Faru akiwa ameuawa mbugani. |
Kasi
ya ujangili imeendelea kuleta hofu dhidi ya rasilimali nchini, baada ya
juzi majangili kuua faru aitwaye ‘Mama Serengeti’ na kumng’oa pembe
zake katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aidha,
kundi jingine linalosadikiwa kuwa la majangili, likiwa ndani ya Hifadhi
ya Mamlaka ya Ngorongoro lilivamia basi la abiria na kuwapora wasafiri
fedha na mali zao juzi alasiri.
Kutokana
na hali hiyo, Serikali jana alfajiri ilituma kikosi maalumu cha askari
20 wenye silaha na vifaa maalumu vya kupambana na ujangili ili kuongeza
nguvu na kuhakikisha majangili hao wanatiwa mbaroni.
Hayo
yamethibitishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, huku
akisisitiza kuwa, hali ya ujangili nchini ni mbaya na kwamba, kwa namna
yoyote ile Serikali itapambana na vitendo hivyo vya uhujumu uchumi
vinavyofanywa dhidi ya rasilimali za Taifa.
“Tumeagiza
kila gari ama mtu anayeingia na kutoka katika hifadhi ya Serengeti na
Ngorongoro apekuliwe, ikiwa ni sehemu ya kuwasaka wahalifu, tahadhari
imetolewa kwa mwananchi yeyote kutoa taarifa zinazohusu wageni na watu
wanaotiliwa shaka, tuna taarifa ya raia watatu wa nchi moja ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) hivyo kuonesha dalili kuwa mtandao wa kuua
faru ni mkubwa,” alisema Nyalandu.
Akielezea
ilivyokuwa, Nyalandu alisema walipokea taarifa za kusikitisha usiku wa
kuamkia jana, saa 6.30 za majangili kuua faru katika eneo la Moru,
Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwamba askari wa wanyamapori
waliokuwa doria ndio waliogundua faru huyo akiwa amepigwa risasi na
pembe zake kung’olewa.
Faru
huyo ameacha mtoto mwenye umri wa miezi miwili na mpaka taarifa hiyo
ilipotolewa, mtoto huyo alikuwa hajulikani alipo. Inaelezwa alipewa jina
Mama Serengeti kutokana na kuwa chimbuko na faru wengine 31 `wazalendo’
waliobaki katika Hifadhi ya Serengeti.
Mbali
ya faru hao `wazalendo’, hifadhi hiyo pia ina faru wengine wanne kati
ya watano ambao waliletwa nchini kwa mradi maalumu uliosimamiwa na Rais
Jakaya Kikwete kutoka Afrika Kusini. Faru mmoja kutoka Afrika Kusini
aliuawa na majangili Desemba mwaka 2012.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri huyo, baada ya kupokea taarifa, Serikali kupitia
Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na
usalama ilichukua hatua ya dharura kuagiza msako wa majangili katika
maeneo yote yanayozunguka hifadhi hizo mbili.
“Serikali
inawasaka kwa udi na uvumba raia hao watatu na wananchi wanaombwa
kusaidia kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, sambamba na
hatua hiyo, mapema leo (jana), wizara imetuma kikosi maalum (Rapid
response team) cha askari 20 wakiwa na silaha na vifaa maalumu ili
kuongeza nguvu na kuhakikisha majangili wanapatikana,” alieleza
Nyalandu.
Akielezea
hatua nyingine zilizochukuliwa katika mapambano dhidi ya ujangili,
Nyalandu alisema serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge
yaliyotolewa na Kamati ya James Lembeli, Mbunge wa Kahama (CCM),
imechukua hatua mahususi ikiwa ni pamoja na kutekeleza agizo la Rais
Kikwete la kuundwa kwa Tume ya Kimahakama kuchunguza tuhuma dhidi ya
operesheni tokomeza.
Nyalandu
alisema baada ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika operesheni
hiyo, serikali itaendesha operesheni nyingine. Lakini wakati ikijiandaa
kwa `vita’ nyingine kali dhidi ya majangili, alisema wizara
imewasimamisha kazi watumishi 23 wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali
zikiwemo za kula rushwa na kusaidia majangili.
Alisema
pamoja na taarifa za kukamatwa kwa meno ya tembo katika maeneo
mbalimbali nchini, ikiwemo tukio lililoripotiwa katika Bandari ya Dar es
Salaam mapema mwezi huu, wiki iliyopita, katika Kijiji cha Ugenza,
Mufindi, waliwakamata majangili watatu wakazi wa Dar es Salaam
wakisafirisha meno ya tembo kilo 37.
Aliwataja
waliokamatwa na maeneo wanakoishi kwenye mabano kuwa ni mwanamke mmoja
ambaye ni Salome Aloyce (Sinza Madukani), Rajabu Omari (Kigogo) na
Kadili Kisanduku (dereva teksi wa Mbezi Louis). Alisema walikuwa na gari
aina ya Toyota Corona yenye namba za usajili T580 ABL, mali ya Florian
Elias wa Dar es Salaam na walikuwa wanaelekea jijini humo. Sasa
wanashikiliwa na Polisi.
Katika
kipindi cha miaka mitatu (2008 hadi 2013), meno ya tembo yenye uzito wa
kilo 32,987 yalikamatwa ndani na nje ya nchi, jambo lililo ishara ya
kukithiri wa ujangili wa wanyama hao nchini.
Mwaka
2010, Tanzania ilipigiwa mstari mwekundu kuwa moja ya nchi
iliyoathirika zaidi kwa ujangili na biashara ya meno ya tembo duniani.
Idadi ya tembo inaelezwa kupungua nchini kwa kasi ambapo mwaka 2009
kulikuwa na tembo 109,000 lakini kutokana na ujangili, walifikia 70,000
mwaka 2012.
Post a Comment