*********
Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko katika
Baraza la Mawaziri ambayo yamewatupa nje mawaziri watano, kuwaingiza 10
wapya, kuwapandisha manaibu wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha
wengine wanane kutoka wizara zao kwenda nyingine.
Miongoni mwa walioachwa katika mabadiliko
yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana,
ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya
Huvisa ambaye nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa
Maji, Dk Binilith Mahenge.
Wengine walioachwa na wizara zao kwenye mabano ni
Manaibu Waziri, Goodlucky Ole Medeye (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi), Gregory Teu (Viwanda na Biashara), Benedict Ole Nangoro
(Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Philipo Mulugo (Elimu na Mafunzo ya
Ufundi).
Mawaziri hao wanaungana na waliokuwa mawaziri wa
Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,
Shamsi Vuai Nahodha, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David na
Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki ambao uteuzi wao ulitenguliwa na
Rais kutokana na matokeo ya uchunguzi wa Kamati ya Bunge kuhusu
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Balozi Sefue alisema kuachwa kwa mawaziri hao ni
moja ya hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete kuimarisha utendaji
serikalini. Pia alisema mabadiliko hayo yametokana na kuwapo kwa nafasi
baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao na kifo cha aliyekuwa
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
“Rais amefanya mabadiliko kwa mujibu wa Ibara ya
55 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mamlaka ya
kutekeleza wajibu huo,” alisema Balozi Sefue.
Sura mpya
Sura 10 mpya zilizoingia katika Baraza hilo ni
pamoja na Dk Asha Rose Migiro aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani ambaye anakuwa Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Naibu wake, Kaika Saning’o ole Telele
ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro.
Wengine wapya ni wale walioteuliwa kuwa Naibu
Mawaziri na wizara zao kwenye mabano, Mbunge wa Iramba Mashariki,
Mwigulu Nchemba (Fedha), Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto) na Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama
(Elimu na Mafunzo ya Ufundi).
Pia wapo Mbunge wa Serengeti, Dk Steven Kwebwe
(Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Mbozi Magharibi, Godfrey Zambi
(Kilimo, Chakula na Ushirika), Mbunge wa Mufindi Kusini, Mahmoud Ngimwa
(Maliasili na Utalii) na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo).
Waliopandishwa, kuhamishwa
Mbali na Dk Mahenge, Rais Kikwete pia
amewapandisha manaibu waziri wengine watatu kuwa mawaziri kamili pasipo
kuwahamisha wizara walizokuwa. Hao ni Saada Nkuya Salum anayekuwa Waziri
wa Fedha, Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Rashid (Afya
na Ustawi wa Jamii)
MWANANCHI
Post a Comment