
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian akizungumza baada ya kutiliana saini na Umoja wa Ulaya Tanzania (EU) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) jijini Dar es Salaam jana, Kutoka kushoto ni Mratibu Mkazi wa UNDP, Alberic Kacou na katikati ni Balozi wa EU Tanzania, Ceriani Sebregondi. Picha na Salim Shao
******
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu, Amir Manento na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu, Damian Lubuva jana walilumbana mbele ya wafadhili kuhusu ufanisi wa Nec katika chaguzi mbalimbali nchini.
Malumbano hayo yalitokea mbele Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alberic Kacou wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya EU kutoa msaada wa Sh8.2 bilioni kwa Nec na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec).
Akizungumza katika halfa hiyo, Jaji Manento alisema Nec haifanyi kazi kwa uwazi na kwamba imekuwa ikivibagua baadhi ya vyama vya siasa katika utendaji wake. Hata hivyo, hakutaja chama chochote.
“Tume ya Uchaguzi haifanyi kazi kwa usawa, inavibagua baadhi ya vyama vya siasa, haiko huru, hii ni hatari katika ujenzi wa demokrasia hapa nchini,” alisema Jaji Manento.
Alisema hadi sasa, Daftari la Kudumu la Wapigakura halijaanza kufanyiwa marekebisho hali ambayo inaweza kuwakosesha haki ya kupiga kura ya maoni baadhi ya wananchi katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Alisema Serikali haijapeleka fedha kwa ajili ya kurekebisha daftari na kwamba kazi hii ilitakiwa kuanza mapema.
“Hata hizi fedha zinazotolewa na wafadhili kunakuwa na urasimu katika kuzipata. Wao wanazitoa mapema lakini Hazina inachelewesha, hivyo Tume inashindwa kutekeleza majukumu yake,” alisema Jaji Manento.
Hata hivyo, Jaji Lubuva alijibu mapigo kwa kusema Nec haijawahi kuvibagua vyama vya siasa na kwamba inafanya kazi zake kwa uwazi na kufuata sheria.
Alisema kiutendaji, Tume hiyo iko huru na kwamba yeye na wajumbe wenzake hawajawahi kushinikizwa na kiongozi yeyote ili kupendelea upande fulani.
Kuhusu Daftari la Wapigakura, alisema wakati wowote kuanzia sasa wataanza kuandikisha watu ambao hawakuwamo kwenye daftari hilo.
Kwa muda mrefu vyama vya siasa vya upinzani vimekuwa vikiilalamikia Nec kuwa inafanya kazi kwa kukipendelea CCM kutokana na muundo wake wakisema mwenyekiti wake anateuliwa na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho tawala.
MWANANCHI


Post a Comment