Maulidi alitoweka ghafla Januari 1, 2011. Wazazi wake wanasema siku hiyo
aliondoka nyumbani asubuhi na kupeleka mbuzi malishoni, na kwamba siku
hiyo hakurudi, jambo lililowatia mashaka wazazi wake hivyo kuamua kutoa
taarifa polisi na kwa uongozi wa kijiji.PICHA|MAKTABA
******
Ni hivi karibuni, Mji wa Geita na maeneo jirani ulikubwa na
taharuki ya aina yake,pale mtoto Shabani Maulid (15) anaedaiwa kwamba
alifariki dunia miaka miaka mitatu iliyopita, alipoonekana akiwa hai
katika Kijiji cha 14 Kambarage, Mtaa wa Mbugani.
Tukio hilo lilizua hofu kwa wakazi wa Mji wa Geita
huku waliowengi wakitaka kujua mtoto huyo aliyekutwa amefariki dunia
baada ya kupotea kwa siku nne mwaka 2011 na mwili wake kuzikwa,
inakuwaje leo hii anaonekana akiwa hai?
Tukio hilo lililotokea Septemba mwaka huu
linashuhudiwa na wazazi wa Shaban, ndugu zake, jamaa na hata majirani wa
eneo hilo ambao pia wanahoji, je aliyezikwa wakati mwili wa mtoto huyo
ulipookotwa ni nani na je mwili wake uko kaburini au la?
Maswali haya na mengine, yalikosa majibu kwani
baada ya kuonekana kwake, Shaban hakuweza kuongea vizuri na alionekana
kutofahamu kabisa Kiswahili, lugha ambayo kabla ya kutoweka kwake
aliifahamu vyema. Wakati huu mtoto huyu anaongea Kiha, japo nayo kwa
tabu.
Hali hiyo iliwalazimisha wazazi wake kushirikiana
na Jeshi la Polisi kumpeleka Haospitali ya Wilaya ya Geita ili apatiwe
matibabu, lakini ni kama hawakuona mtoto wao akipata nafuu hivyo
waliondoka naye na kuamua kumpeleka Kigoma Kambako anapatiwa tiba za
jadi.
“Niliamua nimpeleke kwa waganga wa jadi huku
nyumbani Kigoma na sasa hali inaendelea vizuri kwani anaweza kuongea
japo ni kwa muda mfupi kisha hunyamaza”, alisema baba mzazi wa mtoto
huyo, Maulidi.
Shaban alikuwa wapi?
Shaban hivi sasa anaendelea vizuri na ‘tiba’
anayopata huko Kigoma na aliweza kuzungumza na gazeti hili kwa simu,
huku akieleza kutoweka kwake, pia huko alikokuwa kwa miaka mitatu, huku
akiweka bayana kwamba hivi sasa anawatambua vizuri
wazazi na ndugu zake.
Alisema anakumbuka Januari 1, 2011 aliondoka
nyumbani kwao na kuelekea malishoni kuchunga mbuzi, na wakati akiwa
machungani ghafla lilitokea kundi la watu ambalo lilimzunguka.
Shabani anasema katika kundi hilo alikuwamo
mwanamke ambaye hakumtaja kwa maelezo kwamba anashindwa kutamka jina
lake, ambaye alimshika mkono na kumtaka waondoke eneo hilo.
“Walikuja watu wengi wanaume kwa wanawake, ghaflla
walinizunguka na nikasikia kama kizunguzungu na akili yangu ikawa kama
imezubaa,”alisema Shaban na kuongeza kuwa baada ya watu hao kumzingira
walimwamuru aswage mbuzi zake na kuwarudisha nyumbani.
MWANANCHI


Post a Comment