JERRY SILAA |
MTANZANIA Jumapili, katika uchunguzi wake lilishuhudia jengo hilo likiendelea kuwepo, huku baadhi ya wafanyabiashara jirani na jengo hilo wakiendelea na kazi zao kama kawaida.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Msemaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Abrahamu Nyantori, ambaye alisema wao kama wizara tayari waliagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuhakikisha jengo hilo linabomolewa ndani ya siku saba.
Gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Mwendahasara Maganga, ambaye alisema kuwa, tayari alianza kutaka kutekeleza amri hiyo, lakini hata hivyo mmiliki wa jengo hilo alikimbilia mahakamani.
Alisema kutokana na mmiliki huyo kukimbilia mahakamani, shughuli za ubomoaji zimesitishwa ambapo shauri hilo limekabidhiwa kwa wanasheria wa manispaa hiyo kwa ajili ya ufuatiliaji zaidi.
“Sina cha kusema zaidi ya kusema tayari tuliandika notisi ya siku saba ili jengo libomolewe, lakini mmiliki amekimbilia mahakamani hivyo wanasheria wetu wanaendelea kufuatilia zaidi kesi hiyo,” alisema Mkurugenzi huyo.
Gazeti hili lilimtafuta Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba (NHC), Yahya Cherehani, kupitia simu yake ya kinganjani, ambapo alisema wao kama NHC, jukumu lao ni kumiliki kiwanja tu, hivyo mwenye jukumu la kutekeleza agizo hilo ni mmiliki wa jengo hilo.
Jengo hilo linapakana na eneo ambapo lilikuwapo jengo la ghorofa 16 lililoanguka hivi karibuni.
Kibali cha kujengwa jengo hilo kinaonyesha kuwa lilipaswa kujengwa ghorofa tisa, lakini limejengwa ghorofa 17 na Waziri wa Ardhi alikwisha agiza libomolewe ili kuzuia maafa mengine.
Suala hilo lilishawahi kufika bungeni katika Bunge lililopita, ambapo Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alitaka kupata ufafanuzi juu ya ubomoaji wa jengo hilo, ambapo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Agrey Mwanri, alisema serikali haiwezi kutoa agizo haraka kiasi hicho kama mbunge huyo anavyopendekeza.
Ghorofa hilo linalomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Ally Raza, linatakiwa kubomolewa baada ya kuanguka kwa jengo pacha la aina hiyo Machi 29, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 36, kujeruhi 18 na uharibifu wa mali.
Awali Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, alisema wametoa notisi ya kubomolewa kwa jengo hilo kuanzia Mei 27 hadi Juni 3, mwaka huu.
Chanzo: mtanzania
Post a Comment