UBAGUZI baina ya vyama vya upinzani uliopata nguvu bungeni wakati wa kuanzisha Kambi Rasmi ya Upinzani chini ya Chadema, umeanza kutafuna chama hicho chenye ushawishi mkubwa kuliko vyama vingine vya upinzani Tanzania Bara.
Uundwaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, ulitokana
na msimamo wa Chadema yenye wabunge wengi bungeni, kukataa kushirikisha vyama
vingine vya upinzani, ikiwamo CUF ambayo ilikuwa na idadi ya wabunge
wanaotosheleza kuunda Kambi ya Upinzani, lakini imezidiwa kiidadi na
Chadema.
Chadema pia ilikataa kushirikiana na NCCR- Mageuzi,
TLP, UDP na kuamua kuunda kambi ya wabunge wa Chadema pekee, ambapo kwa busara
kwa kuwa CUF pia ingeweza kuunda Kambi ya Upinzani, kambi hiyo ya Chadema
ikapewa jina la Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
Athari za ubaguzi huo
zilijitokeza Arusha hivi karibuni, ambapo chama hicho kilionekana kutaka
kuongoza halmashauri ya jiji hilo, lakini kikashindwa baada ya kukosa kura mbili
tu za TLP, na jana imejidhihirisha wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Katika siasa za Arusha, baada ya Chadema kutetea viti
vyake vinne vya udiwani katika uchaguzi mdogo na uliokuwa muhimu kwa siasa za
Chadema, ilifikisha viti 15 kwenye Baraza la Madiwani la Arusha, huku CCM
ikibakiwa na viti 12 na TLP viti sita.
Pia Chadema mbali na kuwa na viti hivyo 15, inayo
nafasi ya kuongeza kiti zaidi, kwani kuna nafasi moja ya viti maalumu iliyokuwa
ikishikiliwa na Rehema Mohamed, aliyetimuliwa mwaka
2011.
Hata hivyo, pamoja na Chadema kuongoza kwa kuwa na viti
vingi vya udiwani Arusha, haikuwa na uwezo wa kumweka Meya, kwa kuwa idadi ya
madiwani wake ni 16 na kingehitaji zaidi ya kura 17 katika baraza, ili kupata
nafasi ya kuongoza halmashauri hiyo.
Hivyo Chadema ilihitaji kushirikiana na TLP, ili kupata
zaidi ya nusu ya kura inayohitajika kikanuni kumuweka Meya
madarakani.
Uvinza Baada ya Chadema kusema haina uroho wa madaraka
katika umeya wa jiji la Arusha, chama hicho kimejikuta katika mazingira kama ya
Arusha, mkoani Kigoma.
Mkoa wa Kigoma, katika halmashauri mpya ya Uvinza, Chadema ikishindwa kuishawishi NCCR-Mageuzi kuwaunga mkono, itakuwa katika mazingira ya kukosa nafasi ya kuongoza halmashauri hiyo mpya.
Mkoa wa Kigoma, katika halmashauri mpya ya Uvinza, Chadema ikishindwa kuishawishi NCCR-Mageuzi kuwaunga mkono, itakuwa katika mazingira ya kukosa nafasi ya kuongoza halmashauri hiyo mpya.
Katika halmashauri hiyo, CCM ina madiwani wanane,
Chadema madiwani saba na NCCR-Mageuzi inayo madiwani watano na Mbunge mmoja,
ambaye anaingia katika Baraza la Madiwani na anaruhusiwa kupiga kura na hivyo
chama hicho kuwa madiwani sita.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alinukuliwa akiwataka madiwani wa Chadema na
NCCR- Mageuzi, kuunganisha nguvu ili CCM iunde Kambi ya Upinzani katika
halmashauri hiyo.
“Chadema na NCCR-Mageuzi tuna madiwani 13 katika
Halmashauri ya Wilaya Uvinza…CCM ina madiwani wanane tu, hivyo tuna kura nyingi
upinzani. Chadema ina madiwani saba, NCCR-Mageuzi watano na Mbunge mmoja,”
alinukuliwa Zitto akishawishi huku akisema wakishindwa kuungana, CCM itapita
katikati.
Umoja wavunjika Tofauti na
matazamio ya Zitto, kwamba vyama hivyo vingeweka mgombea mmoja dhidi
ya mgombea wa CCM, Hamisi Mkwafi, NCCRMageuzi pamoja
na kuwa na madiwani sita tu, ilisimamisha mgombea wake, Fidelis Kumbo, na
Chadema ikaamua kuweka mgombea wake, Cassiano
Mabondo.
Katika mazingira yaliyoonesha kuwa vyama hivyo vya
upinzani, ikiwemo Chadema vilikuwa na uroho wa nafasi ya Mwenyekiti,
havikusimamisha mgombea katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, ambayo CCM ilijikuta
ikiwa haina mpinzani baada ya kumsimamisha Diwani wa Kalya, Lucas
Kanoni.
Awamu ya kwanza ya uchaguzi huo uliokuwa ukisimamiwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Nicolous Kombe na Mbunge
wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ulishindwa kupata mshindi baada ya kila chama
kupata kura saba.
Matokeo hayo yaliamsha mjadala wa muda mrefu na
mwishowe walikubaliana uchaguzi huo urudiwe, ambapo matokeo yake yalionesha kuwa
wajumbe walipigia kura wagombea wa vyama vyao kwani mgombea wa CCM, aliongoza
kwa kupata kura nane na kufuatiwa na mgombea wa Chadema aliyepata kura saba na
wa NCCR -Mageuzi aliambulia kura sita.
Utata Baada ya matokeo ya uchaguzi wa raundi ya pili,
mjadala uliibuka tena kuhusu matakwa ya kikanuni, kwamba mshindi anapaswa kupata
zaidi ya nusu ya kura za wajumbe waliopiga kura, ambazo ni 11, jambo ambalo
hakuna mgombea hata mmoja aliyefikisha.
Msimamizi wa Uchaguzi, Kombe alilazimika kusitisha
mjadala huo kwa muda, ili wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wapate ufafanuzi wa
kisheria, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI).
Baada ya zaidi ya saa moja ya kusubiri, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Miriam Mbaga, alisema majibu
waliyopata yanaeleza kuwa aliyeshinda kwa kura nyingi, mgombea wa CCM Mkwafi,
anapaswa kutangazwa mshindi.
Majibu hayo ya Mkurugenzi yalizua tafrani ambapo baadhi
ya madiwani walimtaka Mkurugenzi huyo kufuta kauli hiyo, kwa madai kwamba si
kauli rasmi.
Mkurugenzi huyo alilazimika kufuta kauli hiyo, na
baadaye Msimamizi wa Uchaguzi, Kombe aliahirisha uchaguzi huo hadi
utakapoitishwa upya.
Baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa Mwenyekiti,
wajumbe walikataa kupiga kura kumchagua Makamu Mwenyekiti, ambayo ilikuwa na
mgombea mmoja, Kanoni (CCM).
Post a Comment