
Kushoto ni Mjumbe wa baraza la mashehe
wilaya ya Arumeru, Haruna Hussein Lotta, pembeni ni viongozi wa zamani
wakikabidhiana rasmi ofisi (picha: JamiiBlog)
*******
BARAZA kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) limetatua mgogoro uliokuwepo kati yao na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Arumeru na Katibu wa Wilaya wa baraza hilo
baada ya kusimamishwa nafasi zao za uongozi kwa miezi saba.
Kaimu katibu wa (BAKWATA) mkoa wa Arusha, Abdallah Masoud alisema kuwa bazara hilo limefikia hatua ya kuwarudisha.
viongozi hao kwenye nafasi zao baada
ya kusimamishwa katika nafasi hizo kutokana na ukwiukaji wa sheria
walioufanya wakiwa madarakani kinyume cha sheria cha baraza hilo.
Alisema kuwa, baada ya baraza kuu
kukaa na kufanya vikao vyake, walipitia barua mbalimbali zilizoandikwa
na viongozi hao za kuomba kurudi katika nafasi hizo huku wakikiri
kutorudia tena makosa waliyofanya ndipo baraza hilo lilipopitia na
kuwarudisha tena katika nafasi.
'Sisi dini yetu inaturuhusu kusamehe
na kuwasikiliza watu mbalimbali katika shida zao ikiwemo kutatua
migogoro mbalimbali iliyopo katika misikiti yetu lengo likiwa ni
kuhakikisha kila mmoja wetu anaishi kwa amani na kuondoa tofauti
miongoni mwa waumini wetu kwani ndio lengo letu la kuleta amani kwa
waumini na viongozi wetu kwa ujumla' alisema Kaimu katibu huyo.
Masoud aliwataka viongozi hao pamoja
na mashehe mbalimbali kuhakikisha wanahubiri amani katika maeneo yao
sambamba na kuondoa migogoro iliyopo miongoni mwao na hatimaye kuweza
kuishi kwa amani na upendo ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Naye Mjumbe wa baraza la mashehe
wilaya ya Arumeru, Haruna Hussein Lotta alisema kuwa, aliwataka viongozi
mbalimbali wa dini hiyo kuacha majungu na unafiki badala kwani kwa
kufanya hivyo ndio wanazidi kuliharibu baraza hilo badala ya kulijenga.
Haruna alisema kuwa,waislamu wengi
sasa hivi wameishia kukaa na kupiga majungu na kusengenyana hali ambayo
inachangia kwa kiasi kikubwa sana kuleta mpasuko ndani ya baraza la
bakwata wilaya ya Arumeru.
Aliongeza kuwa, endapo viongozi wa
dini hiyo pamoja na waumini hawataepuka masengenyo na majungu katika
baraza hilo wataendelea kuwa na migogoro ambayo haitaisha, hivyo
kuwataka kukaa na kuacha tofauti zao kwa muda huu ambao viongozi
wamerudishwa katika nafasi zao na hivyo kulijenga baraza hilo ili lidumu
na kuwa na amani toafuti na ilivyokuwa hapo awali.
Aidha waliorudishwa katika nafasi zao
ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru ,Jumanne Zuberi na
katibu wa wilaya Ramadhani Kumallah ambapo aliyekuwa akikaimu nafasi
hiyo ya Mwenyekiti ni Yahaya Hajji na Katibu alikuwa Yahaya Mwengellah.


Post a Comment