Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
umempelekea Zitto Kabwe (pichani) taarifa ya kikao cha Kamati Kuu kilichomvua
madaraka yake ndani ya chama hicho ili aweze kukata rufaa.
Habari za kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kuwa
Kamati Kuu ya chama hicho ilifikia uamuzi huo wakati wa vikao vyake
vilivyofanyika kati ya Januari 3 na 4, mwaka huu.
Kutokana na uamuzi huo, Zitto sasa ataweza kukata rufaa ya kupinga kuvuliwa madaraka kwenye Baraza Kuu la chama hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa kamati hiyo ilimwagiza
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kumpatia mwenendo wa kikao
Zitto ili aweze kukata rufaa.
Dk Slaa alithibitisha jana kuwa chama hicho tayari
kimetuma muhtasari wa kikao hicho kwa Zitto, ambaye alikuwa anauhitaji
hadi kufikia hatua ya kufungua mashtaka mahakamani.
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando alisema wamepokea barua hiyo na walikuwa wanajiandaa kukata rufaa.
“Ni kweli tumepokea taarifa ile na tulikuwa tuna
fursa ya kuchagua kukata rufaa au la, lakini tumeisoma na tumeona tukate
rufaa,” aliongeza Msando.
Alisema hatua hiyo, bado haitasimamisha kesi
inayoendelea mahakamani, bali walalamikiwa sasa wana fursa ya kuitisha
kikao cha Baraza Kuu na kupima kama wana haja ya kuendelea na kesi.
Gazeti hili limeshuhudia barua hiyo iliyotumwa kwa Zitto, Januari 20, 2014 ikiwa na namba ya kumbukumbu namba C/HQ/ADM/KK/08/40.
Katika barua hiyo, Zitto aliarifiwa kuwa Kamati
Kuu ya Chadema katika kikao chake cha Januari 3 na 4, 2014 kiliandaa
taarifa kamili ya mwenendo wa shauri lake.
“Kwa kuwa Kamati Kuu ilikuwa ikitambua umuhimu wa
yeye kupewa nakala za mwenendo huo wa uamuzi wa kikao hicho, ilimwagiza
Katibu Mkuu wa Chadema kumpatia Zitto nakala za mwenendo wa kikao.
Barua hiyo inaeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa
baada ya taarifa ya Zitto iliyoeleza nia yake ya kukata rufaa dhidi ya
uamuzi wa Kamati Kuu, wa kumvua nyadhifa zake.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment