Mama Salma Kikwete, akikata utepe kuzindua rasmi jengo la Wodi ya Watoto, katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa.
Mama Salma, akitembelea katika Wodi ya watoto.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimjulia hali mtoto Saimon Gamaya , mwenye umri wa
miezi 11 na nusu akiwa na Mama yake Vumilia Ernest aliyelazwa katika
jengo la wodi ya watoto akiwa anaumwa sikio na kuharisha. Jengo hilo
lilifunguliwa rasmi na Mama Salma. Picha na John Lukuwi
*******************************************************************
Na Anna Nkinda- Maelezo, Iringa
Wanawake
mkoani Iringa wametakiwa kuitumia Hospitali ya rufaa ya mkoa huo kupata
huduma ya uzazi pamoja na watoto wao na kuachana na tabia ya
kujifungulia majumbani, kupeleka watoto kwa waganga wa jadi kwa kudhani
kuwa magonjwa wanayoumwa hayawezi kutibika Hospitalini.
Wito
huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua
jengo la huduma za watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa
ambayo imejengwa kwa msaada wa Hospitali rafiki ya Vicenza iliyopo
katika mkoa wa Veneto nchini Italia.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) alisema kuna baadhi ya wazazi wakiona watoto afya za
watoto wao zinadhoofika ikiwa ni pamoja na kuumwa ugonjwa wa utapiamlo
wanadhani kuwa jirani zao wanawaonea wivu na kuwaroga na wanaona njia
sahihi ni kwenda kwa waganga wa jadi badala ya kuwapeleka Hospitali
ili wakaonane na wataalamu wa afya.
Alisema
vifo vya watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa sasa ni
54 katika kila watoto wanaozaliwa wakiwa hai 1000 na katika mkoa huo
idadi ya vifo hivyo ni watoto 20 kwa kila vizazi hai 1000 nia ya
Serikali ni kuhakikisha kuwa vifo hivyo vinapungua ili kuweza kufikia
malengo ya Maendeleo ya Milinia ifikapo mwaka 2015.
Aidha
Mama Kikwete pia aliwataka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na mazingira
yawatayowapeleka kupata maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi na kuwa
waaminifu katika ndoa zao na kwa wale ambao hawana ndoa watulie na
kujitunza huku wasubiri muda wao wa kuoa au kuolewa ukifika.
“Mkoa
huu maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) yako juu takwimu zinaonyesha
kuwa watu tisa kati ya 100 wanamaambukizi , hivyo basi nawasihi mjitunze
na kuheshimu ndoa zenu kwa kufanya hivyo hamtaweza kupata maambukizi ya
ugonjwa huu kirahisi ingawa unaweza ukapata kwa njia nyingi lakini
maambukizi mengi yanapatikana kwa njia ya kufanya mapenzi yasiyo
salama”, alisema Mama Kikwete.
Mkuu
wa mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma aliushukuru uongozi wa mkoa
wa Veneto na Hospitali ya Vicenza kwa msaada wa ujenzi wa wodi ya
watoto na ujenzi wa jengo la kujifungulia kina mama wajawazito.
Dkt.
Ishengoma aliahidi atahakikisha na kusimamia ili jengo hilo liweze
kutumika kama lilivyokusudiwa na wahudumu wa Hospitali hiyo waweze
kutoa huduma bora kwa wananchi wa mkoa wa Iringa.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa jengo hilo mganga mkuu wa mkoa Dkt. Robert Salim
alisema jengo hilo ni awamu ya pili ya ujenzi kwani awamu ya kwanza
ilikuwa ni ujenzi wa jengo la kujifungulia wajawazito ambalo kwa kiasi
kikubwa limeboresha huduma na kupuza vifo vya wazazi na watoto wachanga.
Dkt. Salim alisema lengo la kujengwa kwa wodi ya watoto ni kuboresha
huduma ya afya, kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka
mitano vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza na kupunguza msongamano
katika wodi ya watoto.
"Faida za mradi huu ni kuboresha utoaji wa huduma kwa urahisi kwa
watoto wagonjwa kwa kuwa na eneo kubwa la kufanyia kazi, kupunguza
msongamano na kutatua tatizo la wagonjwa kulala wawili wawili au zaidi
katika kitanda kimoja.
Pia
ni kupunguza maambukizi ya magonjwa kwa watoto waliolazwa , kuwa na
eneo la kutolea elimu ya lishe kwa watoto na kuwapatia watoto eneo la
michezo na kupenda kusoma", alisema Dkt. Salim.
Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Luigi Scotto aliwashukuru
watu wote waliohusika hadi kukamilika kwa mradi huo na kusema
anajivunia kuwa balozi katika nchi ya Tanzania yenye ambayo watu wake ni
wakarimu na wenye ushirikiano wa hali ya juu.
Kukamilika kwa mradi huu ambao ni moja ya kazi zinazofanywa na n chi
ya Itali hapa Tanzania inaonyesha mahusiano mazuri ya kirafiki ambayo
yalikuwepo kwa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili nitaendelea
kuhakikisha kuwa tunaimarisha sekta ya afya hapa nchini ili watanzania
wapate huduma bora”, alisema Balozi Scotto.
Naye Katibu Tawala (RAS) wa mkoa wa Veneto nchini Italia Roberto
Ciambetti alisema uhusiano kati ya hospitali ya Vicenta ya nchini humo
na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa mwaka 2003 ukiwa ni muendelezo
wa miradi iliyoanzishwa na shirika lisilo la kiserikali la “Doctor
with Africa CUAMM” la nchini humo.
Alisema
shirika la Doctor with Africa CUAMM linafanya shughuli mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kuandaa na kutengeneza miradi ya afya ya ushirikiano,
kuwaleta madaktari bingwa na wataalamu wengine wa afya katika nchi za
Afrika, kuwasomesha madaktari katika fani za afya, kufanya tafiti za
afya na kutekeleza program za uelimishaji jamii.
Alisema
Hospitali ya Vicenza imekamilisa miradi miwili na a Hospitali ya rufaa
ya Iringa ambayo malengo yake ni kutoa msaada wa kitaaluma ili
kuboresha ubora wa huduma, kuanzisha progeamu ya kubadilishana wataalamu
kati ya pande mbili ili kuboresha zinazotolewa.
Kuisaidia
Hospitali ya Rufaa ya mkoa kupata vifaa vya kisasa na vifaa tiba,
kuwasomesha watumishi wa hospitalikwenye fani mbalimbali ndani nan je ya
nchi na kuboresha miundombinu.
Hospitali
ya Rufaa ya Iringa inahudumia wakazi zaidi ya milioni moja na nusu wa
mkoa huo na Njombe pia ina uwezo wa kubeba vitanda 500 lakini vilivyopo
ni 455. Kwa sasa inatoa huduma za kawaida na huduma zinazohitajika
utaalamu zaidi kwa wagonjwa wanaopata rufaa kutoka hospitali za wilaya.
Wastani wa wagonjwa wanaotibiwa kwa mwezi ni 4310 na wanaolazwa kwa siku
ni 59.
Kukamilika
kwa mradi huo ni jitihada kubwa iliyofanywa na Baba Askofu wa jimbo
katoliki la Iringa Mhashamu Tarciusius Ngalalekumtwa pamoja na baraza la
maaskofu Tanzania (TEC) katika kuanzishwa kwa uhusiano wa Hospitali
hizo mbili na kupendekeza kwa wafadhili kuwepo kwa mradi wa kuboresha
huduma za Mama na mtoto ambao ulipata fedha za utekelezaji.
Mradi wa ujenzi wa wodi hiyo ya ghorofa moja lenye sehemu mbili za
kulaza wagonjwa ulianza mwaka 2010 na kukamilika 2012 umegharimu
shilingi bilioni moja milioni mia nane na arobaini na mbili ambazo
zimetolewa na Hospitali ya a Vicenza kwa upande wa ofisi ya Mkuu wa
mkoa imechangia shilingi milioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa mfumo wa maji
taka na kujenga mfumo wa umwagiliaji kwa kutumia maji ya kisima.
Post a Comment