Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

RAIS KIKWETE: TUNAJIPANGA UPYA KWA OPERESHENI TOKOMEZA MAJANGILI

tembo_675cc.jpg
Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imesitisha kwa muda Operesheni Tokomeza Ujangili ili iweze kujipanga upya.
Akilihutubia Bunge Mjini Dodoma jana, Rais Kikwete alisema uamuzi wa kuendesha operesheni hiyo ulikuwa sahihi kutokana na historia ya ujangili nchini, lakini kutokana na malalamiko yaliyoibuka baada ya operesheni hiyo kuanza yameilazimu kusitisha kwa muda.
Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wabunge, wanaharakati na wananchi dhidi ya askari waliokuwa wakiiendesha yakiwamo ya watu kujeruhiwa, kuchomewa nyumba, mifugo kuuawa, kupigwa na uporaji.
Operesheni hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa pamoja na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa).
Operesheni hiyo ilizuiwa baada ya suala hilo kutinga bungeni na watunga sheria hao kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kuungana wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mathayo David Mathayo wawajibike.
Rais Kikwete alisema hakukasirishwa na maoni ya wabunge kuhusu kuwapo kwa kasoro za utekelezaji wa operesheni hiyo iliyolenga kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori.
Alisema Tanzania ilikuwa na tembo 350,000 wakati inapata uhuru mwaka 1961 kabla ya ujangili kuibuka kati ya miaka ya 1970 na 1980.
Alisema sensa iliyofanyika mwaka 1989 ilibaini kubaki kwa tembo 55,000 tu nchini wakati Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa idadi kubwa ya wanyamapori hao.
"Baada ya hapo Serikali ilianzisha Operesheni Uhai iliyoongozwa na Kamanda wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Meja Jenerali John Walden ambaye ametangulia mbele za haki dhidi ya majangili. Tulifanikiwa kwani mwaka 2009 ilipofanyika sensa ya wanyama, ilibainika tembo walikuwa 110,000," alisema.
Alisema baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya la ujangili wa meno ya tembo... "Kati ya mwaka 2010 hadi Septemba 2013, meno ya tembo yaliyokamatwa ni 3,899 yenye uzito wa kilo 11,212. Pia vilikamatwa vipande 22 vya meno vilivyochakatwa kuwa fimbo na urembo ambavyo vilikuwa na uzito wa kilo 3,978." Alisema pia vilikamatwa vipande 4,692 vya meno ya tembo vikiwa vimetoroshwa nje ya nchi vikiwa na uzito wa kilo 17,797... "Hapo unazungumzia zaidi ya kilo 36,000, sawa na zaidi ya tembo 15,000.
"Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa kulingana na manufaa yaliyopatikana katika operesheni zilizopita. Tusipochukua hatua ni sawa na kuwapa kibali majangili kuua tembo. Wanyama watakwisha na historia itatuhukumu vibaya."
Alisema Serikali itazingatia maoni ya wabunge kuhusu operesheni hiyo na kurekebisha dosari zilizojitokeza. "Serikali itachukua hatua dhidi ya watendaji wasiokuwa waadilifu na wasiokuwa waaminifu wataondolewa, kasoro za kimfumo nazo zitasahihishwa ili tukianza upya operesheni itekelezwe kwa mafanikio yaliyokusudiwa," aliongeza.
JK afagilia wanajeshi walioko Congo
Rais Kikwete pia amekipongeza kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichoko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kwa kuonyesha weledi mkubwa na kusaidia kusambaratisha Kundi la Waasi wa M23.
Wanajeshi hao ni sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani Kongo (Monusco) ambacho kilipewa kazi ya kusambaratisha na kuvipokonya silaha vikundi vinavyoendesha uasi nchini humo.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine ambazo zimepeleka askari wake katika kikosi hicho ni Afrika Kusini na Malawi.
Rais Kikwete alisema kikosi hicho kinachoongozwa na Brigedia Jenerali, James Mwakibolwa wa JWTZ kimefanya kazi kwa weledi mkubwa katika mapambano hayo na kuiletea sifa Tanzania.
Alisema jeshi hilo lilikwenda DRC baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa.
"Kuna sura mbili za sheria inayoongoza vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa kuna 'Chapter 6' (Sura ya sita) na 'Chapter 7'(Sura ya Saba)," alisema Rais Kikwete.
Alisema sura ya sita ya sheria hiyo inakataza majeshi hayo kupigana hata kama yatashambuliwa kama ilivyotokea kwa wanajeshi wa Tanzania walioko Darfur, isipokuwa kujihami tu.
"Ila ile 'Chapter 7' inaruhusu kupigana kama ikitokea ulazima wa kufanya hivyo. Majeshi yetu yako Kongo kwa sura hiyo," alifafanua Rais Kikwete.
Kikwete alisema mapigano ya Kongo yalisababisha wanajeshi watatu wa Tanzania wapoteze maisha... "Tutawakumbuka daima mashujaa wetu hawa kwa utumishi wao uliotukuka."
Rais Kikwete pia alimpongeza Rais wa DRC, Joseph Kabila kwa ushindi huo na kutaka aendelee kuijenga nchi hiyo katika harakati zake za kusaka amani kwa kuyaunganisha makundi yote yanayovutana nchini humo.
Chanzo:Mwananchi
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top