Ndugu Nape, akizungumza leo |
NA Mwandishi Wetu
SIKU
moja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, kutoa taarifa
zinazoshutumu kuwa vyama vya siasa nchini havijafanyiwa ukaguzi wa
mahesabu kwa muda mrefu, CCM imeibuka na kuitwisha Chadema tuhuma hizo.
Imesema yenyewe (CCM) imekuwa ikiitika mwito wa sheria hiyo na kwamba
hesabu zake zimekuwa zikikaguliwa kwa miaka mingi sasa, hata kabla ya
kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa
NEC, Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye amesema, ni sahihi kwa hesabu za
vyama vya siasa kukagukiwa kwani ni kwa mujibu wa sheria, na ndiyo
sababu CCM imekua ikitekeleza sheria hiyo kwa miaka mingi hata kabla ya
kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Nape alisema, badala yake chama kinachopaswa kutiliwa shaka kuhusu
ukiukaji wa sheria hiyo, ni Chadema, chama ambacho alidai kimekuwa na
tabia ya kufanya mambo mengi kinyume cha sheria kwa kisingizio cha
mwavuli wa siasa.
"Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikiitekeleza sheria hii vizuri. Kwa mfano
hesabu za CCM zilikaguliwa na wakaguzi wa nje TAC (Tanzania Audit
Corporation) kuanzia mwaka wa Fedha 1977/1978 hadi mwaka 2002/2003.
Kuanzia mwaka 2003/2004 hadi 2010/2011 tulikaguliwa na TAC- Associates,
shirika hili linatokana na Tanzania Audit Corporation
lililobinafisishwa", alisema Nape.
Alisema, 29/01/2013 CCM iliandika barua yenye kumbukumbu CMM/F. 20/80/89
kuwasilisha rasimu ya hesabu za mwaka wa fedha wa 2011/2012 ili
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aipangie mkaguzi.
"Kufuatia barua hiyo, CAG alitupangia TAC-Associates kukagua hesabu hizo za mwaka 2011/2012.
Kwa kawaida muda wa wakaguzi ni miaka mitatu hivyo TAC- Associates
watakua wakaguzi wetu mpaka mwaka wa fedha wa 2013/2014, baada ya hapo
CAG anaweza kuteua wakaguzi wengine", alisema Nape.
Nape alisema, hesabu za CCM zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje TAC-
Associates mwaka wa fedha 2009/2010 na 2010/2011 zilikwishawasilishwa
kwa CAG na kwamba hesabu za mwaka wa fedha 2011/2012 bado ziko kwa
wakaguzi wa nje, wakishakamilisha nazo zitawasilishwa kwenye vikao vya
Chama na hatimaye kwa CAG.
Alifafanua kwamba, hesabu hizo zikikaguliwa kwa mujibu wa utaratibu,
anapelekewa CAG ambaye ndiye anazipeleka kwa Msajili wa vyama vya siasa.
Nape alisema kutokana na maelezo haya CCM haihusiki na agizo la PAC na
kama kamati ya bunge ikitaka CCM ipo tayari kwenda kukutana kamati hiyo,
huku CCM ikiwa na mahesabu yake yaliyokaguliwa.
"Mwito wetu kwa Zitto aanze kwa kutoa boriti kwenye jicho lake ndipo
aone kibanzi kwenye jicho la mwenzake. Tunaamini kwa sababu mbalimbali
zikiwemo za kuwa na vyanzo vya fedha visivyo visafi na tabia iliyokubuhu
ya kupenda kukiuka kila sheria nchini wakidhani ndio staili ya kujenga
chama chao, si ajabu kuwa Chadema wanaweza kuwa hawajakaguliwa kwa miaka
yote hiyo. Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama chake anapaswa
kuwajibika kwa hili, yeye na Chama chake", alisema Nape na kuongeza;
"Wote tunakumbuka kelele zilizopo mtaani juu ya matumizi mabaya ya
ruzuku zinazoelekezwa na Chadema na viongozi wake kutoka kwa wanachama
wao, hivyo si ajabu wakawa wanakiuka sheria hii na ndio chanzo cha
kelele hizo za wanachama wao".
Nape alitaka ikibainika kuwa ni kweli Chadema wamekiuka sheria hiyo
muhimu, basi viongozi wa vyama husika wawajibike kwa kuwa si busara kuwa
na viongozi wa kisiasa walikubuhu kwa kuvunja sheria za nchi na
kujificha chiniya mwamvuli wa siasa.
"Uvunjaji wa sheria hii kwa wenzetu sio kwa bahati mbaya kwani wamezoea
kutoheshimu sheria za nchi mpaka kufikia mahali pa kutangaza hadharani
kuwa wanatamani nchi isitawalike. Ni muhimu kujenga utamaduni", alisema
Nape.
Post a Comment