Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaa kuhusu
mfumuko wa bei kwa Mwezi Oktoba 2013
…………………………………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
.Dar es salaam.
Hali
ya kuongezeka kwa bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula
katika maeneo mbalimbali nchini imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa
mfumuko wa bei.
Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam amesema
kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa Mwezi Oktoba 2013 umeongezeka hadi
kufikia asilimia 6.3 kutoka 6.1 za mwezi Septemba 2013 kutokana na kasi
ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma.
Amesema
kuwa hali ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula
majumbani na migahawani umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.3 kwa mwezi
Oktoba ikilinganishwa na asilimia 6.9 za mwezi Septemba, 2013.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula Kwesigabo ameeleza kuwa kumekuwa na
ongezeko dogo hadi asilimia 6.1 kwa mwezi Oktoba 21013 ukilinganisha na
asilimia 6.0 za mwezi Septemba.
Amefafanua
kuwa taarifa za matokeo ya mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi
zinaonyesha kuwa mwezi Oktoba ulikua asilimia 0.6 ikilinganishwa na
asilimia 0.5 za mwezi Septemba kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa
za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Amezitaja
baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka
kwa mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi kuwa ni pamoja na unga wa
mahindi kwa asilimia 1.5, unga wa Muhogo kwa silimia 3.5, nyama kwa
asilimia 1.2, kuku kwa asilimia 3.7, samaki wabichi kwa asilimia 4.1 na
kuku kwa asilimia 3.7.
Bidhaa
nyingine ni pamoja na samaki wakavu kwa asilimia 9.0, dagaa kwa
asilimia 2.5, maziwa ya ng’ombe kwa asilimia 1.2, matunda kwa asilimia
2.9, nazi kwa asilimia 2.6, viazi vitamu kwa asilimia 4.2 na asali kwa
asilimia 5.0.
Ameongeza
kuwa mchango wa bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kwa kiasi
kikubwa kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi ni pamoja na
mavazi ya watoto kwa asilimia 0.4, mafuta ya taa kwa asilimia 2.1 na
vifaa mbalimbali vya usafi ambavyo kwa ujumla wake ni aslimia 0.4.
Hata
hivyo kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa
uwezo wa shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii
umeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kipindi chote cha mwaka kuanzia
mwezi Januari hadi Oktoba 2013.
“Napenda
niwahakikishie kuwa fahirisi za bei za Taifa zimeonyesha kuwa na
mwelekeo imara kwa kipindi chote, kwa hiyo uwezo wa shilingi 100 ya
Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo
imara” amesema.
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya umefikia asilimia 7.76 kwa mwezi Oktoba 2013 huku
nchini Uganda Ukifikia asilimia 8.1 kwa mwezi Oktoba kutoka asilimia 8.0
za mwezi Septemba.
Post a Comment