Mbunge Henry Bellingham katikati akiwa na mfanyabiashara Byran Shand -kulia na mwenzake
……………………………………………………………………………………
Imeandaliwa kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy Macha
Wawekezaji wamehimizwa kutosikiliza propaganda za uongo kuhusu uporaji ardhi Tanzania na kuendeleza miradi ya kilimo nchini.
Akiongea
katika mkutano wa wafanyabiashara na viongozi wa taasisi, mashirika na
makampuni mbalimbali ya ukulima na mazao Uingereza na Tanzania, Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza alisisitiza
serikali iko tayari kumsaidia yeyote anayetaka kuchangia idara hii
muhimu ya uchumi.
Waziri
Chiza aliyewasili London Jumatatu, kwa ziara ya kiserikali ya siku
tano akiongoza msafara wa wanataaluma wa kilimo, alikuwa akijibu swali
lililoulizwa mara kadhaa kuhusu ugawaji ardhi Tanzania.
Alifafanua:
“ Lipo gazeti moja lilisema serikali imechukua hekta milioni tatu. Si
kweli. Ardhi iliyoshakaguliwa katika miaka miwili iliyopita si zaidi ya
hekta 4,000. Habari hizi zimesababisha Tanzania kuondolewa katika kundi
la nchi za kuwekeza kilimo. Hata wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya
kiserikali (NGOs) yanatangaza uongo huu ambao ni marudio tu ya mambo
yasiyo kweli yaliyoshazushwa zamani. Tafadhali njooni muongee na sisi
wizarani na serikalini au taasisi zinazoaminika kama SAGCOT.
Tutawaambia ukweli na kufanya nanyi kazi.”
Mkutano
husika ulifanyika ukumbi wa Reform Club mtaa wa Pall Mall, London, na
kuhusisha wafanyabiashara wenye shughuli za kilimo Tanzania, makampuni
makubwa yanayojishughulisha bara Asia, Afrika na Uingereza, mathalan
duka maarufu la Sainsburys.
Kati
ya wazungumzaji wakuu alikuwa Balozi wetu, Uingereza, Mhe Peter
Kallaghe aliyesisitiza sera ya Tanzania kuendeleza mahusiano ya
kibiashara badala ya kutegemea sana misaada ya kigeni; Rachel Turner
mkurugenzi wa tawi la Mashariki na Afrika ya kati, idara ya serikali ya
Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID); Afisa Mtendaji Mkuu wa
kituo cha mpango maalum wa uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini Tanzania (
SAGCOT), Geoffrey Kirenga na Profesa Peter Mahamudu Msolla, Mwenyekiti
wa Kamati ya Wabunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Katika
hotuba yake Waziri Chiza alifafanua malengo matatu muhimu kuhusu ziara
hii, yaani kuendeleza fursa ya kibiashara na uwezekaji, kujifunza
teknolojia zinazohitajika na kuwaeleza wakulima na wafanyabiashara mambo
takikana.
Msisitizo
wa uwekezaji kupitia sekta binafsi ulitolewa mfano mzuri na Bwana
Carter Coleman, Afisa Mtendaji wa Agrica linaloongoza mradi wa
kuendeleza hifadhi, misitu na kilimo bora Afrika Mashariki.
Coleman
ambaye amekuwa na mahusiano ya karibu na Tanzania toka 1987 alieleza
baadhi ya shida zinazokabili kilimo kwa kusisitiza kuwa “ kilimo Afrika
ni aghali kuliko sehemu nyingine zote duniani.”
Alitaja
baadhi ya matatizo makuu kuwa kupatikana kwa umeme, ghala na hifadhi za
mazao, matengenezo ya vifaa kama trekta, maradhi ya mimea na kujua
mbegu zipi zitumike wapi na vipi.
“Kutokana na hayo kitengo cha uwekezaji na biashara ya binafsi ni muhimu sana kuendeleza kilimo Afrika,” alikumbusha.
Mheshimiwa
Waziri Chiza anatazamiwa kukutana na Watanzania leo Jumatano katika
ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania London, uliomtayarishaji mkuu wa safari
hii nzima.
Post a Comment