Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SPIKA MAKINDA AONJA JOTO YA JIWE

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Anna Makinda, kudai kuwa wanasiasa wengi walioshindwa kutetea ubunge wao wako hoi kifedha, huku wengine wakifikia hatua ya kubisha hodi ofisini kwake kuomba msaada, baadhi ya wabunge waliopita, wa sasa na wasomi wamemshukia wakisema kauli yake ililenga kuwadhalilisha.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema Makinda aliamua kuwadhalilisha wabunge na taasisi ya Bunge kwa ujumla kwa kujifanya anawalilia wale aliowaita omba omba.
Mbunge wa zamani wa Muleba Kaskazini, Ndimara Tegambwage (NCCR-Mageuzi 1995-2000), alisema kauli ya Spika kulinganisha kipato cha sasa cha wabunge ni fedheha kwa Watanzania wanaopata kipato cha chini.
Alisema ubunge ni kazi ya kujitolea na kwamba muda unapokwisha mhusika anapaswa kurudi katika shughuli yake ya awali kwa ajili ya kujipatia kipato.
Huku akionyesha furaha ya kicheko, Ndimara alisema wakati wao wakiwa wabunge walikuwa wakipata mshahara wa sh 200,000 kabla ya makato na kwamba baada ya makato walisaliwa na sh 80,000.

“Ubunge si kazi na hao wanaofanya kazi ya kuwapatia ajira wajue hivyo. Kwa maana leo hii ubunge umekuwa kimbilio la watu wasio na kazi, ambao lakini wana uwezo wa kupata fedha za mara moja za kuwaingiza katika nafasi hizo, hii si sawa, wajue wapo kwa ajili ya wananchi,” alisema.
Ndimara ambaye alipata kuwa Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi kabla ya kuachana na siasa na kurejea kwenye taaluma yake ya uandishi wa habari, aliongeza kuwa ni wakati wa Spika kujitokeza hadharani na kusema kiwango anachofikiria kuwa ni muafaka kwa wabunge ili wasihangaike baada ya muda wao wa uwakilishi kwisha.
Tumbo
Aliyekuwa Mbunge wa Kisesa (1995-2000), Erasto Tumbo (UDP), alisema Makinda amelewa madaraka na kuanza kutukana wabunge wote bila kuchambua.
Tumbo ambaye alikorofishana na mwenyekiti wa chama hicho, John Cheyo, hivyo kuvuliwa uanachama, uamuzi ambao ulimpotezea ubunge wake, alisema ni vema kiongozi huyo ajitokeze hadharani na kuwataja kwa majina wabunge wastaafu waliofika kwake kumlilia awasaidie.
“Awataje na sisi wabunge wa zamani tuguswe tuwasaidie wenzetu hao, kwa maana kama mtu ameshindwa kujipanga kwa maisha yake, asisingizie ubunge aliokuwa nao kuwa umemfanya kufika hapo alipo,” alisema.
Tumbo, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Uenezi wa CHADEMA, alisisitiza kuwa kama kauli ya Makinda inawalenga wabunge wa CCM angemuelewa badala ya kujumuisha wabunge wote.
“Ndani ya CCM kuanzia mchakato wa kuteuliwa kuwania nafasi ya ubunge unahusisha suala zima la rushwa, pia kwa sababau ya mazoea mabaya waliyonayo ya kutoa na kupokea rushwa ndiyo maana wanadhalilika na hawa anaowasema ni wa CCM tu walio na ukaribu naye,” alisema Tumbo.
Kimaro
Mbunge wa zamani wa Vunjo (2005-2010), Aloyce Kimaro (CCM), amemtaka Spika kuacha kuwaendekeza waliokuwa wabunge wanaofika ofisini kwake kumwomba fedha.
Kimaro ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita alianguka awali kwenye kura za maoni ndani ya chama, alisema kazi ya ubunge ni sawa na uchungaji ambao ni utumishi wa umma, hivyo hauna malipo makubwa kama wanavyofikiri wengine.
“Ubunge ni kazi ya kujitolea, kama kuna mtu anakwenda bungeni akitegemea kutengeneza fedha anakosea na akifanya hivyo, atashindwa kuwahudumia wananchi waliomchagua,” alisema.
Kimaro ambaye ni mfanyabiashara kwa sasa, aliwashauri wanaoshindwa kwenye ubunge kurejea kwenye shughuli zao za awali huku akisisitiza kwamba ubunge ni kazi ya kujitolea, hivyo lazima mbunge awe na shughuli nyingine za kumuingizia kipato.
Chegeni
Raphael Chegeni (CCM), ambaye alikuwa mbunge wa Busega hadi mwaka 2010, alisema kauli ya Spika ni ya kudhalilisha wabunge wa zamani na kwamba yeye binafsi hajawahi kwenda kuomba fedha kwake.
Chegeni ambaye aliangushwa kwenye kura za maoni na Dk. Titus Kamani, alifafanua kuwa hategemei kufanya hivyo na kushauri kwamba badala ya Spika kuwadhalilisha wabunge wote angepigania kuandaa mfumo mzuri zaidi wa malipo yao na kutaka wawe na mishahara mikubwa pamoja na mafao ya uzeeni.
Aliwataka wabunge wasiridhike na kiwango cha elimu walichonacho na badala yake waongeze taaluma nyingine ili waweze kufanya shughuli nyingine tofauti na siasa baada ya kumaliza utumishi wa kuwawakilisha wananchi.
Ntagazwa
Aliyewahi kuwa mbunge wa Muhambwe (CCM), Arcado Ntagazwa, na baadaye waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema kushindwa kujiandaa kwa wabunge wengi ndicho chanzo cha udhalilishwaji huo aliosema umefanywa na Spika.
Ntagazwa ambaye ameshika nyadhifa kadhaa kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza, ikiwamo ya naibu mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, aliongeza kuwa wakati wa utawala wa hayati Julius Nyerere, ubunge ulikuwa ni utumishi wa wananchi na kazi ya kujitolea tofauti na ilivyo sasa ambapo imegeuzwa ajira na njia ya kujipatia utajiri wa haraka.
“Kama wangefuata misingi ya utumishi wakaachana na tamaa pamoja na anasa, maisha baada ya ubunge yasingeishia kuwa ya ombaomba,” alisema Ntagazwa ambaye sasa ni kada wa CHADEMA ambaye aligombea ubunge Muhambwe 2010 na kuangushwa na Felix Mkosamali wa NCCR-Mageuzi.
Rajab Mohamed
Mbunge wa Ole, Rajab Mohamed Mbaruk (CUF), alisema badala ya Spika kuwapatia elimu ya ujasiriamali, akae na wabunge ili ajue sababu zinazowafanya wafikie kuwa ombaomba baada ya muda wa utumishi kwisha.
Alisema kujua tatizo ni msingi mzuri wa kutatua kuliko kuwaandaa kuwa wajasiriamali wakati tatizo linalowafikisha katika hali ya kuomba likiwa halijatatuliwa.
Kawawa
Naye Mbunge wa Namtumbo, Vitta Kawawa (CCM), alisema nafasi ya ubunge waliyonayo imekuwa kero kwa familia zao kutokana na kutumia muda mwingi kuwasaidia wananchi.
Alisema licha ya kuwapo kwa mfuko wa jimbo bado fedha hizo hazitoshelezi, hali inayowalazimu kutumia sehemu ya mishahara kwa ajili ya kutatua kero katika jamii.
Alisema hata mafao wanayopewa baada ya muda wa Bunge kwisha yanakuwa hayawasaidii kwa kuwa wengi wanakuwa wameshakopa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na wengine kufanyia kazi ya kampeni kwa uchaguzi ulio mbele yao.
Dk. Bana
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk. Benson Bana, alisema kauli ya Makinda inawadhalilisha wanaoomba.
“Si kauli ya kiungwana, sote tunajua kwamba ubunge ni utumishi wa umma na hakuna mtumishi wa umma ambaye mshahara wake unamtosha, sote tunafunga mikanda.
“Lakini pia na wabunge wetu wanatakiwa kutambua kwamba ubunge si kazi ya kudumu na haina pensheni, hivyo wajipange kama wanavyojipanga watumishi wengine wa umma,” alisema Dk. Bana.
TANZANIA DAIMA
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top