Mshindi wa wanaume, Alphonce Felix akipongezwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Rais
mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi akimpongeza mshindi
wa kwanza wa mbio za Dar Rotary Marathon kwa upande wa wanawake, Sarah
Ramadhani.
Baadhi ya wanariadha wakichuana
katika mashindano ya mbio za Dar Rotary Marathon zilizofanyika jijini Dar es
Salaam juzi, zilizowashirikisha wanariadha kutoka nchi mbalimbali. (Na Mpiga
Picha Wetu)
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Shirikisho la Riadhaa Tanzania (RT), Tullo Chambo akiweka namba ya mkimbiaji Zhakia Mrisho.
Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA kutoka klabu ya Holili Youth Athletics Club ya Kilimanjaro,
Alphonce Felix na Sarah Ramadhani jana walitamba katika mbio za nusu marathoni
za Rotary Dar Marathoni.
Ushindi huo umewatoa kimasomaso Watanzania ambao mara nyingi wamekuwa
wakivurugwa na Wakenya katika mbio mbalimbali zinazoandaliwa nchini Tanzania.
Kwa upande wa wanaume Felix alikuwa wa kwanza kwa kutumia saa
01:03:00:79 wakati Ramadhani alitamba kwa upande wa wanawake kwa kutumia saa 01:13:41:39
na kila mmoja aliondoka na Sh. Milioni 2, saa ya mkononi na medali za dhahabu.
Mkenya Daniel Muindi alimaliza wa pili kwa kutumia saa 01:03:34:17 kwa
upande wa wanaume wakati kwa upande wa wanawake Mkenya mwingine Eunice Mutie
alimaliza wa pili kwa kutumia saa 01:16:29:81.
Mary Naali ambaye ni bingwa mtetezi wa mbio hizo alimaliza watatu kwa
kutumia saa 01:17:40:64.
Washindi wa pili wa mbio hizo kwa wanaume na wanawake kila mmoka
aliondoka na Sh. Milioni 1 na watatu Sh. 500,000.
Washindi walikabidhiwa zawadi zao na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ali
Hassan Mwinyi aliyekuwa mgeni rasmi katika mbio hizo ambazo washindi wan ne
hadi wa 10 kwa upande wa wanawake na wanaume, kila mmoja aliondoka na Sh.
100,000.
Felix akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mbio hizo
alisema kuwa, zilikuwa ngumu na alishinda kwa sababu amefanya mazoezi vizuri
katika kambi yao ya Holili mkoani Kilimanjaro.
Mbio hizo hufanyika kila mwaka Oktoba 14, ambayo ni Siku ya Kumbukumbu
ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye ni Rais wa Kwanza wa Tanzania.
Mwinyi akizungumza baada ya kukabidhi zawadi hizo alisema kuwa,
Watanzania lazima waenzi fikra za mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa akipiga vita
sana ubaguzi wa rangi, dini, ukabila na mambo mengine yanayopinga amani.
Post a Comment