
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye harambee hiyo, alisema kunahitajika mjadala mkubwa kuhusu elimu bora inayoongelea maisha ya sasa.
“Mimi nazungumza kila siku, lakini wananiona mwendawazimu, tunataka mtu akimaliza kidato cha nne, sita na chuo apate ajira. Tunashukuru Serikali ya CCM inatekeleza hilo, sehemu za vijijini shule zipo lakini hazina vifaa, napenda kusafiri kwa basi kwenda mikoani, nakutana na wanafunzi, najiuliza kama shule za Kata zisingekuwepo hawa wanafunzi wangekuwa wapi?” Alihoji Lowassa.
Harambee hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Mt. Antony jijini hapa, ililenga kuchangisha kiasi cha shilingi 429, 250,000, ambapo Lowassa alifanikiwa kuchangisha nusu ya lengo hilo ambacho ni kiasi cha Sh milioni 233,610 zikiwa ni pamoja na ahadi iliyotolewa ya ujenzi wa maktaba ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya shule 12 za Kata zilizo katika Tarafa hiyo.
Lowassa alisema shule nyingi za Kata, zinakabiliwa na upungufu wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia, hivyo aliwataka wadau wa elimu hasa wale wanaoishi kwenye shule zilizopo kwenye mazingira magumu, kujitokeza kufanikisha kukidhi viwango vya elimu.
“Wenzangu wa Dar es Salaam sawa na Monduli, kuchangia elimu ni tabu. Nawapongeza mna shule nzuri, lakini hali si nzuri, wanafunzi 90 mpaka 100 kwa darasa moja! Mkiendelea hivi mtabaki nyuma, nimekuja kujiunga nanyi kuboresha na kutekeleza sera ya Chama Cha Mapinduzi, wanaziita zangu lakini mimi ni mtekelezaji. Serikali imeahidi kuleta walimu,” alisema.
Awali katika risala zao walimu pamoja na wanafunzi wanaojumuisha muungano wa shule 12 za tarafa hiyo, ikiwemo Chamanzi, Changanyikeni, Mbande, Mbagala na Nzasa walisema shule hizo kwa pamoja zinakabiliwa na changamoto ikiwemo upungufu wa madawati 5050, viti na meza za walimu 337, vyumba vya madarasa 162, maabara 35, ukarabati wa madarasa 12, nyumba 90 za walimu pamoja na ujenzi wa uzio utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 1.3.
Naye, mwenyeji wa harambee hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile alisema tangu kuasisiwa kwa shule za kata kiwango cha elimu kimepanda kwa kiasi kikubwa.
“Shule hizi za Kata ziliasisiwa ukiwa Waziri Mkuu, takwimu zinaonyesha kutoka 2005 tulikuwa na shule 1000 sasa ni 5000, hongera sana tumepiga hatua, vyuo vikuu zaidi ya 50, Serikali imejitahidi kujenga shule nyingi, lakini tunataka kuboresha kwa madawati na vifaa,” alisema Dk. Ndugulile.
Alisema mji wa Kigamboni ni mkubwa na una wakazi zaidi ya laki saba, hali inayosababisha kuongeza madawati na hivi karibuni wanatarajia kuongeza madawati 200.
“Kigamboni ni Jimbo la pili kwa ukubwa, tunafuatilia kupata wilaya yetu, tunashukuru kwa kuja ungeweza kukataa kwa kuwa si jimbo lako, lakini umekuwa ‘Champion’,” alisema.
Wengine waliohudhuria na kuchagia katika harambee hiyo pamoja na kutoa ahadi ni Mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhresa ambaye alituma wawakilishi wake na kuchangia kiasi cha Sh milioni 10, hata hivyo, Lowassa aliwataka wahusika wa harambee hiyo kuwasiliana na mfanyabiashara huyo kwa nia ya kuziongeza ili zifikie milioni 50.
Pia alikuwepo Mbunge wa Temeke, Abass Mtemvu ambaye pia ni Mwenyekiti wa wabunge wa Dar es Salaam akiwa pamoja na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan ‘Zungu’ ambao walichangia kiasi cha Sh milioni 20.
RAI


Post a Comment