Serikali imeshaanza kuchukua hatua baada ya nchi za Rwanda,
Kenya na Uganda kutoihusisha katika mambo yanayohusu Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), ikiwa ni pamoja na kutohudhuria mikutano ya jumuiya
hiyo yenye ajenda ambazo nchi hizo tatu zimekwishaweka msimamo wa peke
yao.
Nchi za Rwanda, Uganda na Kenya zimeanzisha
ushirikiano wa pamoja katika maeneo ya miundombinu, biashara na viza ya
pamoja na mara nyingi viongozi wakuu wa nchi hizo wamekuwa wakifanya
mikutano bila kuihusisha Tanzania na Burundi.
Serikali jana kupitia kwa Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta ilitoa ufafanuzi huo bungeni, baada ya
wabunge kutaka ieleze msimamo wake kuhusu suala hilo. Katika swali lake
la nyongeza, Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango alitaka kujua
msimamo wa Serikali baada ya kuwepo kwa dalili za kuvunjika kwa jumuiya
hiyo.
Katika ufafanuzi wake, Sitta alisema: “Si kwamba
Serikali imekaa kimya, kuna mambo mengine yanaendelea. Tumeanza kuchukua
hatua kuonyesha kuwa hatuwezi kuendelea na hali hii inayofanana na
mchezo wa kuigiza.”
Sitta alisema kuwa hivi sasa Serikali haitashiriki
katika mikutano ya jumuiya hiyo ambayo ajenda zake zinahusu mambo
ambayo nchi hizo tatu zimekubaliana peke yao. “Kuna mkutano jijini
Nairobi unaowahusisha mawaziri wa mambo ya nje, mamlaka kuu imeamua
kwamba waziri wetu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe asihudhurie,” alisema Sitta na kuongeza:
“Kama tunazungumza sera ya mambo ya nje na wenzetu
wanataka kuunda shirikisho bila kutushirikisha, haitakuwa na maana sisi
kwenda kukaa katika vikao ambavyo hayo yanayozungumzwa wao tayari
wamekwishayawekea msimamo.”
Alifafanua: “Tunachukua hatua na hatushiriki
katika vikao vyao, kama wao wamekubaliana, basi haipo sababu ya sisi
kwenda. Tunaitazama hali hii siku hadi siku.”
Alisema kuna mkutano unafanyika Burundi leo,
Serikali imemwagiza Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dk Abdullah Abdullah kutohudhuria, kwa maelezo kuwa ajenda za
mkutano huo zinahusu mambo ambayo tayari nchi hizo zimekubaliana.
“Katibu Mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki
anaondoka leo (jana) kwenda kuhudhuria mkutano huo. Tumetoa ushauri kwa
watendaji wa Serikali wanaohudhuria vikao ambavyo wanasiasa hawapo,
wasitoe msimamo wowote wa nchi, bali wasikilize na kuja kutueleza,”
alisema.
Alisema mpaka sasa Tanzania inatafuta ufafanuzi wa
suala hilo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwamba baada ya
wiki mbili yatatolewa majibu na Tanzania itachukua hatua.
Awali, katika maswali ya nyongeza Mbunge wa Mbinga
Magharibi (CCM), John Komba alihoji kwa nini Tanzania hailaani nchi
hizo kuanzisha jumuiya ndani ya jumuiya, huku akipendekeza Tanzania
iunde jumuiya mpya itakayozihusisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) na Burundi.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alitaka
kujua msimamo wa Tanzania kiuchumi iwapo jumuiya hiyo itavunjika, huku
akieleza kuwa tayari Kenya imekubaliana na Ethiopia na Sudan kwa ajili
ya kutumia nchi hizo kibiashara.
MWANANCHI
Post a Comment