Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Jengo jipya la Skuli ya
Maandalizi ya Kikosi cha 14 cha Ali Khamis cha JWTZ Vitongoji Chake
chake Pemba.
Nyuma ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba akiwa pia Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi.
Mkuu wa Kikosi cha 14 Kambi ya Ali
Khamis Vitongoji Chake chake Pemba Luteni Kanali Julius Khombwe Mbwero
akimpatia maelezo ya ujenzi wa Majengo ya Skuli ya Ali Khamis Kamp
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyetembelea
majengo hayo mara baada ya kuweko jiwe la msingi ya jengo jipya la skuli
ya Maandalizi ya skuli hiyo.
Kushoto yake ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi na Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Bibi Mwanajuma Majid.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Skuli ya Kambi ya Ali Khamis Vitongoji Ridhiwan Khalfan Hamad mara baada ya kumwaga kimombo { Kiiingereza } wakati akiwasilisha Risala ya wanafunzi hao.
Balozi Seif akiikagua Hospitali ya Jeshi la Ulinzi wa Tanzania { JWTZ } ya Kikosi cha 14 Viongoji Pemba mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Skuli ya Kikosi hicho.
Picha no:- 105 ni:-
Balozi Seif akiuahidi Uongozi wa Kikosi cha 14 Vitongoji kwamba Serikali
ya SMZ itajipanga kusaidia baadhi ya vifaa, watendaji hospitali hiyo ili itoe huduma bora zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif akiagana na Mkuu wa Kikosi cha 14 cha Ali Khamis Vitongoji
Chake chake Pemba baada ya kuweka jiwe la msingi la skuli ya maandalizi
ya kikosi hicho pamoja na kutembelea Hospitali yaKambi hiyo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Uwamuzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Kikosi cha 14 cha
Ali Khamis kiliopo Vitongoji Chake chake Kisiwani Pemba wa kuanzisha
Skuli ya Maandalizi, Msingi na hatimae melekeo wa Sekondari umesaidia
kuunga mkono azma ya Serikali kupitia Sera ya Elimu ya kulenga kuwapatia
Elimiu ya lazima watoto wote wa Taifa hili.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kuweka
jiwe la msingi la Jengo Jipya la Skuli ya Maandalizi ya Ali Khamis Camp
iliyoanzishwa na Makamanda na wapiganaji wa Kikosi hicho cha 14
Vitongoji hafla ambayo ilipata Baraka pia na wazazi na wanafunzi wa
Skuli hiyo.
Balozi Seif alisema jamii inafahamu juhudi
kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ
} katika kusaidia masuala ya Kijamii katika wakati wa amani jambo ambao
huleta faraja kwa wananchi wanaozizunguuka kambi za Jeshi hilo katika
maeneo mbali mbali Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar alikipongeza Kikosi hicho cha 14 cha Ali Khamis kiliopo
Vitongoji Chake Chake Pemba chini ya usimamizi wa Mkuu wa Kikosi hicho
ambae ndie muanzilishi wa Skuli Hiyo Luteni Kanali Julius Khombwe Mbwelo
kwa wazo lao la kufikiria kuanzisha skuli hiyo.
Balozi Seif alisema
uwamuzi huo umekuja katika kipindi muwafaka utakaochangia kwa kiasi
kikubwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye skuli za Serikali
zinazozizunguuka Kambi hiyo.
Alielezea faraja na kuvutiwa na uamuzi wa kizalendo wa Jeshi hilo wa kukubali
kuwapokea watoto wa raia wa jirani na Kambi hiyo ambao ni wa kupigiwa
mfano na Serikali Kuu inaangalia mazingira ya kuisaidia Skuli hiyo
ambayo kwa mazingira yake inahesabika kama ni skuli ya umma licha ya
kwamba inahudumiwa kwa nguvu za wanajeshi wenyewe.
“ JWTZ linafahamika
kwa kuanzisha miradi mbali mbali inayosaidia jamii katika maeneo tofauti
Nchini ikiwemo Skuli za msingi na Sekondari, Vituo vya Afya na hata
kazi za kujitolea “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliwataka wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma kwenye
skuli hiyo kuhakikisha kwamba wanatoa ada zao ndogo walizopangiwa kwa
wakati ili huduma za wanafunzi zinazotolewa skulini hapo ziendelee kama
kawaida.
Katika kuunga mkono
juhudi za Makambanda na wapiganaji wakambi hiyo ya 14 Vitongoji Chake
Chake Pemba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi
kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar katika kuhakikisha Skuli hiyo
inaondokana na tatizo la huduma za Umeme.
Balozi Seif pia
aliahidi kuchangia gharama za matofali elfu moja yatakayosaidia
kuendeleza ujenzi wa jengo aliloliwekea jiwe la nsingi la Skuli ya
Maandalizi pamoja na kusaidia mipira kumi ya mchezo wa soka na kumi ya
mchezo wa Pete.
Akitoa Taarifa fupi ya Skuli ya Kikosi cha 14 cha Ali Khamis Mwalimu
Mkuu wa Skuli hiyo mwalimu Yugin Lutagengwa alisema skuli hiyo
ilianzishwa mwaka 2009 ikiwa na wanafunzi 39 na sasa wamefikia 604 wengi
wao wakia raia wa jirani wanayoizunguuka skuli hiyo.
Mwalimu Yugin
Lutagengwa alisema lengo la kuanzishwa kwa skuli hiyo chini ya Mkuu wa
Kikosi hicho Luteni Kanali Juius Khombwe Mbwelo ni kushiriki kwa
wanajensi katika Jamii wakati wa amani pamoja na kupunguza maafa kwa
watoto hasa pale wanapofuata elimu masafa ya mbali.
Hata hivyo Mwalimu Mkuu Yugin alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili skuli hiyo kuwa ni
pamoja na jamii kutoelewa elimu ya ushindani, uhaba wa majengo kutokana
na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi pamoja na tatizo la huduma za
umeme.
Katika Risala yao
iliyosomwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Skuli hiyo Mwanafunzi
Ridhiwan Khalfan Hamad wameelezea kufarajika kwa kiwango cha elimu
wanachokipata katika skuli yao.
Hata hivyo wanafunzi
hao waliiomba Serikali na wafadhili kufikiria wazo la kuwapatia huduma
za mitandao Kompyuta ambayo wanaimani kwamba itaongeza nguvu zao za
ufahamu katika masomo yao mbali mbali.
Mapema Kamanda wa
Kikoci cha 14 cha Ali Khamis kiliopo Vitongoji Chake chake Pemba Luteni
Kanali Julius Khombwe Mbwelo alisema katika kuwajengea mazingira bora ya
kufaulu vyema wanafunzi wao Uongozi wa Skuli hiyo uko katika juhudi za
kujenga Bwalo la wanafunzi ili kuwapa utulivu katika masomo yao.
Kamanda Julius alisema
hatua hiyo imelenga kuwaanda vizuri wanafunzi wa darasa la saba
walioingia mwaka huu ambao wanatarajiwa kufanya mtihani wa Taifa kwa
ajili ya kujiwekea malengo ya kuingia skuli za Sekondari za Mchepuo.
Wakati huo huo Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikagua Hospitali ya Jeshi hilo
iliyopo jirani na eneo hilo ambayo pia hutoa huduma za afya kwa askari
pamoja na wananchi wanaolizunguuka eneo hilo.
Hospitali hiyo kubwa
imefanyiwa matengenezo makubwa kwa msaada wa Serikali ya marekani ambapo
baadaye inatarajiwa kuongeza huduma zake za afya likiwemo suala la
kulaza wagonjwa.
Mganga Mkuu wa
Hospitali hiyo Kepteni Said Omar Mwege alimueleza Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif change moto wanazokabiliana nazo kubwa likiwa
ongezeko la wagonjwa ambapo uwezo wa kuwapatia huduma za dawa ni mdogo.
Kepteni Said alieleza
kwamba licha ya mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya Uongozi wa Kambi
hiyo na Uongozi wa Wizara ya Afya Pemba lakini suala la upatikanaji wa
dawa Hospitalini hapo linahitaji kuungwa mkono ya Serikali.
Akitoa shukrani zake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliueleza uongozi wa
Hospitali hiyo kwamba Serikali itaangalia nama ya kuiwezesha Hospitali
hiyo kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi.
Balozi Seif aliuagiza
Uongozi wa Hospitali hiyo kupitia Mkuu wa Kambi hiyo kuorodhesha
mapungufu yote yaliyomo ndani ya Hospitali hiyo ikiwemo wafanyakazi ili
Serikali ijipange katika kuona inatoa msukumo kwa Hospitali hiyo.
Aliopungeza Uongizo wa
Kambi hiyo katika juhudi za kuimarisha huduma za afya kwa uwamuzi wake
wa Kujenga jengo jipya la huduma za uchunguzi wa X Ray,Utra sound pamoja
na ushauri nasaha kwa wananchi walioambukizwa na virusi vya Ukimwi.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi aliueleza Uongozi wa Hospitali hiyo
kwamba yeye binafsi ataangalia mazingira ya kusaidia vitanda vya
wagonjwa kwa ajili ya Hospitali hiyo katika kipindi kifupi kijacho.
Credit: Zanzinews
Post a Comment