Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Serikali: Pinda hashitakiki


UPANDE wa Jamhuri katika shauri linalomkabili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani) katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, umeeleza kwamba kanuni za Bunge zinamlinda kiongozi huyo kushtakiwa kortini. Ugumu wa Pinda kushitakiwa umekuja baada ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kueleza kuwa Pinda hawezi kushitakiwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Masaju alikosoa maombi ya walalamikaji wanaoitaka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imuamuru Pinda afute kauli yake akisema mahakama hiyo haina uwezo huo.

Masaju alidai hayo jana mahakamani hapo mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Kiongozi, Fakih Jundu, Dk. Fauz Twaib na Augustine Mwarija wakati akiwasilisha hoja tano za kupinga Pinda kushtakiwa.

Juni 20 mwaka huu akiwa katika mkutano wa 11 wa Bunge, Pinda alitoa kauli ya kuwataka polisi kuwapiga wananchi wanaokaidi maelekezo ya jeshi hilo, kauli ambayo imeonekana kukiuka misingi ya utawala bora na haki za binadamu.

“Madai dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yako mahakamani kimakosa, kwani yanakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 100 (1) na (2).



“Ibara hiyo inasomeka kwamba kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, mahakama au mahala penginepo nje ya Bunge.

“Bila kuathiri Katiba au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, mbunge yeyote hawezi kushtakiwa wala kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo alilosema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo,” Katiba inaeleza.

Masaju aliendelea kusema kwamba, msingi wa kesi hiyo umetokana na maneno yaliyozungumzwa bungeni, hivyo Pinda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mlele hawezi kushitakiwa kwa kusema maneno hayo akiwa ndani ya Bunge.

Masaju alitoa mifano ya kesi mbalimbali na maamuzi yaliyowahi kutolewa, ambapo kwa upande wa Jaji Katiti katika shauri mojawapo linalofanana na hilo alisema kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba, anakubali kwamba mahakama haina uwezo wa kusikiliza maombi ya aina hiyo.

“Kufungwa kwa mahakama si kwamba hakuna njia mbadala ya kudai haki kama mtu amekerwa na jambo fulani katika shughuli za Bunge, kanuni za kudumu za Bunge zimeweka utaratibu kwa wanaokiuka utaratibu ndani ya Bunge.

“Kuna Kanuni ya Bunge namba 71 na 73, zinatoa utaratibu wa nini kifanyike kwa madai yaliyotolewa, mbali na kanuni za kudumu za Bunge kuna Sheria ya Haki za Wabunge, Mamlaka na Kinga ya mwaka 1988, kifungu namba 12 kinatoa fursa ya namna ya kushughulikia makosa yanayofanyika bungeni.

“Sheria hiyo inalindwa na Ibara ya 101 ya Katiba inayosema kwamba Bunge kuweza kutunga sheria na kuweka masharti ya kuiwezesha mahakama na sheria kuhifadhi na kutilia nguvu uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu wa shughuli katika Bunge, kwa mujibu wa Ibara ya 100 uhuru huo umedhaminiwa na Katiba,” alidai Masaju.

Akizungumzia sababu namba tano ya kupinga Pinda kufuta kauli yake, Masaju alidai mahakama haina uwezo wa kumwamuru kufuta kauli yake kwa sababu mahakamani si bungeni.

“Haiwezekani Pinda kufuta kauli yake kwa sababu hapa si bungeni ni mahakamani, kuna utaratibu uliowekwa bungeni, mbunge anaweza kusimama na kuomba mbunge mwenzake afute kauli yake au athibitishe. Kanuni ya 71 imeweka utaratibu huo.

“Kila muhimili una utaratibu wake, jambo la muhimili mmoja haliwezi kupelekwa katika muhimili mwingine, walalamikaji wanachokifanya ni kupoteza muda wa mahakama, waheshimiwa majaji tunaomba madai yaliyopo mbele yenu yatupwe na waamuriwe kulipa gharama za kesi,” alidai Masaju.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha baadhi ya hoja na nyingine hawakuweza kumaliza kwa sababu ya muda, kesi iliahirishwa hadi Jumatatu ambapo watamalizia na kuwapa nafasi walalamikaji kujibu.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakidai kuwa Pinda amevunja Katiba ya nchi.

Mbali na Waziri Mkuu, mdaiwa mwingine katika shauri hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mdaiwa wa pili.

MTANZANIA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top