Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MADINI NI MAJANGA MATUPU

 

WAFANYABIASHARA WAPIGWA RISASI, WAPORWA ARUSHA

Na Irene Mark

MATUKIO ya uporaji na utoroshaji madini yanazidi kushika kasi ambapo wafanyabishara wawili wa madini ya Tanzanite jijini Arusha wamejeruhiwa kwa risasi na kuporwa kiasi kikubwa cha madini yenye thamani ya zaidi ya sh mil. 60 fedha taslimu huku Ofisa Usalama wa Uwanja wa ndege mkoani Kigoma naye akitiwa mbaroni kwa kutaka kutorosha madini.

Matukio hayo mawili yalitokea juzi na jana zikiwa ni siku chache tangu kuuawa kwa mfanyabiashara bilionea wa jijini Arusha Erasto Msuya aliyepigwa risasi zaidi ya 20 wilayani Hai mkoani Kilimanajaro.

Wakati hali ikiwa hivyo, wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) umetangaza kukamata shehena ya madini yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 13 katika kipindi cha miezi 10 yaliyokuwa yakitoroshwa nchini kinyume cha utaratibu.

Katika tukio la jijini Arusha lililotokea jana saa 9:30 alasiri eneo la Pangani, wafanyabiashara Steven Alex na Abel Mutta walipigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakati wakiwa kwenye gari kando ya barabara walikokuwa wamekuja kununua madini hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini akadai asingeweza kulizungumzia kwa vile hakuwa na taarifa kamili.


Hata hivyo mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa wafanyabiashara hao walikuwa ndani ya gari aina ya Range rangi ya Silva ambapo Alex alikuwa upande wa dereva na Abel alikuwa upande wa pili wakiwa na mtu mwingine nyuma ambaye hakufahamika jina lake mara moja.

Wakati wafanyabiashara hao wakiwa wameegesha gari kando ya barabara kusubiri kuwalipa watu waliowauzia madini, zilikuja pikipiki tatu zikasimama kando ya gari lile na vijana watatu walishuka na bastola kisha kumsogelea Alex wakimtaka afungue mlango.

“Vijana hao walikuwa wakidai afungue awape hela zao lakini hakufanya hivyo, ndipo wakampiga risasi tumboni na kwenye paja huku Mutta akipigwa ya mguuni na kisha walifungua mlango wa gari baada ya kuwajeruhi wakachukua madini na fedha,” alisema shuhuda mmoja.

Aliongeza kuwa baada ya kufanikisha mpango wao, vijana hao waliondoka na pikipiki zao ambazo zilifichwa sehemu ya namba za usajili huku kila mmoja akielekea barabara yake.

Ofisa Kigoma

Mkoani Kigoma, mmoja wa maofisa usalama wa uwanja wa ndege, Clephace Lukindo, alikamatwa na maofisa wenzake uwanjani hapo akitaka kuvusha madini ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu tisa sawa na thamani ya sh milioni 400.

Hata hivyo tukio hilo limekuwa likifichwa na uongozi wa uwanja pamoja na jeshi la polisi mkoani humo kwa kile kinachodaiwa kuwa ofisa huyo amekuwa akitoa vitisho kwa wafanyakazi wenzake.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, ofisa huyo ambaye anadaiwa kuwekewa mtego na maofisa wenzake wawili baada ya kubaini mpango wake huo wa kutaka kuvusha mzigo huo kwa kutumia leseni ya kusafirishia madini ya mtu mwingine.

Taarifa zilidokeza kuwa ofisa huyo licha ya kuwa na leseni hiyo isiyokuwa ya kwake, hakuwa na nyaraka zingine za kuonyesha alikopata mzigo, anaupeleka wapi na kiasi chake.

Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya kufika eneo la ukaguzi, ofisa mwenzake, Yusuf Mpame, na polisi Koplo Theophil walimtaka aonyeshe vibali na nyaraka hizo ili wathibitishe kuwa mzigo huo unasafirishwa kihalali.

Hata hivyo Lukindo baada ya kuona wenzake wamemshtukia na kutaka kumkamata alitumia nguvu kumkaba ofisa mwenzake Mpame ambaye alimnyonga shingo na kisha kung’ata lakini akanusuriwa na wenzake Koplo Theophil na Jeremiah.

Meneja wa uwanja huo aliyefahamika kwa jina moja la Tesha, alipotafutwa na gazeti hili alipokea simu lakini alipoulizwa juu ya sakata hilo alikatika ghafla hewani na alipopigiwa tena hakupokea.

Mmoja wa wafanyakazi wa uwanja huo alilidokeza gazeti hili kuwa Lukindo alikuwa ayasafirishe madini hayo kwenda jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la ndege la Tanzania lakini baada ya sakata hilo alikamatwa na kupelekwa polisi alikoshikiliwa hadi jana.

Majeruhi aliyeumizwa na mtuhumiwa huyo alifikishwa hospitali na kupatiwa matibabu ya shingo ingawa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, licha ya kupigiwa simu mara mbili alikwepa kulizungumzi tukio hilo akisema anaendelea kulifuatilia.

“Sina taarifa kuhusu tukio hilo unaloliuliza hadi sasa,” alijibu kamanda lakini alipobanwa aeleze hali ya ofisa aliyejeruhiwa inaendeleaje alisema hilo bado walikuwa bado wanalichunguza na likikamilika watalitolea taarifa.

Wakati tunakwenda mitamboni, taarifa zilizotufikia zilisema kuwa ofisa huyo alipewa dhamana na jeshi hilo.

TMAA na utoroshaji

Madini hayo yalikamatwa kwenye viwanja mbalimbali vya ndege nchini ambapo wakaguzi wa TMAA walishirikiana na Idara ya Uhamiaji, Usalama wa Taifa, watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Jeshi la Polisi na wafanyakazi wa viwanja vya ndege (TAA).

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za wakala huyo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta, alisema madini hayo yalikamatwa kati ya Septemba mwaka 2012 na Julai mwaka huu katika matukio 23 tofauti.

Alisema kwa mwezi huu tayari wakala huyo amewakamata raia wawili wa kigeni wakiwa na shehena ya madini wakitaka kutoroka nayo huku akisisitiza kwamba watapandishwa kizimbani wakati wowote.

“Agosti 20, mwaka huu, tumewakamata raia wawili wa kigeni mmoja aliyekuwa anasafiri amekamatiwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na madini ya vito yenye thamani ya sh milioni 25.32.

“Wa pili amekamatwa akiwa kwenye makazi yake Jangwani Beach hapa jijini kwa kweli thamani ya madini ya mtuhumiwa huyu haijafahamika,” alisema na kuongeza kuwa serikali imeyataifisha madini hayo.

Kwa mujibu wa Mteta wafanyabiashara wa kigeni na wazawa wanaruhusiwa kusafirisha madini hayo kwa kuzingatia utaratibu ili serikali ipate mgao wake.

Awali, mkurugenzi huyo alisema tangu mwaka 2009 hadi mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilipokea sh bilioni 317.74 ambazo ni mrabaha uliolipwa na kampuni 10 kubwa za madini hapa nchni.

Alisema hivi sasa wizi wa madini kwenye migodi mikubwa haupo kutokana na uwepo wa watumishi wa TMAA wanaotoa ripoti ya uzalishaji kila siku na kwamba wafanyabiashara wa madini wanaoongoza kwa kukwepa kodi ni wazawa.

Mteta alieleza changamoto zinazowakabili kuwa ni kushindwa kuifikia mipaka yote inayounganisha nchi jirani (njia za panya) ambazo hutumiwa na wafanyabiashara wengi kutorosha madini hayo.

Alisema watoroshaji wengi wa madini hayo ni wageni kutoka nchi mbalimbali ambao wanauziwa madini na Watanzania na kufafanua kwamba kati ya matukio 23 Watanzania ni wawili.

Alisema tayari kesi tatu kati ya 23 zimesikilizwa na kutolewa hukumu na kutoa mfano wa kesi ya mgeni aliyekamatwa na madini yenye thamani ya zaidi ya dola 6,200 za Marekani kwamba alitozwa faini ya sh milioni 1.5 na madini yake kutaifishwa na serikali.

Chanzo - Tanzania Daima
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top