Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya.PICHA|MAKTABA
*****
Serikali imesema kuwa mgomo wa wafanyabiashara hauwezi kubadili
uamuzi wake wa kukusanya kodi kupitia mashine za elektroniki za EFD na
imewataka wafanyabiashara hao kufungua maduka yao kwa sababu hata
wakiyafunga watatakiwa kuwa nazo.
Hatua hiyo ya Serikali imekuja ikiwa ni siku ya
pili tangu wafanyabiashara hao walipogoma kufungua maduka wakipinga
kutumia mfumo huo wa ulipaji kodi.
Aidha, imeliagiza Jeshi la Polisi kusaka
wafanyabiashara wanaotishia usalama wa mali za wenzao wakiwashinikiza
kugoma kwa kisingizio cha kupinga matumizi ya mashine hizo.
Hata hivyo, Serikali imesikia kilio cha
wafanyabiashara hao kuhusu bei ya mashine hizo na imetangaza kupunguza
na sasa zitauzwa kati ya Sh600,000 hadi Sh778,000 badala ya Sh800,000
hadi 1.5milioni.
Wakizungumza kuhusu suala hilo kwa nyakati tofauti
jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene
waliwataka wafanyabiashara kuacha mgomo kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Waziri Mkuu alisema kuwa mashine hizo zilizotolewa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iko sahihi kabisa na kuwa haiwezi
kuacha kukusanya mapato kwa njia ya mashine hizo.
Akizindua miradi wa maji katika Shule ya Msingi
Olomitu, Kata ya Mlangarini, Arusha, Pinda alisema mashine hizo hazina
tatizo na kwamba TRA haina mpango wa kubadili msimamo wake wa kuzitumia.
Mbali ya uamuzi wa kupunguza bei, Waziri Mkuu
alisema wafanyabiashara wanapaswa kukumbuka kuwa gharama za ununuaji wa
mashine hizo mwishowe zitabebwa na TRA kwani watarudishiwa fedha hizo
kadri watakavyokuwa wanazitumia kwa mfumo wa makato.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mbene alisema:
“Hawa waliogoma si kweli kwamba hawajapata elimu kuhusiana na utumiaji
wa mashine hizo ila kuna waliopata elimu na kupata msukumo kutoka kwa
wenzao na wengine walipata elimu hiyo lakini haikuwasaidia.”
“Mgomo huu umeleta usumbufu mkubwa siyo hapa
nchini tu, bali hata katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa wale
wanaotegemea maduka hayo.”
Naibu wa waziri huyo alisema Serikali kupita TRA,
ilianzisha mashine hizo kwa lengo la kuondoa usumbufu wa wafanyabiashara
kukatwa kodi kubwa kwa kukisia, kumrahisishia mfanyabiashara kutunza
kumbukumbu na kuondoa usumbufu wa kukisia kukata kodi.
Akizungumzia mgomo huo Mbene alisema: “Tumegawana
majukumu. Sisi tumeshawabaini ni wafanyabiashara wakubwa tena wala
hawatoki hapa Dar es Salaam, hawa ni wakwepa kodi, wanaamua kutumia
nguvu yao ya fedha kuwalazimisha wenzao kugoma tena kwa kuwatishia
tumeshawasiliana na polisi kwa hatua za kisheria.”
MWANANCHI


Post a Comment