Profesa Muhongo alisema katika kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania wote, serikali imeanza mchakato wa kuwanyang’anya vitalu wamiliki wanaoonekana kusuasua kuviendeleza na kuwapatia wachimbaji wadogo.
“Serikali imeanza kusikiliza kilio cha wachimbaji wadogo kwa kutenga maeneo mbalimbali ambayo yatarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali, ikiwamo kupatiwa mikopo na vifaa,” alisema.
Akizungumzia suala la ununuzi wa mgodi huo, Profesa Muhongo alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha STAMICO inaimarika kwa kuanzisha kampuni mbalimbali.
“STAMICO itachukua mgodi wa dhahabu wa Tulawaka na baadhi ya leseni za utafutaji wa madini zinazozunguka eneo la mgodi kwa gharama ya dola za Marekani milioni 4.5.
“Kama sehemu ya makubaliano hayo, shirika litachukua umiliki na usimamizi wa mfuko wa fedha za ukarabati wa mazingira, ikiwa kama sehemu ya mpango wa ufungaji wa mgodi huo,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Gary Mwakalukwa, alisema kutokana na makubaliano hayo, Watanzania pia wataweza kununua hisa za kampuni hiyo.
“Kwa sababu ndani ya Stamico, tutaunda kampuni ya serikali ya madini itakayoitwa Stamigol, ambayo itashughulikia kusimamia shughuli zote za mgodi huo wa dhahabu,” alisema.
Naye Makamu wa Rais wa ABG, Deo Mwanyika, alisema Tulawaka ulikuwa ni mgodi wenye mafanikio makubwa kwa kampuni hiyo, hivyo makubaliano hayo ya biashara na STAMICO ni fursa ya kuendeleza sekta ya madini nchini.
RAI


Post a Comment