*********
Mshtakiwa George Mulungu (28) mkazi wa Vingunguti amefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kumuua kwa
kukusudia aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo
Mvungi.
Mulungu alisomewa shtaka la mauaji ya kukusudia
juzi na Wakili wa Serikali, Charles Anindo ambaye pia alimwomba Hakimu
Mkazi, Geni Dudu kuwa mshtakiwa huyo Januari 30, 2014, aunganishwe na
wenzake 10 wanaokabiliwa na kesi hiyo.
Hakimu Dudu alikubaliana na ombi hilo na
kuiahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2014 ambapo mshtakiwa huyo
ataunganishwa na wenzake Chibago Magozi (32) mfanyabiashara na mkazi wa
Vingunguti Machinjioni, John Mayunga (56) mfanyabiashara na mkazi wa
Kiwalani na Juma Kangungu (29) mkazi wa Vingunguti.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi,
Longishu Losingo (29) na Masunga Makenza (40) dereva na mkazi wa
Kitunda, Paulo Mdonondo (30) Mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa (40)
mkazi wa Vingunguti, Zacharia Msese (33) mkazi wa Buguruni, Msungwa
Matonya (30) mkazi wa Vingunguti na Ahmad Kitabu (30) mkazi wa
Mwananyamala wilayani Kinondoni na kufanya idadi ya washtakiwa hao
kufikia 11.
Awali akiwasomea hati ya mashtaka washtakiwa hao,
Wakili wa Serikali, Aida Kisumo alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja
Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa hilo la mauaji ya kukusudia
kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kisumo alidai kuwa siku ya tukio, katika eneo la
Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao
kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi ambaye ni Mjumbe wa
Tume ya Katiba Mpya.
MWANANCHI
Post a Comment