Vijana wachangishwa mamilioni kujiunga jeshi bandia
Walipigishwa kwata, wakakimbizwa mchakamchaka kijijini
DC afunguka, asema askari mstaafu wa JWTZ anahusika
****
Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni wilayani Butiama, na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Angelina Mabula.
Vyanzo kadhaa vya taarifa vimelidokeza
NIPASHE Jumapili kuwa katika tukio hilo, Afisa mstaafu wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Dickson Malemo, anatajwa kuwa mhusika wa
utapeli huo. Malemo anadaiwa kuutangazia umma kwa njia zisizo rasmi,
kuwa ametumwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa), Jumanne Sagini, aorodheshe majina ya vijana
wanaotaka kujiunga kwenye majeshi ya ulinzi na usalama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Afisa huyo,
aliifanya kazi hiyo pasipo kificho, akisema Sagini, ambaye anatokea
kitongoji cha Nyamimisye wilayani humo, amepata nafasi 21 za vijana
kujiunga kwenye majeshi hayo.
Hata hivyo, nafasi hizo hazikupaswa
kutolewa ‘mfano wa sadaka’, bali mhitaji alitakiwa kuchangia fedha
kuanzia Sh. 500,000 hadi zaidi ya Shilingi milioni moja ili kupata
nafasi hizo.
“Tulitangaziwa kwamba kuna nafasi za ajira
majeshini na watu waliokuwa na uwezo walitoa fedha ili vijana wao
waingizwe,” kilieleza chanzo kimoja katika kitongoji cha Nyamimisye.
Kutokana na `kiu ya ajira’ inayowakabili
vijana, baadhi ya wazazi, ndugu na jamaa wenye asili ya nje ya wilaya
hiyo na mkoa wa Mara, waliwasiliana na ndugu zao na kuwaleta Butiama ili
waorodheshwe.
Mbali na Malemo, mtuhumiwa mwingine
anatajwa kuwa ni Bwana Miti aliyetambulika kwa jina moja la Chikonya
wakati wengine wawili majina yao hayakujulikama mara moja.
IDADI ILIPOTIMIA
Taarifa zinaeleza kuwa, idadi ya vijana takribani 21 ilipotimia, huku Afisa huyo na wenzake wanaokadiriwa kuwa wanne, walifungua kambi hewa kijijini Butiama, na kutoa mafunzo ya awali kwa vijana waliojiandikisha.
Taarifa zinaeleza kuwa, idadi ya vijana takribani 21 ilipotimia, huku Afisa huyo na wenzake wanaokadiriwa kuwa wanne, walifungua kambi hewa kijijini Butiama, na kutoa mafunzo ya awali kwa vijana waliojiandikisha.
Vijana hao wanadaiwa kuwekwa kwenye nyumba
kadhaa zilizopo kijijini humo na nyakati za asubuhi, walikimbizwa
mchakamchaka hadi barabara kuu inayokwenda na kutoka Mwanza, eneo la
Nyamimisye.
“Tuliwaona vijana wakikimbia mchakamchaka
na waliporejea Butiama, tukaambiwa walikuwa wanapigishwa kwata,
walionekana kufurahia ajira kabla ya kuajiriwa,” kilieleza chanzo
kingine.
Ingawa ni hivyo, NIPASHE Jumapili
ilifanikiwa kuwapata baadhi ya vijana wanaotajwa kukabiliwa na kadhia
hiyo, lakini hawakuwa tayari kutajwa ama kunukuliwa gazetini.
“Tumeambiwa suala hili ni la hatari sana
kwa maisha yetu hasa kwa atakayebainika kuzungumzia mambo
yalivyotutokea,” alikaririwa mmoja wa vijana hao akisema.
SIRI ILIVYOFICHUKA
Kufichuka kwa kashfa hiyo kulitokea moja ya Jumapili zilizopita, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mabula, kumpa ‘lifti’ mmoja wa wazazi waliochangia fedha kwa ajili ya ‘ajira hewa’ hizo.
Kufichuka kwa kashfa hiyo kulitokea moja ya Jumapili zilizopita, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mabula, kumpa ‘lifti’ mmoja wa wazazi waliochangia fedha kwa ajili ya ‘ajira hewa’ hizo.
Wawili hao walikuwa wakitokea kusali kwenye Kanisa Katoliki, parokia ya Kiabakari wilayani.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, mzazi huyo
alimuuliza Mkuu wa wilaya kuhusu mipango ya safari ya vijana hao, kwa
vile wahusika walitangaza kuwa vijana hao wangesafirishwa na kiongozi
huyo.
Kuhoji kwa mzazi huyo, kunatajwa kufungua
njia ya kufichuka kwa kashfa hiyo ambapo Mabula, alichukua hatua ya
kufuatilia na kufanikisha kukamatwa watuhumiwa wanne.
MKUU WA WILAYA ‘AFUNGUKA’
Akithibitisha kuwapo kwa tukio hilo, Mabula, aliliambia gazeti hili kuwa Sajini (Katibu Mkuu-Tamisemi), alihusishwa kwa kutajwa na kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa alikuwa sehemu ya mpango huo.
Akithibitisha kuwapo kwa tukio hilo, Mabula, aliliambia gazeti hili kuwa Sajini (Katibu Mkuu-Tamisemi), alihusishwa kwa kutajwa na kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa alikuwa sehemu ya mpango huo.
“Jina la huyu Sagini limetumiwa na watu
kwa nia ovu lakini si kwamba amehusika, lakini mpaka sasa
tumeshawakamata watuhumiwa wanne na mmoja anatafutwa,” alisema.
Mabula, alisema kutumiwa kwa jina hilo kunatokana na jinsi kiongozi huyo, akiwa mwenyeji wa wilayani humo, anavyofahamika.
“Inaonekana watuhumiwa walitumia jina hilo kutaka kuaminiwa kirahisi ili wafanikishwe uovu wao,” alisema Mabula.
Kwa mujibu wa Mabula, uchunguzi wa awali
ulithibitisha kuwa kila kijana, alitozwa kuanzia Shilingi 500,000 hadi
zaidi ya milioni moja.
FAILI LAFIKISHWA KWA MWANASHERIA WA SERIKALI
Hata hivyo, Mabula, aliliambia gazeti hili
kwa njia ya simu jana, kuwa faili lenye tuhuma hizo limefikishwa kwa
Mwanasheria wa serikali, ili kuchukua hatua zinazostahili.
“Nimeambiwa na wasaidizi wangu kwamba faili lipo kwa Mwanasheria wa serikali na wakati wowote watafikishwa mahakamani,” alisema.
SAGINI ATOA TAMKO ZITO
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mjini
Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Juma Sagini alikiri
kupata taarifa hizo, ambapo alitaka watu wote waliohusika na utapeli
huo wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema yeye kama mtendaji wa serikali
mwenye wajibu wa kusukuma maendeleo ya Watanzania, hawezi kufanya
jambo hilo ambalo misingi yake ni kutapeli wananchi na kuchukua kidogo
walichochuma kwa jasho lao.
Sajini alisema alitaka wananchi wa Butiama
kutokubali kutoa pesa kwa jambo lolote linalohusu kupata ajira za
serikalini kwani wakati wa kufanya hivyo taratibu zote za kuajiri
zinawekwa wazi na hazihitaji kutoa rushwa.
“Niweke wazi kwamba walioibiwa pesa ni
wananchi wa kijiji nilipozaliwa, nimeumizwa sana siwezi kuwakandamiza
ndugu zangu hata kidogo, nataka watu hao waeleze nia yao ilikuwa nini,”
alisema Sagini kwa masikitiko.
Alisema anaamini hana maadui wa kisiasa
kwa sababu hana ndoto ya kugombea ubunge, bali watu hao ni sehemu ya
‘mtandao’ uliosambaa nchini wanaotumia majina ya viongozi kujipatia
pesa.
“Nashukuru DC ameniambia tayari baadhi wamekamatwa, wabanwe waseme kwa nini walifanya jambo hilo,” aliongeza kusema.
BAADHI YA MATUKIO YA UTAPELI WA AJIRA
Januari 11, mwaka huu, vijana zaidi ya 160
walitapeliwa fedha na madalali `wanaouza’ ajira katika ofisi nyeti za
serikali hasa zinazohusu ulinzi na usalama.
Matapeli hao wamekuwa wakiuza ajira za
Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Polisi na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Julai 13, mwaka huu, polisi mkoani Dodoma
iliwashikilia watu wawili waliokuwa wakitapeli wananchi kwa kutoa
vipeperushi vinavyoonesha nafasi za kazi mbalimbali za ajira kutoka kwa
kampuni inayojulikana kama Granton Market Dubai (BJM).
Zaidi ya watu 300 mkoani Dodoma na mikoa
mingine wanadaiwa kutapeliwa katika sakata la mlolongo wa kuahidiwa
ajira; huku mmoja wao akitapeliwa Sh 400,000.
*Taarifa hii imeandaliwa na Mashaka Mgeta na Moshi Lusonzo
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI



Post a Comment