Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Maghembe akisukuma maji katika kisima kilichopo kata ya
Mvomero, wakati wa ziara yake wilayani Mvomero huku akishuhudiwa na Diwani wa
Kata hiyo, Ally Masoud.
Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Maghembe akimsikiliza Mkandarasi Mshauri wa kampuni ya AAW ya
Misri, kuhusu ujenzi wa tanki la maji litakalojengwa katika mji mdogo wa
Turiani, Wilayani Mvomero. Tanki hilo likimalizika litahudumia wanachi wa mji
wa Turiani na maeneo ya jirani.
Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Maghembe akisikiliza maelezo ya ukarabati na upanuzi wa mtambo
wa kusafishia maji kutoka kwa Mkandarasi, Nicholaus Gerny alipotembelea
chujio la kusafishia maji la MORUWASA.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Morogoro (MORUWASA) wakimsikiliza
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe alipotembelea mamlaka hiyo kuona
uzalishaji wa maji kwa mji wa Morogoro, wakati wa ziara yake mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya
ya Kilombero, Hassan Elias Masala (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Wilaya ya
Gairo, Khanifa Karamagi (kushoto), akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa,
Elias Tarimo wakimsikiliza Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa
ziara yake (hayupo pichani) mkoani Morogoro kufuatilia utekelezaji wa miradi
ya maji.Picha zote na Dennis Henry-Wizara ya Maji
---
WAZIRI wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe
amewaagiza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji mkoani Morogoro,
kurejea katika maeneo ya ujenzi wa miradi “site” na kuendelea na kazi kulingana
na mikataba yao.
Hayo aliyasema, wakati wa ziara yake ya kikazi
ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo, ambapo alikuta baadhi
ya wakandarasi wamesimamisha kazi za ujenzi wa miradi wakati wamekwisha lipwa
madai yao yote kwa kazi walizokwisha fanya.
“Nawaagiza wakandarasi wote warejee katika
maeneo yao ya kazi na kukamilisha kazi hizo kwa muda uliopangwa kufuatana na
mikataba yao”, alisema Prof. Maghembe.
Wakandarasi hao wamepewa mpaka tarehe 15 mwezi
huu, wawe wamerejea na kuendelea na kazi za ujenzi wa miradi katika miji midogo
ya Kilosa, Turiani na Mvomero, kinyume na hapo Wizara itawanyang’anya kazi
hizo na kupewa wakandarasi wengine.
Kwa upande wa wakandarasi, wameahidi kurejea
kwenye site zao na kumuomba Waziri wa Maji kufikiria madai yao ya ongezeko la
gharama za vifaa na gharama nyingine za ujenzi.
Vile vile, Prof. Maghembe ameiagiza Mamlaka ya
Majisafi na Majitaka Morogoro (MORUWASA) kushirikiana na Ofisi ya Bonde la Maji
la Wami/ Ruvu katika kutunza vyanzo vya maji na si kulalamika kuwa vinaharibiwa
na shughuli za kibinadamu.
“Tumieni sheria za rasilimali za maji kulinda
vyanzo vya maji na si kulalamika kuwa vyanzo vya maji vinaharibiwa na
binadamu”, alisema Prof. Maghembe.
Awali, akisoma taarifa ya hali ya huduma ya maji
mjini, Mkurugenzi wa MORUWASA, John Mtaita, alimweleza Waziri kuwa uharibifu wa vyanzo vya maji
unaosababishwa na shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo unaathiri utoaji
wa huduma wakati wa kiangazi.
Mpaka kufikia Septemba mwaka huu asilimia 63 ya
wananchi waishio mkoani Morogoro ndio wanaopata huduma ya majisafi na salama,
huku lengo la mkoa ni kufikia asilimia 90 ifikapo 2015.
Post a Comment