MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rosweeter
Kasikila (60), amejikuta kwenye kashfa nzito ya kufunga ndoa na kijana,
kinda wa miaka 26, Michael Christian.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa katika Kanisa la Tanzania Assembles of God
(TAG), linaloongoz
wa na Mchungaji Getrude Rwakatare ambaye pia ni
Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, imebaki kuwa gumzo na kuwaacha hoi
baadhi ya mawaziri, wabunge wanaoifahamu pamoja na majirani wanaoishi
na mbunge huyo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya wanandoa hao na majirani
wanaowazunguka, vililiambia gazeti hili kuwa ndoa hiyo ilifungwa
Septemba Mosi mwaka 2011, na imebaki kuwa siri kabla ya wawili hao
kukorogana.
Kabla ya wawili hao kuamua kufunga ndoa, mbunge huyo kutoka mkoani
Rukwa, mwenye makazi yake Bagamoyo mkoani Pwani, alikuwa akimtumia
Michael kwenye shughuli mbalimbali na muda wote alikuwa akiishi
nyumbani kwa mbunge huyo.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo ambaye ana familia ya watoto wawili ambao
kiumri wanalingana na Michael, alianza uhusiano wa kimapenzi na kijana
huyo kwa siri kubwa na baadaye alifanikiwa kumshawishi wafunge ndoa
huku akimuahidi kumpa huduma mbalimbali anazotaka.
Kwa mujibu wa habari hizo, wawili hao waliamua kufunga ndoa katika
Kanisa la TAG baada ya mbunge huyo kufanikiwa kumshawishi Mchungaji
Rwakatare kwamba ndoa hiyo itakuwa siri, hasa kutokana na tofauti ya
kiumri kati yao.
Hata hivyo ndoa hiyo kwa sasa imekumbwa na mgogoro mkubwa, huku
mbunge huyo akidaiwa kuzuia kila kitu cha mumewe huyo, hasa vyeti vyake
vya shule kama njia ya kumbana warudiane.
Siku ya harusi
Kwa mujibu wa mashuhuda wa harusi hiyo ya aina yake, mbunge na
kijana huyo walikwenda kanisani wakiwa wawili bila mashahidi kama
ilivyo kawaida, na ndoa hiyo ilifungwa katika ofisi ya kanisa na sio
ndani ya kanisa.
Mashahidi wa ndoa hiyo waliitwa hapo hapo kanisani na walisimamia na
kushuhudia utiaji saini wa cheti cha ndoa na kisha wanandoa hao
kutawanyika kwenda kwenye fungate (Honey Moon). Hakukuwa na sherehe baada ya kufungwa ndoa.
Inadaiwa kuwa hakukuwa na ndugu yeyote wa maharusi hao aliyeshuhudia
tukio hilo la kihistoria la wawili hao kuunganishwa na kuwa mwili
mmoja.
Kauli ya Bwana harusi
Tanzania Daima Jumatano, lilifanikiwa kumpata Michael, ambaye katika
mazungumzo yake alikiri kufunga ndoa na mbunge huyo Septemba Mosi
mwaka 2011, lakini kwa sasa wametengana kutokana na sababu ambazo
hakutaka kuziweka wazi.
“Mimi nadhani hili ni jambo binafsi, sio vizuri kulizungumza
hadharani ila kweli nilifunga naye ndoa maana inaonekana mnajua mambo
mengi kunihusu, na ni kweli kwa sasa tumeachana,” alisema kwa kifupi.
Alisema walikutana na mbunge huyo Bagamoyo wakati alipokuwa akifanya
mafunzo kwa vitendo katika hospitali ya wilaya hiyo kama muuguzi mkunga
wakati mbunge huyo akiwa muuguzi mkuu wa wilaya katika hospitali hiyo.
Alipoulizwa sababu za kukubali kufunga ndoa na mama wa umri wa miaka
60 wakati ana miaka 26 na sababu za ndoa hiyo kuvunjika, Michael
alisema ana historia ndefu katika maisha yake kwani alizaliwa yatima na
amekua na kulelewa kwa ufadhili wa kituo cha Safina Street Network.
“Katika mazingira niliyokulia, unaweza kujua kwanini nilikubali
kuingia kwenye ndoa hiyo. Sina ndugu hata wa kunishauri. Hata hivyo,
hayo tuyaache. Lakini ukweli ndio huo, lakini kwa sasa tumeachana, kila
mtu ana maisha yake,” alisema Michael kwa masikitiko.
Michael ambaye kwa sasa anasoma katika Chuo Kikuu cha Muhimbili, pia
alikiri kuwa mbunge huyo anashikilia vyeti vyote vya shule ambavyo
anavihitaji sana kwa ajili ya kusaka ajira baada ya kumaliza masomo
yake Muhimbili.
Alitaja sababu ya kuvunja ndoa hiyo kuwa ni manyanyaso kwa vile ni
mdogo na masikini kwani hakuwa na sauti na alibanwa kwa kila kitu kiasi
cha kukosa kabisa amani katika maisha yake.
“Kimsingi ndoa yangu na mama imevunjika na ilivunjikia mikononi mwa
Rwakatare wakati akijaribu kutusuluhisha, alinitaka nirudi kwa mama,
hapana, siko tayari na hapa nataka vyeti vyangu tu basi,” alisema
Michael.
Mbunge ang’aka
Kwa upande wake, mbunge huyo alipoulizwa, kwanza alikuwa mbogo na
kukataa katakata kuzungumza kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia jambo
hilo zito kwenye simu.
Mbunge huyo alikiri kuwapo kwa ndoa hiyo, lakini alipinga kwamba
haijavunjika na kumhoji mwandishi wa habari hizi kama anajua taratibu
za kuvunja ndoa.
“Michael kakuambia hiyo ndoa imevunjika? Wewe si unajua taratibu za
ndoa kuvunjika? Kwanza nimeshasema sitaki kuzungumzia suala hili kwenye
simu ukitaka tuonane kesho kwani kuna haraka gani? Jambo la haraka ni
la mjamzito kutaka kujifungua, lakini kama ni suala hilo hakuna sababu
ya uharaka,” alisema mbunge huyo.
Hata hivyo baada ya kubanwa, mbunge huyo alimtaka mwandishi wa habari
hizo kukutana naye katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya kupata ufafanuzi, lakini cha ajabu mwandishi alipofika
katika ofisi hizo hizo, mama huyo alizima simu yake na hakupatikana
tena.
Mchungaji Rwakatare
Alipotakiwa kuzungumzia ndoa hiyo, Mchungaji Rwakatare kwanza aling’aka kwamba hajawahi kufungisha ndoa ya aina hiyo.
Lakini alipobanwa alikiri kuikumbuka ndoa hiyo na kwamba ilifungishwa
na mchungaji wa kanisa lake, aliyemtaja kwa jina la Mchungaji
Mtetumo.
Alimtetea mchungaji wake kwamba alichokifanya ni kutimiza wajibu wake
wa kichungaji wa kufungisha ndoa, hasa kama wanandoa wametimiza
vigezo.
“Wajibu wa kanisa ni kufungisha ndoa, kama wanandoa wamekidhi vigezo
vya kanisa. Sio kazi ya kanisa kuwachagulia wachumba kwa maana hakukuwa
na sababu ya kuhoji umri wao, wala jambo lolote zaidi ya kufungisha
ndoa hiyo,” alisema Mchungaji Rwakatare. TANZANIA DAIMA.
Loading...
Post a Comment