Miss utalii Tanzania 2013, Hadija
Mswaga (kushoto) akiingia kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana, kuelekea Equatorial
Guinea kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya Miss
Tourisim World 2013, pembeni ni mshindi wa tatu, Teresia Kimolo.
aliyemsindikiza (Picha na Hosea Joseph)
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata),
limempa karipio kali Mwenyekiti wa shindano la Miss Utalii, Gideon
Chipungahelo kwa kosa la kudhalilisha baadhi ya washiriki na malalamiko
kufanyiwa kazi na Baraza hilo. Kalipio hilo lilitolewa baada ya Basata
kupitia tathmini iliyohusisha vipande vya matukio yaliyorekodiwa
(clips) na kujionea namna wasichana wanavyofanyiwa vitendo vya
udhalilishaji na Chipungahelo kwa kipindi cha kambi ya miezi mitatu.
Katika hafla ya upitiaji wa clips hizo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Basata, Ilala, jijini Dar es Salaam mbele ya Chipungahelo, ilionekana wazi wasichana kukosa uangalizi walipokuwa kambini, hivyo kuwepo kwa matukio mbalimbali yasiyofaa.
Akizungumza katika kikao hicho,
Mkuu wa kitengo cha Sanaa wa Basata, Nsao Shaluwa alisema baada ya
kupata malalamiko kuwa wasichana wanafanyiwa mambo yasiyofaa wakiwa
kambini, waliamua kuutafuta ukweli na kujiridhisha shindano hilo lina
ukakasi mwingi.
Alisema baada ya kukusanya baadhi
ya matukio katika kuthibitisha hali halisi iliyopo kwenye shindanohilo,
watapeleka vielelezo kwa Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana Michezo na
Utamaduni ili Chipungahelo ajadiliwe kwa kosa la kudhalilisha warembo
wa shindano hilo.
Alisema kwa kukosa matroni,
yaelezwa warembo walikuwa wakizurula kutwa nzima hadi usiku kwenye
gari huku kukiwa hakuna ratiba ya chakula ya kueleweka huku
wakifanyishwa mazoezi muda mrefu.
Mbali ya muda mrefu kuanzia saa 2
usiku hadi 9, pia walikuwa wakivaa viatu virefu, hivyo miguu kuvimba na
wakati mwingine walikuwa wakichapwa makofi na kulazimishwa mapenzi.
Aidha, Chipungahelo anakabiliwa na
shutuma ya kuwaweka mabini washiriki kwa muda wa miezi mitatu tofauti
na alivyoeleza Basata kuwa kambi ni ya wiki tatu.
Zaidi ya hapo, Chipungahelo
alishindwa kutoa zawadi kwa washindi wala kifuta jasho kwa washiriki
wengine huku mshindi wa mwaka 2013, akidaiwa kubebwa kwa hila.
Shaluwa alisema baada ya
malalamiko hayo kufikishwa kwao, waliamua kunyatia katika kambi yake
iliyokuwa na warembo saba ambayo pia Chipungahelo aliwaficha.
Baada ya kuwahoji washiriki,
walikiri kwamba walikuwa wakilala warembo saba, wengine watano katika
chumba kimoja na wengine wakilala chini huku wakila mlo mmoja tena
katika muda usiofaa.
“Warembo wengi wamekiri walikuwa wakifanyishwa mazoezi kwa muda mrefu huku wakiwa wamevaa viatu virefu,
“Tulikuwa tukifanyishwa mazoezi
kuanzia saa mbili usiku hadi saa tisa, tuna njaa na tulipolalamika,
baba alitutukana matuzi ya nguoni na kukashifu tupu zetu” mmoja wsa
warembo alisema katika CD ya Basata. Shaluwa anasema walipofika
Ikondolelo ambako kulikuwa na kambi ya awali, walizungumza na warembo
hao, lakini wakishindwa kusema ukweli mbele ya Chipungahelo.
Alisema walipowapa karatasi
kuandika kero zao, kila mtu aliandika jina na kusaini ambapo walieleza
mengi yaliyorekodiwa na wadau kuoneshwa mwishoni mwa wiki mbele ya
mwanasheria Ashura Mzava kutoka TAWLA.
Mzava alisema wazi kwa madudu yaliyopo kwenye shindano hilo, Chipungahelo anapaswa kushtakiwa kwa udhalilishaji.
Kashfa nyingine ni kitendo cha
Chipungahelo kutumia kiasi cha sh 200,000 ambazo zilitolewa na Mkuu wa
Wilaya Tanga Mjini, Halima Dendego ili washiriki waende saloon kabla
ya fainali.
“Baba ametunyanyasa sana hadi,
ametumia pesa tuliyopewa na mama Halima Dendego, lakini hapohapo
amekuwa akimpendelea mshiriki mwenzetu (jina tunalo), kwa vile alikuwa
na uhusiano naye wa kimapenzi,” alisema mmoja wa washiriki na kuongeza:
“Hata siku ile ya fainali,
alipokuja mpambaji kutoka Sofia Record, alimuita na kumvalisha nguo
nzuri pamoja na kumpamba tofauti na alivyovalisha washiriki wengine”
wamesema washiriki hao.
Wakati huohuo Mkurugenzi Msaidizi
wa Sanaa kutoka Wizarani, Leah Kihimbi alisema atalifikisha kwa
usahihi suala hilo katika ngazi ya juu akimtaka Chipungahelo
ajitayarishe kwa maamuzi yoyote.
Mshiriki pekee wa Miss Utalii 2013
aliyefika kwenye tahmini hiyo, ni Glory John aliyesema wazi shutuma
zote zilizoelezwa na wenzake dhidi ya Chipungahelo ni kweli.
“Tulipokuwa tunakwenda Mikumi ,
tulilala Morogoro, Baba (Chipungahelo) aliniita akaniambia nipande juu
katika chumba kimojawapo, nilipokwenda na kufungua mlango, nikakutana
na moshi wa ajabu nikashindwa kuvumilia nikatoka.
Akanifuata akinitaka nirudi
chmbani mle, nikagoma, nilipowaeleza wenzangu, walinieleza nilielekea
kunaswa kwenye mtego wake,” alisema Glory.
Naye Katibu Mtendaji BASATA
Godfrey Mngereza alisema, hilo ni suala nyeti linalogusa jinsia ya
kike, hivyo ni hatari kwa ustawi wa jamii.
Kupitia tathmini hiyo ya aina
yake, Basata itachunguza mazingira ya ushindi wa Miss Utalii mwaka
2013, ikibainika hakustahili, atavuliwa taji hilo ili iwe fundisho.
“Tabia hizi chafu zinatuchafua
hata sisi BASATA tunaonekana hatufanyi kazi sasa ndio tutaanza na Miss
Utalii na ikibidi kusiwe na shindano la aina yeyote kama mambo yenyewe
ni kudhalilishana,” alisema Mngereza.
Wadau wengine waliohudhuria
tathmini hiyo ni kutoka TAMWA, TAWLA,TGNP,THAWE, Polisi Jamii, Polisi
kutoka kituo cha Pangani Ilala, Dar es Salaam, Shirikisho la Sanaa na
Ufundi, Binti Leo na wengineo.
Shaluwa alisema suala hilo
litapelekwa ngazi za juu na vielelezo kuonesha wasichana wakieleza
yanayotokea kambini pamoja na maoni ya wadau yaliyorekodiwa.
Akizungumnzia tuhuma dhidi yake,
Chipungahelo alisema ni majungu yaliyopikwa na maadui zake ambao
walimpandikizia makahaba kwa lengo la kuchafua taswira ya shindano hilo
ili kummaliza, lakini aliomba radhi kwa dosari na mapungufu
yaliyojitokeza na kuahidi kuwa hazitajirudia tena.
Post a Comment