Ushiriki wa Tanzania katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani nchini DRC, unatokana na mgogoro kati ya Serikali DRC na waasi hususan kikundi cha waasi cha M23. Mgogoro huo ulianza mwezi Aprili 2012 ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika Jeshji la serikali ya DRC na kuanzisha mapigano hali iliyopelekea hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.
Kufuatia hali hiyo mbaya ya usalama, wakati wa kikao
cha International Conference on the Great Lakes Region kilichofanyika tarehe 12
Julai 2012 mjini Addis Ababa, Ethiopia, Mhe. Rais Joseph Kabila aliwasilisha
ombi kwa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu ambazo Rwanda, Uganda, Tanzania, na DRC
akaomba nchi wanachama wa Maziwa Makuu zisaidie kuwapokonya silaha waasi wa
M23.
Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu walikubaliana na ombi
hilo na kutoa maelekezo kwa Mawaziri wa Ulinzi ambao walikutana tarehe 01 hadi 2
Agosti 2012 na kujadili maelekezo ya Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu. Mawaziri wa
Ulinzi walikubaliana kuwa ni muhimu kwa vikundi vyote vya Waasi (ADF, FDLR na
M23) kushughulikiwa na wakawasilisha mapendekezo yao kwa Wakuu wa Nchi za
Maziwa Makuu.
Tarehe 7 Agosti 2012, Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu
walikutana tena mjini Kampala, Uganda na kupanga mkakati wa kuanzishwa kwa
‘Neutral Intervention Force (NIF)’ na nchi wanachama wa Nchi za Maziwa
Makuu zikaombwa kuchangia askari watakaounda ‘Neutral Intervention Force
(NIF)’ ambapo Tanzania iliombwa na ikahadi kuchangia kikosi kimoja. Kikao
hiki kilitoa maelekezo ya hatua inayofuata kwa Mawaziri wa Ulinzi wa Maziwa
Makuu.
Tarehe 7 hadi 8 Sep 2012, Mawaziri wa Ulinzi wa
maziwa Makuu, walikutana na kujadili utekelezaji wa uanzishwaji wa
‘Neutral Intervention Force (NIF)’. Wakaunda ‘Military Assessment Team
(MAT)’ kufanya tathmini ya tishio. Timu hiyo ililifanya tathmini na kuwasilisha
taarifa yake kwenye kikao cha Mawaziri wa Ulinzi kilichofanyika tarehe 25 Oktoba
2012 mjini Goma, DRC na baadaye taarifa hiyo iliwasilishwa kwa Wakuu wa Nchi za
Maziwa Makuu ambao waliagiza kushirikishwa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya
maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika(AU) na Umja wa Mataifa(UN)
ili kufanikisha mkakati huo.
Nchi wanachamma wa SADC na Nchi za Maziwa Mkuu kwa
pamoja walikubaliana na kupendekeza SADC Standby Brigade ipelekwe DRC kama
‘Neutral Intervention Force (NIF)’. Kufuatia ridhaa hiyo nchi wanachama
wa SADC ziliombwa kuchangia ambapo nchi mbalimbali wanachama zilikubali
kuchangia, lakini Umoja wa Mataifa(UN) ilizipitisha nchi za Tanzania, Afrika
Kusini na Malawi kuchangia askari nguvu ya Brigedi moja kuunda NIF ya
MONUSCO.
Aidha, Umoja wa Mataifa mwezi Januari 2013 uliridhia
mapendekezo ya Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu na Nchi wanachama wa SADC ya
kuundwa ‘Neutral Intervention Force (NIF)’ na kupelekwa DRC. Kufuatia
idhini hiyo tarehe 28 Machi 2013, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
lilipitisha Azimio (Resolution) namba 2098 (2013) na kutoa jukumu maalumu la
ulinzi wa amani nchini DRC, likijumuisha ushiriki wa Neutral Intervention
Force (NIF) kama sehemu ya MONUSCO, na ikaitwa ‘Force Intervention
Brigade (FIB)’ ambayo kikosi cha Tanzania ni sehemu ya Brigade
hiyo.
Kwa mantiki hiyo ieleweke kwamba, Kikosi cha Tanzania
kilichopo DRC ni sehemu ya SADC standby brigade iliyotoa mchango wake katika
Jeshi la Umoja wa Mataifa (MONUSCO). Kinafanya kazi chini ya Force
Commander, MONUSCO na majukumu yake ni:
- Kuzuia waasi kujitanua (Prevention of Expansion)
- Kuvunja nguvu za waasi (Neutralization)
- Kuwapokonya silaha makundi yote ya waasi.
Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko chini ya majeshi
ya Umoja wa Mataifa ya MONUSCO, inamanisha kuwa Operesheni hiyo ni ya Umoja wa
Mataifa, Tanzania haipigani na M-23 na haina tatizo na Rwanda kuhusiana
na Operesheni hiyo na ridhaa ya kikosi chetu kwenda DRC ilikubaliwa pia na
Rwanda, nchi ambayo ni mwanachama wa nchi za Maziwa Makuu. Aidha, Rwanda
imesaidia sana kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha watu, vifaa na zana
katika nchi yake kupeleka DRC.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi.
6/9/2013
6/9/2013
Dar es Salaam.
Post a Comment