Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo,
Amos Makalla (pichani), amemuomba Rais Jakaya Kikwete kutengua umiliki ardhi wa
hekta 5000 wa Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, wilayani Mvomero
kutokana na kushindwa kuiendeleza.
Makalla alisema kuwa ameshaiandikia Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, imshauri Rais kutengua umiliki huo wa Sumaye
kupitia kikundi cha Katenda ili kurudishwa kwa wananchi.
Maeneo mengine aliyopendekeza yarudishwe kwa wananchi ni pamoja na
ranchi ya Mkata na Kipunguni katika kata ya Melela wilayani humo.
Makalla ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mvomero, alisema hayo
wakati akichangia hoja za migogoro ya ardhi iliyoibuliwa na wajumbe
katika kikao cha kamati ya ushauri (RCC) ya mkoa wa Morogoro.
Alisema kuwa kuna mashamba mengi yanamilikiwa na vigogo akiwemo
waziri mkuu huyo mstaafu kupitia kikundi hicho lakini yameshindwa
kuendelezwa na kubaki mapori huku wananchi wakikosa maeneo ya kilimo.
“Sisi Mvomero tayari tumeshabaini hayo mashamba pori likiwemo la
Sumaye na tumewandikia barua Wizara ya ardhi kumshauri Rais Kikwete
kutengua umiliki wake ili wapewe wananchi wake,” alisema.
Awali Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogerezi,
akielezea kwa kina suala la mashamba pori yanayomilikiwa na vigogo
katika mkoa huo likiwemo la Mvomero alitaka kikao hicho kutoka na
maazimio ya kuunda kamati itakayobaini mashamba pori ambayo
hayaendelezwi.
Alisema kuwa kamati hiyo itakapobaini wamiliki wa mashamba pori
bila kujali nyadhifa za viongozi mbalimbali wawasilishe kwa Rais Kikwete
ili afute umiliki na kupewa wananchi.
Kalogerezi ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa
wa Morogoro, alisema kupitia umoja wao wa wabunge wa mkoa huo
watalizungumzia suala hilo katika bunge ili liweze kutoa maamuzi.
Alisema kuwa mkoa wa Morogoro umekuwa ukikabiliwa na migogoro ya
wakulima na wafugaji kutokana na maeneo mengi kuhodhiwa bila kuendelezwa
na vigogo.
“Lazima ifike mwisho kwa migogoro hii ya wakulima na wafugaji,
tuunganishe nguvu ya pamoja bila kujali itikadi ya siasa kutetea mkoa wa
Morogoro ambao kiasili ni mkoa wa kilimo,” alisema.
Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo ya ushauri ya mkoa wa Morogoro,
kufanya maamuzi ya kuzuia uingizaji wa wafugaji wapya pamoja na kutambua
wingi wa mifugo na hatua ya kuipunguza iweze kufanyika na kuepusha mkoa
kugeuka kuwa jangwa.
Naye Kaimu katibu wa Chama cha Demokrasia ma Maendeleo (Chadema),
mkoa wa Morogoro, Boniface Ngonyani, aliunga mkono hoja ya wabunge hao
wa CCM kwa hatua ya kumwandikia Rais Kikwete kutengua umiliki wa
mashamba pori yanayomilikiwa na vigogo katika wilaya mbalimbali za mkoa
wa Morogoro.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI



Post a Comment