JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema haliogopi vitisho vya aina yoyote vinavyotolewa na Serikali ya Malawi kutokana na mgogoro uliopo. Hatua hiyo imetokana na viongozi waandamizi wa Serikali ya Malawi, kutangaza baadhi ya vijiji vya Tanzania vilivyopo kilomita 10 kutoka mpakani mwa Ziwa Nyasa kuwa ni mali yao.
Hatua ya JWTZ imekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete Februari
2, mwaka huu, wakati wa kilele cha sherehe za miaka 37 ya kuzaliwa kwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusema wananchi walioko kando ya Ziwa Nyasa
hawastahili kutishwa, kwani ufumbuzi wa jambo hilo unasubiri kamati ya
Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano na Rais mstaafu wa Botswana,
Festus Mogae ambao wataeleza ukweli wa jambo hilo.
“Kwa sasa kama kuna mwanasiasa analizungumzia jambo hili anatafuta
umaarufu tu, jambo hili lipo katika hatua nzuri na kamati ya Chissano
itatueleza ukweli,” alisema Kikwete.
Akizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya Brigedi ya
Chui iliyopo Lugalo mjini Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Brigedi ya Kusini,
Brigedia Jenerali John Chacha alisema kauli ya viongozi wa Malawi
isisababishe wananchi wa vijiji hivyo kuingiwa hofu, kwa sababu ni watu
halali kutoka nchini Tanzania.
Alisema wakati viongozi wa Malawi wanatangaza hayo, tayari mgogoro huo
upo kwenye kamati ya usuluhishi ya Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim
Chissano na Rais mstaafu wa Botswana, Festus Mogae.
Alisema kutokana na mgogoro huo, JWTZ imekuwa ikitumia nguvu kubwa
kulinda mipaka ya nchi yake, ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya
uhalifu vinavyoweza kutokea ndani ya maeneo hayo.
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment