Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ILI
kujenga jamii bora na yenye kujua tamaduni zao, kunahitajika kuandaliwa
matamasha muhimu yenye dhamira ya kweli katika kona mbalimbali za nchi
yetu. Huo ni mpango mzuri na wenye tija.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, pichani.
Katika
suala hilo, wale wadau wanaotarajia au waliowahi kuandaa matamasha ya
aina hiyo ni dhahiri wanatakiwa waungwe mkono badala ya kukatishwa
tamaa.
Kwa
sasa, tamasha ambalo linatajwa katika vinywa vya watu wengi ni lile la
Handeni, linalotarajiwa kufanyika Desemba 14, wilayani Handeni mkoani
Tanga.
Tamasha
hilo la utamaduni na michezo linatambulika kwa jina la ‘Handeni Kwetu,’
jina lililotokana na mtandao ‘blog’ ya Handeni Kwetu.
Mratibu wa Tamasha la Handeni, Kambi Mbwana, pichani.
Vyovyote
litakavyotajwa na wadau wa matamasha duniani kote, ili mradi linatimiza
na kutoa majibu halisi ya namna ya kutangaza na kukuza utamaduni wa
Tanzania, si vibaya na njia ya kulitangaza mbele ya jamii.
Katika
mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii, mwishoni mwa wiki iliyopita,
Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, anasema kuwa lengo la
kuandaa tamasha hilo ni kushirikiana na serikali na wananchi wote kujua
mbinu imara za kuutangaza utamaduni wetu.
Anasema
kwa maeneo kama Handeni na kwingineko, kumekuwa na changamoto kubwa za
wananchi kuacha utamaduni wao na kufuata wa wenzao jambo linalotakiwa
lipingwe vikali.
“Nilikaa
chini na kutafakari namna gani ya kuwaunganisha watu wote katika tukio
moja na kuwa sehemu ya wao kuangalia ngoma zetu, nyimbo zetu na mbinu za
kijamii kwa ujumla wake.
“Naamini
katika umri wa taifa letu la Tanzania, kuna mengi yametokea na yaliwahi
kutokea hasa wakati wa ukoloni, hivyo naamini siku hiyo tutajua ni
kiasi gani watu wa asili ya Handeni walikuwa na mchango kwenye jamii
yao,” alisema Mbwana.
Mbwana
ambaye ni mwandishi wa habari na mmiliki wa ‘blog’ ya Handeni Kwetu
(www.handenikwetu.blogspot), anasema kwamba kwa kukutana watu wote ni
sehemu ya kuangalia namna ya kulitumikia taifa letu la Tanzania na
kubuni mbinu za kujikomboa kiuchumi.
Mdau
huyo wa mambo ya utamaduni, michezo na sanaa kwa ujumla wake ukiwamo
muziki, anasema kwamba Handeni ni miongoni mwa wilaya zenye changamoto
kubwa hivyo kuna haja ya wadau wote kukutana kwa pamoja na kuangalia
namna ya kuzitatua, hasa kwa kupitia tamasha hilo.
“Huu
si wakati wa kuangalia Mkuu wa Wilaya (DC) Muhingo Rweyemamu anafanya
nini au Mbunge Abdallah Kigoda na viongozi wote wa serikali, ila jambo
la muhimu ni kushirikiana nao kuleta maendeleo.
“Mtu
wa kwanza katika maendeleo ni mwananchi mwenyewe, hivyo naomba
kuwakaribisha Watanzania na hata wale wasiokuwa Watanzania kukutana
pamoja na sisi kwenye tamasha hili,” alisisitiza Mbwana.
Aidha,
Mbwana anatumia muda huo kuwaomba wadau wote, wakiwamo viongozi wa
serikali, mashirika na kampuni kujitokeza kudhamini tamasha hilo
litakalokuwa la aina yake.
Tamasha
la Utamaduni la Handeni Kwetu linafanyika kwa mara ya kwanza,
likipangwa kuanza saa tatu asubuhi hadi saa 12 jioni, ambapo vikundi
mbalimbali vya sanaa vitashiriki.
Ili
kuleta hali ya kimkoa, Mbwana anasema juhudi zinafanyika kupata vikundi
katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Tanga ili kuimba nao, kucheza nao na
kushiriki nao katika jambo la kimaendeleo.
Mdau
huyo wa habari anasema kwamba hadi sasa wadau kadhaa wamejitokeza
kudhamini tamasha hilo linalotikisa katika maeneo ya Handeni na Tanzania
kwa ujumla.
Anawataja
wadau hao kuwa ni pamoja na Yusuphed Mhandeni, ambaye ni Mchumi wa CCM
Kata ya Makumbusho kwa kupitia Kampuni yake ya Yusuphed Trans, yenye
magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda Mkata, wilayani Handeni, Grace
Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles
& Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, Country Business
Directory (CBD) na Michuzi Media Group.
Wengine
ni duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini
ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati
Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog na Taifa
Letu.com.
Mbwana
anasema kwamba kwa kupitia tamasha hili, wadau wote watapata fursa ya
kutangaza biashara zao, ukizingatia kuwa tamasha hili linatarajia
kukutanisha watu wengi zaidi sehemu moja.
“Tunaomba
udhamini kwa watu wote ili tushirikiane katika kufanikisha tamasha hili
la kihistoria, huku tukiamini kuwa wenzetu wa Kilindi, Korogwe tutakuwa
nao pamoja.
“Maandalizi
yanaendelea kuhakikisha kuwa tunafanya kitu cha tofauti katika tamasha
hilo, nikiamini kuwa mguso huu utaendelea kushika kasi na habari hizi
njema kuenea nchini kote,” alisema.
Mbwana
anasema kwamba wazo la kufanyika kwa tamasha hilo limepewa baraka na
viongozi wote, akiwamo DC Rweyemamu na Mbunge, Abdalah Kigoda, ambaye
pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
Anasema
kuwa kwa kufanyika kwa tamasha hili ni muendelezo wa mipango mingi
mizuri ya kimaendeleo itakayoandaliwa kwa kushirikiana na Watanzania
wote, hususan wananchi wa Handeni.
Mwisho
kabisa Mbwana alitumia muda huo kuwakumbusha wafanyabiashara mbalimbali
wilayani Handeni na Tanga kwa ujumla, kuingia moja kwa moja katika
tamasha hili la aina yake.


Post a Comment