Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema baraza lake linajiandaa kutumia teknolojia
ya kompyuta wakati wa kusahihisha maswali ya mitihani ambayo wanafunzi wanajibu
kwa kujieleza.
Kwa sasa teknolojia ya usahihishaji kwa kompyuta
inayotumika nchini ni ile ya kujibu maswali ya kuchagua tu ya`Optical Mark
Reader’ (OMR) iliyoanza kutumika mwaka jana kusahihisha mitihani ya darasa la
saba.
Akizungumza na mwandishi wetu jana wakati wa Mkutano wa
Mabaraza ya Mitihani Afrika (AEAA), unaoendelea mjini hapa, Dk Ndalichako
alisema: “Kwa kuanzia, Necta itafanya majaribio ya teknolojia hiyo mwakani na
ninaamini itaongeza ubora katika usahihishaji.”
“Kwa kutumia hii teknolojia msahihishaji hawezi kuona
namba ya mwanafunzi, anachoona ni sehemu ya swali anayotakiwa kusahihisha na
jibu lake, akimaliza swali moja jingine linakuja moja kwa moja,”
aliongeza.
Alisema kwa kutumia teknolojia hiyo, mratibu wa
usahihishaji anaweza kuona kazi inayofanywa na msahihishaji yeyote na hata
kuwapima kama atakuwa na wasiwasi wowote.
Alisema Zimbabwe imeanza kutumia teknolojia hiyo
aliyosema itasaidia kuongeza ubora katika suala la
usahihishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi
wa mkutano huo jana, alisema teknolojia ya OMR imeongeza ubora wa hali ya juu
kwenye mtihani wa darasa la saba pamoja na usahihishaji
wake.
“Watu wanasema kuwa mtihani wa maswali ya kuchagua ni
mrahisi, lakini hii siyo kweli, inatungwa na wataalamu na inalenga kumpima mtoto
katika kila nyanja, ndiyo maana hata mtihani wa darasa la saba mwaka jana
ilibidi Serikali ishushe alama za kwenda kidato cha kwanza zikawa 70 badala ya
100,” alisema Dk Ndalichako.
Akizungumzia teknolojia hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema wamebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya
nchi za Afrika zinatumia mfumo wa usahihishaji kwa OMR.
Alisema baadhi ya nchi zimeanza kusahihisha kwa kutumia
kompyuta hata katika maswali ya kujieleza na kuwataka Watanzania kuacha
kujirudisha nyuma.
Post a Comment