huyo alitekwa na mwenzake aitwae Maganga ambaye alifanikiwa
kutoroka na kwenda kutoa taarifa polisi ambao walianza msako wa
kumtafuta Odero na kumkuta akiwa ametelekezwa katika pori moja huko
Engototo akiwa hoi kwa kipigo huku watekaji wakiwa wameondoka na nyaraka
zote alizokuwa nazo.
Wamvunja mbavu mwanachama
Mei 22, 2009, vijana wa Green Guard walimshushia kipigo na kumvunja
mbavu mwanachama wa CHADEMA katika Jimbo la Busanda, mkoani Geita.
Polisi hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la kihalifu.
Washambulia wananchi
Oktoba 25, 2012, vijana wa Green Guard waliwashambulia na kuwaumiza
vibaya wananchi wa Daraja Mbili, mkoani Arusha, baada ya kuonyesha
ishara ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA.
Wavamia hoteli
Septemba 24, 2011, vijana wa Green Guard waliokuwa wakipatiwa mafunzo
haramu ya kijeshi na kigaidi katika makambi maalumu mkoani Singida,
walivamia hoteli waliyofikia viongozi wakuu wa CHADEMA wilayani Igunga
wakiwa na gari aina ya Toyota Landcruiser VX mbili mali ya CCM wakitaka
kuchoma moto magari mawili ya matangazo (PA).
Jaribio hilo lilishindwa baada ya kudhibitiwa na walinzi wa CHADEMA na
kufanikiwa kuwakamata na kisha kuwapeleka polisi, lakini katika
mazingira ya kushangaza, vijana hao waliachiwa huru bila kufikishwa
mahakamani.
Washambulia mwandishi
Septemba 25, 2011, vijana wa Green Guard walimshambulia kwa ngumi na
mateke mwandishi wa gazeti la Dira ya Mtanzania, Mussa Mkama
aliyekwenda katika hoteli waliyofikia viongozi wa CCM ili kuzungumza na
mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya (CCM).
Walimshambuliwa kwa maelekezo ya Mwigulu Nchemba, kutokana na
mwandishi huyo kuandika habari ya kushikwa ugoni kwa kiongozi huyo wa
CCM ambaye katika kampeni za uchaguzi mdogo wilayani Igunga alikuwa
meneja wa kampeni za chama chake.
Mwandishi Tanzania Daima anusurika kuchinjwa
Oktoba 4, 2011, mwandishi wa gazeti hili George Maziku aliyekuwa
wilayani Igunga kuripoti uchaguzi mdogo wa ubunge, alinusurika kuchinjwa
na vijana wa Green Guard wa CCM akifuatilia vurugu zilizofanywa na
vijana hao wakitaka kuwadhuru wafuasi wa CHADEMA huku wakiwa wamebeba
silaha za jadi, yakiwemo mapanga, visu, nondo, marungu, na majembe.
Maziku alijikuta akiwa amezingirwa na vijana hao ambao hawakutaka kuandikwa maovu yao, wakiwa tayari kumtoa uhai.
Aliokolewa na kiongozi mmoja wa CCM aliyekuwa katika hoteli ya
viongozi wa CCM, na kumtoa kwa nguvu kwenye mikono ya Green Guard
waliokuwa tayari kumcharanga mapanga na visu.
Tindikali
Septemba 11, 2011, mmoja wa vijana wa Green Guard alikamatwa na kiasi
kikubwa cha tindikali na polisi. Ndiyo siku aliyomwagiwa tindikali
Mussa Tesha.
Kada wa CHADEMA auawa
Oktoba, 2011, Green Guard walimteka, wakampiga na kumtesa, na kisha
kumuua kada wa CHADEMA Mbwana Masudi mkazi wa Dar es Salaam ambaye
alipelekwa na chama chake wilayani Igunga kuwa wakala katika uchaguzi
mdogo wa ubunge.
Mashambulizi kituo cha polisi
Kiteto (2007) waliwashambulia wafuasi wa CHADEMA ndani ya kituo cha polisi.
Wakata mapanga
Tarime (2008) wanatuhumiwa kuwakata mapanga wanachama wa CHADEMA, na wakafanya tena hivyo Busanda na Biharamulo (2009)
Kambi za mafunzo
Kambi ya vijana iliyofanyika Kijiji cha Ughaugha, mwaka 2005, kabla
ya Uchaguzi Mkuu, vijana zaidi ya 200 walikaa wiki sita, chini ya
Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Singida Mjini.
Kata ya Unyambwa, katika Shule ya Msingi Ipungi, Kijiji cha Kisasida,
chini ya Katibu wa UVCCM wa Singida Mjini, Musa Sunja, kijana kutoka
Kata ya Mwankoko na walikaa wiki mbili wakipata mafunzo yaliyoitwa ya
ukakamavu.
Kambi iliyoundwa mkoani Mbeya baada ya Mwigulu kufika mkoani humo,
iliyokuwa na vijana 376, katika Shule ya Sekondari ya Ivumwe, Kata ya
Mwakibete, na walifanya vitendo vya utekaji, kauli iliyothibitishwa na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.
Kambi nyingine kubwa ni ile ya Ulemo, iliyofanyika kwa ajili ya
kuhusika na fujo katika uchaguzi mdogo wa Igunga na mmoja wa washiriki
amekiri chini ya kiapo mafunzo waliyokuwa wanafanya.
TANZANIA DAIMA:::::::::::::
Post a Comment