Kaimu
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Bw. Mbaraka Batega(kushoto) akieleza
kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu udhibiti wa wahamiaji
haramu kwenye maeneo yaliyopo nje ya mikoa ya "operesheni kimbunga",
UDHIBITI WA WAHAMIAJI HARAMU KWENYE MAENEO YALIYOPO NJE YA MIKOA YA "OPERESHENI KIMBUNGA".
Idara ya Uhamiaji ni moja ya Vyombo
vya Ulinzi na Usalama vyenye jukumu la kuhakikisha kwamba Ulinzi na
Usalama wa nchi unaimarishwa. Katika kusimamia jukumu hilo kikamilifu,
Idara ya Uhamiaji inatekeleza majukumu makuu ya Msingi yafuatayo:(P.T)
i. Kuwezesha na kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu nchini
ii. Kutoa huduma ya pasipoti au hati nyingine za safari kwa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali.
iii. Kutoa huduma ya Vibali vya kuishi nchini pamoja na Pasi mbalimbali kwa wageni wanaokuja nchini kwa shughuli mbalimbali.
iv. Kufanya misako, doria, kubaini na kuwakamata wahamiaji haramu nchini na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
v. Kuratibu mchakato wa maombi ya
wageni wanaoomba uraia wa Tanzania na kumshauri ipasavyo Mhe. Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi kwa hatua ya uamuzi.
Majukumu hayo ndiyo yanaipatia Idara
ya uhamiaji wajibu wa kulinda na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi,
sambamba na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
Uwezeshaji na Udhibiti wa wahamiaji nchini
Tanzania ni nchi inayofahamika sana
duniani kwa ukarimu wa watu wake, ardhi yenye rutuba, rasilimali
mbalimbali na vivutio vingi vya aina yake kwa watalii. Tanzania pia
kutokana na historia yake ya amani na utulivu pamoja na imani ya
viongozi wake kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja, Tanzania
imekuwa ni kimbilio salama la wakimbizi wengi na wapigania uhuru kutoka
mataifa mbalimbali Barani Africa.
Tanzania pia inazidi kuwa kivutio kwa
wageni wengi kutokana na kuwa na fursa nyingi za uwekezaji katika sekta
mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, madini, utalii n.k. Hata hivyo, si
wageni wote wanaoingia nchini wanafuata taratibu za kiuhamiaji katika
kipindi chote cha kuwepo hapa nchini. Hivyo, Tanzania kama zilivyo nchi
nyingine duniani inakabiliwa na changamoto ya kuwepo wahamiaji haramu.
Wahamiaji haramu hao wanatokana na makundi makuu yafuatayo:
Wahamiaji haramu walioingia nchini kabla ya uhuru pamoja na vizazi vyao.
Wengi walikuja kama manamba katika
mashamba ya wakoloni. Ingawa wengi wao wamefariki, lakini vizazi vyao
bado vipo. Wahamiaji haramu wa aina hii wengi wanapatikana katika mikoa
mingi ya mpakani, Tanga, Pwani na Morogoro. Hawa kwa mujibu wa historia
yao ni miongoni mwa wahamiaji "walowezi" hapa nchini. Kazi kubwa
inayofanywa na Idara ya Uhamiaji ni kuwatambua, kuwaandikisha na baadae
kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu hatua za kuchukua.
Wahamiaji haramu wanaotokana na kuwepo kwa makambi ya wakimbizi na wapigania uhuru nchini.
Baada ya nchi nyingi kupata uhuru,
wapigania uhuru wengi waliondoka, lakini baadhi vizazi vyao bado vipo
hapa nchini na baadhi ya vizazi hivyo vinaishi isivyo halali nchini.
Aidha, wengine ni wale walioishi nchini kama wakimbizi na baadae
kutorejea nchini kwao pamoja na vizazi vyao. Wengi wa wahamiaji haramu
hao wapo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mtwara Ruvuma,
Morogoro.
Katika kuwashughulikia Wahamiaji
haramu wa aina hii, Idara imeweka utaratibu wa kuwatambua kwa
kuwaandikisha katika madaftari maalum ili kuwa na kumbu kumbu zao sahihi
na baadae kuishauri Serikali kuhusu hatua za kuchukua. Madaftari haya
yameisaidia Serikali kuwatambua Wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kagera
na Kigoma wakati wa Operesheni "Kimbunga" inayoendelea hadi sasa.
Wahamiaji wanaozidisha muda wa ruhusa ya kuwepo nchini.
Hawa ni Wahamiaji wanaoingia nchini
kihalali na kupewa muda maalum wa kuwepo nchini. Baadhi yao muda huo
unapokwisha hawaondoki, wanaendelea kuishi kwa kujificha na kuukimbia
mkono wa sheria. Wahamiaji haramu wa aina hii wanashughulikiwa kwa
kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na
kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa nchini.
Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Hawa ni wale ambao wanaingia nchini
bila kufuata taratibu zozote za Uhamiaji. Wengi wao wanatumia njia
zisizohalali wakati wa kuingia nchini. Kundi hili linahusisha Wahamiaji
haramu wengi waliopo katika maeneo ya mipaka yetu na nchi jirani pamoja
na makundi ya Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kutoka nchi za Pembe ya
Afrika (Somalia na Ethiopia).
Wahamiaji haramu wa aina hii
wanashughulikiwa kwa kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua kwa
mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa
nchini.
Udhibiti wa Wahamiaji haramu katika maeneo yaliyopo nje ya Mikoa ya "Operesheni Kimbunga"
Wakati wa utekelezaji wa agizo la Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la
kuwataka majambazi, majangili na wamiliki wa silaha kinyume cha sheria
kujisalimsha na Wahamiaji haramu walipo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma
na Geita kurudi nchini kwao kwa hiari, Idara ya Uhamiaji iliendelea na
shughuli za udhibiti wa wageni katika kipindi hicho kwenye Mikoa iliyopo
nje ya eneo la operesheni. Katika shughuli hizo za udhibiti wa wageni,
Jumla ya wahamiaji haramu 6,653 kutoka mataifa mbalimbali wamekamatwa na
kuchukuliwa hatua mbali kwa mujibu wa sheria. Mataifa ya Wahamiaji hao
haramu na idadi yao kwenye mabano ni kama ifuatavyo:- Malawi (3,778),
Burundi (696), Congo DRC (1,739), Kenya (147), Uganda (20), Pakistan
(12), Somalia (31), Nigeria (23) na Msumbiji (20). Wengine ni India
(16), China (09), Rwanda (40), Ethiopia (97), Komoro (10), Uturuki (03),
Afrika Kusini (02), Bukina Faso (01), Liberia (02), Italia (01),
Singapore (01), Libya (01), Bulgaria (01), Ghana (02) na Syria (01).
Wengi wa Wahamiaji haramu hao
wameondolewa nchini, wengine wamefikishwa mahakamani wakati wengine
uchunguzi dhidi yao bado unaendelea. Aidha, wapo walio halalisha ukaazi
wao nchini wakati wengine wameorodheshwa kwa ajili ya hatua zaidi.
Watanzania Wahamiaji haramu katika nchi nyingine.
Wakati Tanzania ikiendelea na udhibiti
wa Wahamiaji haramu nchini, takwimu zilizopo zonaonesha kwamba wapo
watanzania ambao nao wanakiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi
mbalimbali wanazokwenda, ikiwemo kuingia na kuishi katika nchi hizo
wakiwa Wahamiaji haramu.
Katika kipindi cha mwaka 2012, Jumla
ya watanzania 1,263 walirejeshwa nchini kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha, katika kipindi cha Januari-August, 2013 jumla ya watanzania 715
wamerejeshwa nchini kwa makosa ya kukiuka taratibu za Uhamiaji katika
nchi walizokwenda, hususan Afrika Kusini.
Kwa kuwa sasa tunaishi katika
ulimwengu ambao watu wanasafiri kutoka nchi moja hadi nyingine kuliko
kipindi chochote kile katika historia ya binadamu, tunapenda watanzania
nao wasafiri nje ya nchi kwa ajili ya kunufaika na fursa mbalimbali na
tumekuwa tukiwawezesha kufanya hivyo. Pamoja na nia hiyo njema ya
Serikali, tunatoa wito kwa watanzania wenzetu kuheshimu Sheria, Kanuni
na taratibu zilizopo katika nchi wanazo kwenda, kama ambavyo tunapenda
wageni nao waheshimu Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo hapa nchini.
Kufanya hivyo sio tu kwamba kutatujengea uaminifu na uadhilifu katika
jamii ya watu tunaoishi nao ugenini, bali pia kutajenga jina zuri na
heshma kwa nchi yetu miongoni mwa mataifa mengine.
Sote tufahamu kuwa hakuna nchi yoyote
duniani inayoweza kuvumilia Wahamiaji haramu, bila kujali wanatoka taifa
gani. Kila nchi inajitahidi kukabiliana na changamoto hii ya Wahamiaji
haramu. Tofauti ni mbinu zinazotumika kulingana na mazingira na uwezo wa
nchi husika. Ndio maana kwa mazingira ya jiografia ya nchi yetu,
mapambano dhidi ya Wahamiaji haramu ni endelevu bila kujali kama kuna
operesheni maalum au ni katika hali ya utendaji kazi wa kawaida.
Hitimisho:
Suala la ulinzi na usalama wa nchi
yetu ni la kila mwananchi. Vyombo vya Ulinzi na Usalama peke yake
haviwezi kutekeleza jukumu hili bila ushirikiano wa karibu na wananchi.
Wahamiaji haramu hawana kisiwa chao wenyewe, bali wanaishi ndani ya
jamii. Tunawashukuru wote waliotupatia ushirikiano katika kutekeleza
majukumu yetu na tunaomba tuendelee kushirikiana kuanzia mwananchi mmoja
mmoja, viongozi wa ngazi mbalimbali, wanahabari pamoja na vikundi
mbalimbali vya kijamii.
Post a Comment