HABARI
zenu wapendwa wasomaji wa safu hii. Nichukue nafasi hii kwa mara
nyingine kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya
njema leo.Kama ninavyosema mara kwa mara, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchukua muda wake, walau kidogo, kumshukuru Mungu kwa sababu daima amekuwa akitenda maajabu makubwa sana kwetu.
Wakati nchi ikijiandaa kuelekea kwenye uundwaji wa Bunge la Katiba litakalojadili rasimu ya pili ya Katiba mpya ya Tanzania, ambayo kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete itakamilika mwaka huu, yapo mambo mawili muhimu ambayo yamekuwa yakifanyika, yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu.
Haya ni vitambulisho vya uraia pamoja na maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura. Nimekuwa nikitatizwa kidogo na jinsi ambavyo mambo yanavyoendelea katika maeneo haya, kiasi cha kuona kuwa haiko sawa, au inabidi kufanya maboresho zaidi.
Na kitu ambacho kimenifanya nipate wasiwasi ni kuhusu muda unaowekwa na vyombo vinavyoshughulika na mambo haya, Vitambulisho vya uraia, mradi unaosimamiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Daftari la kudumu la wapiga kura, lililo chini ya uangalizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika vitambulisho vya taifa, suala la muda limekuwa ni jambo linaloleta usumbufu mkubwa. Kwa kuanzia, maofisa wa mamlaka hii walitembelea kila kata kwa ajili ya kuandikisha watu, wakitoa muda wa mwisho wa kufanya hivyo. Hii ilimaanisha kuwa endapo mtu, kwa sababu zozote zile, hataweza kujitokeza ndani ya muda uliotolewa kabla ya maofisa kuondoka eneo lile, atakuwa amejinyima haki yake mwenyewe ya kupata kitambulisho cha taifa.
Ninazungumzia awamu ya kwanza kabisa ambapo watu waliandikishwa katika misururu mirefu kote nchini, achana na awamu ya pili ambako pia muda wa mwisho ulitolewa.
Na hata sasa tunapozungumza, daftari la kudumu la wapiga kura lililoanzishwa kwa mujibu wa sheria, ambayo katika sura ya 343, inaeleza kuwa uboreshaji wa daftari hilo utafanyika mara mbili kwa muda wa miaka mitano, ikiwa na maana kuwa kila baada ya miaka miwili na nusu, litaboreshwa.
Kwangu, hili ni tatizo, siyo tu la haki za raia kupokwa, bali pia kukiri kwamba tunafanya kazi kukinzana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambayo ndiyo yanaongoza dunia kwa sasa.
Utawezaje kusema tarehe fulani, bila kujali ni lini, eti ndiyo itakuwa mwisho wa kuandikisha majina kwa ajili ya vitambulisho vya taifa au daftari la kudumu la wapiga kura? Ni lazima tupanue mawazo, tukubali changamoto mpya.
Kila siku, watanzania kadhaa, wanaofikia kwa mamia, wanatimiza umri wa miaka 18, unaowapa haki ya kupata kitambulisho cha uraia na haki ya kuwemo katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Katika suala kama hili, unawezaje kutoa muda wa mwisho? Ni wazo langu kwamba haya ni mambo ya kudumu, yasifanywe kidharura. Tusiwachukue watu wa kuifanya kazi hii kwa dharura huku tukiwalipa mamilioni, wakati ni jambo linalopaswa kufanywa na watumishi wa serikali katika ofisi za halmashauri ya miji na serikali za mitaa.
Ofisi ziwepo kila siku kwa ajili ya mtu anayehitaji kitambulisho au kuwemo katika daftari. Achukuliwe maelezo yake, kama ni suala la uhakiki wa taarifa zake, ufanyike, lakini mwisho wa siku mtu aweze kuchukua kitambulisho au kuandikishwa akiwa popote katika Tanzania na siku yoyote.
Kwa teknolojia ya sasa, ni rahisi zaidi kuliko kuwa na rundo la maofisa wanaoweka kambi sehemu mbalimbali kwa ajili ya kupata maelezo ya watu.
Huwezi kujua, wakati maofisa hao wanapofika eneo moja, siyo watu wote wa hapo watapatikana, wengine wako safarini, wengine wamehama, wengine wapo mahospitalini na kadhalika. Sasa kama baada ya wiki moja tutasema watu wa eneo hilo ambao hawakuwepo shauri lao, hatuoni kwamba hatutendi haki?
Na kuhusu daftari la wapiga kura, hivi katika miaka miwili na nusu, kuna chaguzi ngapi ndogo zinazofanyika ambazo zinawanyima watu haki yao ya msingi kwa sababu tu hawakujiandikisha?
Nadhani ni muda muafaka wa kubadili fikra, hili lisiwe suala la muda, uwe utaratibu wa kudumu!
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


Post a Comment