Wizara
ya Maliasili na Utalii inakanusha uvumi
ulioandikwa nakuchapishwa na gazeti la Raia Mwema mnamo tarehe
07/08/2013 ukurasa wa kwanza lililobeba kichwa cha habari UFISADI kama wabunge, wateule wa waziri wasaini posho mara mbili ikiwa na ufafanuzi kuwa yumo Ofisa Takukuru,walipwa na taaasisi wanayoichunguza. Taarifa hii ilikuwa na muendelezo zaidi ukurasa wa tatu wa gazeti hilo.
Wizara inasisitiza kuwa uvumi huo siyo kweli kutokana na sababu zifuatazo:
- Wajumbe wa kamati husika (iliyoundwa kuchunguza tuhuma kuhusu matumizi mabaya ya fedha unaowahusisha watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) (NCAA) HAWAKULIPWA POSHO MARA MBILI.
- Malipo waliyolipwa wajumbe wa kamati husika yalilipwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kama ilivyo kwenye Hadidu za Rejea za kazi husika na hawakulipwa malipo yoyote na wizara ya maliasili na utalii.
- Viwango vya posho vilivyotumika ni kwa mujibu wa Waraka wa Serikali namba 2 wa Mwaka 2010, Ref.Na C/AC/.17/45/01/125
- Malipo yaliyofanywa kwa wajumbe wa kamati husika yalikuwa na kibali halali cha Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Khamis Suedi Kagasheki
- Kamati husika ilifanya kazi vizuri na kukabidhi ripoti ya awali iliyomridhisha Waziri Kagasheki aliyewaagiza kuifanya kazi tajwa hapo juu. Ripoti hiyo ya awali na hii ya mwisho ZITAWEKWA HADHARANI ili Umma uelewe hali halisi ya Mamlaka ya Ngorongoro na siyo upotoshaji wa Raia Mwema.
- Kamati iliyoundwa na Waziri Kagasheki ilikuwa na kazi tofauti na ile kamati ya awali iliyowahi kuongozwa na Jaji Robert Mihayo aliyeteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige mwaka 2011. Raia Mwema ingejiridhisha kwa kutazama hadudi za rejea za Kamati hizo mbili. Si jambo jema Raia Mwema kuupotosha Umma.
Kwa taarifa hii, Wizara inalitaka Gazeti la Raia Mwema kufuta uvumi waliochapisha kwenye gazeti lao kama ilivyotajwa hapo juu na pia kuiomba radhi Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuchapisha habari ambazo si sahihi na pia kuchafua jina la Wizara.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
12/08/2013
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
12/08/2013
Post a Comment