![]() |
| Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athumani |
Na..mkwinda.blogspot |
WAUMINI wa dini ya Kiislamu waliokuwa katika ibada ya Swala ya Idd El Fitri katika msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Wilayani Kyela mkoani Mbeya jana walikumbwa na taharuki baada ya Shekhe wao aliyekuwa akiongoza ibada kuvamiwa kibla wakati akiendesha ibada na kujeruhiwa.
Tukio hilo la aina yake limetokea majira ya asubuhi ambapo Shekhe huyo aliyetambuliwa kwa jina la Nuhu Mwafilango alishambuliwa akiwa katikati ya sijida baada ya mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa Kyela Ally Mwangosi kumpiga Shekhe huyo na kitu chenye ncha kali kichwani.
Taarifa kutoka msikitini hapo zinadai kuwa mara baada ya mwanafunzi huyo kupita upande wa Kibla na shekhe huyo na kupigwa chenye ncha kali alipiga ukelele wa kuomba msaada na hivyo kuibua taharuki miongoni wa waumini waliokuwa wakiswali msikitini hapo.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Wilayani Kyela Bw. Daudi Mwenda alisema kuwa mara baada ya Shekhe huyo kuvamiwa na kupigwa waumini walimuokoa na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Bw. Mwenda alisema kuwa Shekhe huyo ameumizwa vibaya eneo la kichwani ambapo damu nyingi zilivuja mara baada ya kupigwa na kwamba mbali na Shekhe huyo waumini wengine wawili waliokuwa wakijaribu kumuokoa walijeruhiwa kwa kuchomwa na visu.
Wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ni pamoja na mweka hazina wa BAKWATA wilaya Ustadhi Khamis Husein aliyejeruhiwa kichwani na sikioni.
Baadhi ya waumini waliokuwepo katika ibada hiyo walisema kuwa tukio hilo lilitokea wakati waumini wote wakiwa wamesujudu ndipo waliposikia kelele na vurugu ambapo aliinuka mtu mmoja aliyekuwa na kitu mfano wa nondo na kumpiga nayo Shekhe kichwani.Mmoja wa waumini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Husein alisema kuwa wakati kijana huyo aliyekuwa na kitu kinachofanana na nondo liliibuka kundi la watu wengine waliomsaidia na hivyo kuibuka vurugu kubwa iliyosababisha ibada ya swala ya Idd kuvunjika.
Akizungumzia tukio hilo Katibu wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Shekhe Juma Killah alisema kuwa vurugu hizo zimetokea katika swala ya Idd na wahusika wa vurugu hizo ni waislamu ambao wanaipinga BAKWATA.
‘’Hiki ni kikundi cha waislamu waliotoka Jijini Dar es salaam kimekuja huku na kimesambaa katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya kinashawishi watu kuipinga BAKWATA na kinafanya mambo ambayo BAKWATA hatukubaliani nayo,’’alisema Shekhe Killah.
Alisema kuwa kikundi hicho kilikuwa kikimtuhumu Shekhe wa Wilaya kuwa ni mshirikina na kwamba kutokana na hali hiyo hakupaswa kuongoza ibada msikitini na badala yake wao ndio waliopaswa kuongoza ibada msikitini hapo.
Kwa upande wake Shekhe wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Mohamed Mwansasu alisema kuwa kitendo hicho kimeudhalilisha Uislamu na kwamba kilichofanywa na kundi hilo la watu si mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo Shekhe Mwansasu alienda mbali zaidi na kusema kuwa katika kikundi hicho wapo baadhi ya waumini wanaodaiwa kuwa ni askari polisi ambapo inadaiwa kuwa katika moja ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita imamu aliyekuwa akiswalisha alivutwa kanzu yake na kutakiwa kutoka eneo la kuongozea ibada ili kuwapisha wao waendeshe ibada hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema kuwa watu sita wanashikiliwa na Polisi kufuatia vurugu hiyo iliyotokea majira ya saa 2:30 katika msikiti mkuu wa Ijumaa wakati wa swala ya Idd el Fitri.
Kamanda Diwani alisema kuwa kundi la waislamu wanaojiita kuwa ni wenye itikadi kali walivamia msikitini wakati waumini wengine wakiwa wameinama wakisujudu na kumvaa imamu kwa kumpiga kwa mateke na ngumi huku wakiwa na nondo, mikasi na visu.
Alisema waumini hao walikuwa na madai kuwa hawamtaki Shekhe huyo na kwamba uwezo wake ni mdogo katika dini.
Alisema kuwa Shekhe huyo aliokolewa na baadhi ya waislamu ambapo aliwataja walioshikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Mashaka Kassim(30)Issa Juma(37),Ahmed Kassim Magogo(35) Ibrahimu Shaaban(17) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela anayesoma kidato cha Nne,Ambokile Mwangosi,(19)mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Kyela, Sadick Abdul(28).
Kamanda Diwani alisema kuwa taratibu zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.
WILAYA YA KYELA - WATUHUMIWA SITA WADHIBITIWA NA WAUMINI KWA USHIRIKIANO NA MAKACHERO WA POLISI WALIPOTAKA KUANZISHA FUJO.
MNAMO TAREHE 09.08.2013 MAJIRA YA SAA 08:30HRS HUKO ENEO LA BONDENI KATIKA MSIKITI MKUU WA IJUMAA WILAYA YA KYELA MKOA WA MBEYA. NURU S/O MWAFILANGO,MIAKA 77,KYUSA,SHEKHE MKUU WA WILAYA YA KYELA, MKAZI WA BONDENI AKIWA ANAONGOZA IBADA YA SWALA YA IDD EL FITRI MSIKITINI HAPO ALIVAMIWA NA BAADHI YA WAUMINI WANAOJIITA WAISLAM WENYE ITIKADI KALI NA KUANZA KUMSHAMBULIA KWA KUTUMIA FIMBO,NONDO,MKASI NGUMI NA MATEKE SEHEMU MBALIMBALI ZA MWILI WAKE. CHANZO NI
MADAI KUWA HAWAMTAKI SHEKHE HUYO KWA MADAI KUWA HANA UWEZO. MBINU ILIYOTUMIKA NI KUMVAMIA MHANGA WAKATI WAUMINI WOTE WAKIWA WAMEINAMA WAKISWALI NA KUANZA KUMSHAMBULIA. MHANGA HAKUPATA MADHARA BAADA YA BAADHI YA WAUMINI WALIOSHIRIKIANA NA POLISI/MAKACHERO WA-KIISLAMU KUMUOKOA. KUFUATIA TUKIO HILO WATUHUMIWA SITA AMBAO WALIKUWA VINARA WA VURUGU HIZO WAMEKAMATWA AMBAO NI 1.MASHAKA S/O KHASIMU,MIAKA 30,MUHA,MKULIMA MKAZI WA NDANDALO 2. ISSA S/O JUMA, MIAKA 37, MRANGI, MKULIMA,MKAZI WA BONDENI 3.AHMED S/O KHASIMU @ MAGOGO,MIAKA 35,MPOGORO,MKULIMA/MGANGA WA KIENYEJI, MKAZI WA MBUGANI [ALIKUTWA NA MKASI] 4. IBRAHIM S/O SHABAN,MIAKA 17,KYUSA,MWANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI KYELA DAY KIDATO CHA NNE MKAZI WA NDANDALO [ALIKUTWA NA FIMBO KUBWA NA NDIYE ALIYEMNYANG’ANYA SHEKHE KIPAZA SAUTI] 5. AMBOKILE S/O MWANGOSI @ ALLY,MIAKA 19,KYUSA,MWANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI KYELA DAY KIDATO CHA TATU, MKAZI WA BONDENI [ALIKUTWA NA KIPANDE CHA NONDO] NA 6. SADICK S/O ABDUL, MIAKA 28, KYUSA, MKULIMA, MKAZI WA NDANDALO. TARATIBU ZINAFANYWA ILI WAFIKISHWE MAHAKAMANI. KATIKA TUKIO HILO HAMIS S/O HUSSEIN, MIAKA 50, KYUSA, MKULIMA, MKAZI WA BONDENI ALIPATA MAJERAHA KIDOGOKWA KUKATWA MKASI JUU YA SIKIO LA KUSHOTO WAKATI AKIWA KATIKA HARAKATI ZA KUMUOKOA MHANGA ASIPATE MADHARA NA AMEPATIWA MATIBABU NA KURUHUSIWA. HALI YA USALAMA NA AMANI ILIREJEA MUDA MFUPI NA WAUMINI WALIENDELEA NA IBADA YAO CHINI YA UONGOZI WA SHEKHE HUYO NA KUMALIZA SALAMA. HAKUNA UHARIBIFU WA MALI ULIOTOKEA. KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI DIWANI ATHUMANI ANATOA WITO KWA WAUMINI NA JAMII KWA UJUMLA KUTATUA MATATIZO/KERO/MALALAMIKO YAO KWA NJIA YA KUKAA KWENYE MEZA YA MAZUNGUMZO BAADA YA KUYAWASILISHA KATIKA MAMLAKA HUSIKA ILI KUEPUSHA MATATIZO YANAYOWEZA KUEPUKIKA. AIDHA ANASISITIZA KUWA KWA YEYOTE ATAKAYEJARIBU /ATAKAYEVUNJA SHERIA HATAFUMBIWA MACHO.
Imesainiwa na,
[ DIWANI ATHUMANI - ACP ]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.



Post a Comment