"Jamani pesa yenu iliyoibiwa hii
hapa," Ni kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa ACP Athmani Mungi
akiwaonyesha raia wa China maburungutu ya fedha zilizonusurika kutoka
kwa majambazi waliowateka na kuwapora raia wa China.
Fedha shilingi Milioni 80 ambazo
zimerejeshwa na jeshi la polisi kutoka mikononi wa majambazi wa tukio la
utekaji wa raia wa Kichina, waliovamiwa katika mlima wa Nyang'olo
mkoani Iringa.
Kamanda Mungi akiwa ameshika Silaha
aina ya ShortgunGreener ambayo imekatwa Mtutu (kitako) silaha iliyotupwa
na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi baada ya kuzidiwa nguvu na
askari polisi katika mapambano ya kuokoa fedha za raia wa China.
Mamilioni ya fedha yakiwa yameshikwa
na kamanda wa jeshi la Polisi mkoni Iringa, mara baada ya kusalimika
kutoka mikononi mwa majambazi, ambao walipora vitita vya fedha hizo
kutoka kwa raia wa China.
Raia wa China wakiwa na askari polisi
katika ukumbi wa ofisi ya kamanda wa jeshi la polisi wakipewa taarifa za
kupatikana kwa baadhi ya fedha zao na vifaa walivyoporwa na watu
wanaosadikika kuwa ni majambazi.
Raia wa China wakiwa katika ofisi ya
kamanda wa jeshi la Polisi mko wa Iringa, wakifurahia kuziona fedha zao
ambazo zilikuwa zimepolwa na majambazi katika mlima wa Nyang'olo Wilaya
ya Iringa, wengine ni askari wa jeshi la Polisi.
*******
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi,
wamewateka raia wanne wa China mkoani Iringa, na kisha kuwapora fedha,
zaidi ya shilingi Milioni 130 za Kitanzania, fedha za Kichina, pamoja na
vifaa mbalimbali zikiwemo simu tano katika mlima wa Nyang'oro uliopo
mkoani Iringa.
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa
jeshi la Polisi mkoani Iringa ACP Athmani Mungi amesema raia hao wa
china wa kampuni ya SIETCO, inayojenga barabara ya Iringa- Dodoma,
walikutwa na mkasa huo wakati wakirejea kutoka Iringa mjini, ambapo
msako mkali wa jeshi hilo umefanikisha kupatikana kwa shilingi Milioni
80.
ACP Mungi amesema wachina hao
walitekwa na kuporwa kiasi hicho cha fedha na vitu mbalimbali, mara
baada ya kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la Iringa, na
wakiwa katika gari lao aina ya Toyota yenye namba za usajili T. 335 CMX
lilizuiliwa na gari kubwa aina ya Lori katika mlima wa Nyang'olo huku
watu watano wenye siraha wakapora mfuko uliokuwa na fedha hizo.
Amesema majambazi hao walichukua pia
simu za mkononi tano na funguo za gari la wachina na kutokomea nalo
pamoja na kiasi hicho cha fedha cha shilingi Milioni 135, ambazo
walikuwa wanarudi
nazo katika kambi yao ya Mtera.
"Wachina hao walikuwa wametoka
kuchukua fedha hizo katika benki ya CRDB tawi la Iringa mjini bila kuwa
na ulinzi wowote wa askari Polisi, na walikuwa wanazipeleka katika kambi
yao iliyopo
Mtera," Alisema Mungi.
Amesema jeshi la polisi baada ya
kupata taarifa hiyo walifanya oparesheni la kuwasaka majambazi hao
mchana na usiku, kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vya tarafa ya
Isimani, ambapo zoezi hilo liliendelea mpaka siku ya tarehe 23 alfajiri
walipowaona majambazi hao.
"Oparesheni ya kuwasaka majambazi
waliofanya tukio hilo iliendelea usiku na mchana, askari polisi kwa
kushirikiana na wananchi, na alfajiri ya leo majira ya saa kumi askari
yaliyaona majambazi hayo na ndipo mapambano makali yalianza, huku
majambazi na askari wakirushiana risasi za moto," Alisema.
Pia amesema mapambano makali
yaliwachanganya majambazi hayo na kupelekea kutupa Silaha aina ya
Shortgun Greener iliyokuwa imekatwa Mtutu (Kitako) ikiwa na risasi moja
chemba, huku majambazi hayo yakitupa begi moja lililokutwa na shilingi
Milioni 80, na lingine likiwa na Biscuit na vitu vingine vya kichina.
Mungi amesema katika oparesheni hiyo
pia wamefanikiwa kumkatata jambazi mmoja ambaye hakutaka jina lake
litajwe kwa kuhofia kuharibu upelelezi wa kuwasaka majambazi wengine
wanne waliofanikiwa kutoroka.
Mungi amesema jambazi huyo amekamatwa
katika kijiji cha Itono akiwa katika gari aina ya Hiace na kukutwa na
Pochi ya wachina ambayo ilikuwa na vitu vilivyoibwa kwenye eneo la tukio
hilo la
utekaji.
"Vitu alivyokutwa navyo mtu
tuliyemkamata ni fedha za kichina zinazofahamika kama Yuan zikiwa 97,
nyingine ni fedha hizo hizo za kichina zinaitwa Jiao hizo zilikuwa tatu,
leseni ya udereva mali ya mchina Gang Cheng, Leseni ya udereva ya Hua
-Li-wei, Simu moja ya kichina pamoja na Vitambulisho vilivyoandikwa kwa
lugha ya Kichina," Alisema Mungi.
Aidha kamanda Mungi ametoa onyo kwa
majambazi kuacha mara moja uharifu kwa madai kuwa mkoa wa Iringa si
salama kwa majambazi na waharifu wa aina yoyote kwani hata wanaotoka nje
ya mkoa huo wakiingia kufanya uharifu hawatatoka salama, huku akiwaasa
wananchi kuacha mara moja kusafiri na fedha kiasi kikubwa pasipokuwa na
ulinzi wowote.
Pia Kamanda Mungi amewashukuru
wananchi walioshirikiana na jeshi la polisi katika kufanikisha zoezi la
kupatikana kwa fedha hizo, pamoja na baadhi ya vitu vya wachina hao.
Hata hivyo siku za hivi karibuni, gari
la kampuni ya E. Awadhi, kampuni inayojihusisha na usafirishaji wa
mafuta nchini Zambia na Malawi lilitekwa katika eneo la Igumbilo mjini
Iringa na kisha
watekaji kutoroka na gari ambalo
lilikuwa limejaza mafuta katika mataki yake, huku jeshi hilo
likifanikiwa kumnasa mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.
MWISHO
Chanzo:Oliver Motto
Post a Comment