BANA APONGEZA
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala toka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Benson Bana (pichani), alisema rais amefanya uteuzi mzuri akizingatia weledi, uzoefu na rekodi nzuri ya walioteuliwa “Ukiangalia kwa mfano uteuzi wa Dk. Asha- Rose Migiro katika Wizara ya Katiba na Sheria ni mzuri, kwa sababu ni mtu ambaye mbali na kuwa na weledi wa sheria, lakini pia ana uzoefu mkubwa wa uongozi.
Ni uteuzi muafaka tukizingatia kuwa tuko kwenye kipindi cha mchakato wa katiba, hivyo atamsaidia sana rais ili tuweze kuvuke tukiwa salama, na hatimaye tupate katiba itakayotufaa kwa miaka mingi ijayo,” alisema.
Dk. Bana aliipogeza pia hatua ya rais ya kuwaacha badhi ya mawaziri wenye rekodi nzuri kama profesa Anna Tibaijuka, na Sospter Muhongo, hatua inayoonyesha umakini wa rais.
“Hata hivyo, tatizo ambalo bado lipo ni lile la kimfumo linalopaswa kutatuliwa, kwa sababu baadhi ya watendaji katika wizara na hasa makatibu wakuu, wakurugenzi na wengine ndio wanaokwamisha kazi nzuri za baaadhi ya mawaziri...Kwa hiyo kuna haja sasa ya kuugeukia mfumo,” alisema.
Akizungumzia kuhusiana na kuachwa kwa baadhi ya mawaziri, alisema kwa watendaji wazuri kama Dk. Terezya Huviza hawana tatizo, kwa sababu rais anaweza akampangia kazi nyingine, na hata kumrejesha kwenye kazi yake ya awali ya taaluma.
Alisema, kwa mawaziri kama Philipo Mulugo, siyo kitu cha kushangaza kwa sababu alishaonyesha toka mwanzo kuwa anapwaya kwenye hiyo nafasi, na hasa pale aliposhindwa kuongea lugha moja na watendaji katika wizara hiyo.
BAREGU AKOSOA NYALANDU
Naye Profesa wa Sayansi ya Siasa na Utawala toka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwesiga Baregu alisema kitendo cha kuzunguka kwa sura karibu zile zile kwenye uteuzi uliofanywa na rais, kunaonyesha ubaya wa mfumo uliopo chini ya katiba ya sasa, unaomtaka rais ateue mawaziri walio wabunge.
“Hii ni karibu safari ya tatu au ya nne rais anabadilisha baraza lake..na hapa ndiyo umuhimu wa kile Tume ya Warioba iliyopendekeza kwenye rasimu ya katiba mpya, kwamba mawaziri wasiwe wabunge. Nchi yetu ina watanzania wengi wenye uwezo, lakini inawezekana rais anashindwa kuwapata hao kigezo cha kutokuwa wabunge na hivyo kumfanya azungukie sura zile zile,” alisema.
Alisema kasoro anayoiona kwenye uteuzi huo ni kwa baadhi ya mawaziri mizigo kuendelea kuwa ndani ya baraza.
“Nilidhani kwa mfano waziri Lazaro Nyalandu kwa kuzingatia utawala bora, asingebaki kwenye baraza hili, kwa sababu hatujui Tume ya Kimahakama iliyoundwa itamhusisha vipi, ukiichulia kwamba, ametajwa tajwa kwenye operesheni tokomeza uzangiri, ilipaswa awe benchi,” alisema.
Akizungumzia uteuzi wa Dk. Asha Rose Migiro, kwenda wizara ya katiba na sheria, Profesa Baregu alionyesha wasiwasi ikiwa mchakato wa katiba utaenda sawa na watanzania wakapata katiba nzuri.
"Toka mchakato wa katiba mpya uanze, wizara ya katiba na sheria imekuwa na mawaziri watatu sasa, tukianzia kwa Celina Kombani, ambaye hakutaka kabisa kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya, kisha akaja waziri Mathias Chikawe ambaye naye alipeleka sheria bungeni iliyoleta kubadilika kwa nafasi ya tume, na sasa Dk. Migiro, sijui kama atasimamia vyema suala la katiba mpya, au atatanguliza mbele maslahi ya chama chake, ukizingatia kuwa ni kada,” alisema.
Akizungumzia kuachwa kwa baadhi ya mawaziri akiwemo Pillip Mulugo, Profesa Baregu alisema hakushangazwa na hatua hiyo kwa kuwa alishaonekana kupwaya, ila akashangaa kwa nini bosi wake, Dk. Shukuru Kawambwa amebakia kwenye wadhifa, wakati ameshatajwa kuwa mzigo.
TEF: NKAMIA ATAUA
TASNIA YA HABARI
Kwa upande wake, akizungumzia uteuzi wa Juma Nkamia kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alisema uteuzi huo unaonyesha kuwa, Rais Jakaya Kikwete anaiangalia tasnia ya habari nchini kwa jicho baya.
“Toka Nkamia amekuwa mbunge, michango yake bungeni imekuwa dhidi ya tasnia ya habari, Baraza la Habari, Jukwaa la Wahariri na ameonyesha kwa ujumla, kwamba haamini katika uhuru wa habari, huku akivituhumu vyombo vya habari kuandika mambo ya uchochezi tu,” alisema.
Alisema uteuzi wa Nkamia kwenda kwenye wizara hiyo kumsaidia waziri ambaye naye haamini katika uhuru wa habari, ni pigo kwa tasnia ya habari nchini, labda kama atabadilika.
Hata hivyo Kibanda alisema, alichofanya rais ndicho alichoona kinafaa kwa sababu ana haki ya kikatiba ya kuchagua mtu yeyote yule, kwenye nafasi za uwaziri na kama alivyowahi kunukuliwa huko nyuma akisema kwamba, urais wake hauna ubia, vyombo vya habari vitaendelea kufanya kazi yake kufuatana na weledi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Pentecoster Assemblis of God Tanzania (PAG) (T), Daniel Awet alisema kuwa hakuna mabadiliko bali kuzidisha mzigo kwa Serikali yenyewe na Watanzania.
Awet alisema Watanzania walitarajia kuona wale wote waliotanjwa kuwa mawaziri waliotajwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni mizigo wanaondolewa, lakini badala yake wameachwa na kuzidisha matatizo zaidi kwa wananchi.
Alisema mawaziri hao walilalamikiwa na viongozi wa wa CCM na wananchi, lakini wameachwa katika nafasi zao na kuendelea kupeta bila kujali maumivu waliyonayo Watanzania.
“Ukinzingatia kuwa mawaziri hao wamelalamikiwa na Kamati Kuu ya CCM na viongozi mbalimbali na kusemwa hadharani kuwa ni mizigo kwa kuwa hawana uwezo wa
Makamu Mkuu wa Askofu Kanisa la Christian Mission Fellowship Tanzania, Donard Mhango, alisema uteuzi huo ni sawa na nyoka anayetapatapa baada ya kupigwa.
Aliongeza kuwa baadhi ya mawaziri wameteuliwa bila kuangaliwa sifa na ubora wa uongozi kama utawanufaisha wananchi walio wengi ambao kwa sasa wanalalamikia utendaji wa viongozi wengi serikalini.
Hata hivyo, aliwataka mawaziri walioteuliwa kutumia nafasi zao vizuri na kujifunza kwa baadhi ya mawaziri ambao wanatekeleza majukumu yao kwa kuwaangalia watu wa hali ya chini.
Aidha Askofu huyo alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuchukua maamuzi magumu bila kuchelewa pale walioteuliwa watakaposhindwa kuwajibika ili kuwaongezea wananchi imani kwa serikali yao.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment