Bw. Ndebile Kazuri pichani anayedaiwa kutelekeza.
MATUKIO
ya utelekezaji wa mke na watoto nchini Tanzania bado ni changamoto
kubwa katika jamii. Licha ya matukio haya kutofautiana kutoka eneo moja
hadi lingine bado yanachochewa na kulegalega kwa sheria za nchi ikiwemo
sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa baadhi ya vipengele.
Waathirika
wakubwa wa matukio haya ni mama pamoja na watoto ambao ndio hutelekezwa
huku baba aliyetelekeza familia hiyo kutokomea sehemu nyingine na
kwenda kuanzisha familia nyingine, ambayo nayo uhai wake huwa mashakani.
Hivi
karibuni mwandishi wa makala haya kwa ushirikiano wa Chama cha
Wanahabari Wanawake (TAMWA); alifanikiwa kutembelea Wilaya ya Nkasi,
Mkoa wa Rukwa na kufanya utafiti wa kihabari kuangalia matukio ya
kiunyanyasaji na ukatili ambayo huwakumba wanawake na watoto katika
wilaya iliyotajwa.
Maria
Tarafa (25) mkazi wa Kijiji cha Isale, Wilaya ya Nkasi ni miongoni mwa
akinamama ambao amekumbana na matukio ya utelekezwaji. Mama huyu
ameachwa kisheria na mumewe akiwa tayari wamefanikiwa kupata watoto
wanne bila kufanyika mgawanyo wa mali walizochuma na mumewe.
Hata
hivyo huenda tukio la kuachwa kwa Bi. Tarafa lisimuumize roho kama
ilivyo tukio la mume aliyemuacha yaani Bw. Ndebile Kazuri (31) kumtia
ujauzito akiwa darasa la sita katika Shule ya Msingi Isale mwaka 2004 na
kumkatisha masomo yake kabla ya kumuoa. Taarifa zinaonesha binti huyu
alipewa ujauzito akiwa na miaka 15 na kujifungua akiwa na miaka 16 na
papo hapo kufunga ndoa ya kimila kijijini hapo.
Akizungumzia
mkasa mzima, Bi. Tarafa anasema baada ya Kazuri kumkatisha masomo
yalifanyika mazungumzo ya kifamilia bila ya yeye kujua na alishangaa
kuona mzazi wake (ambaye sasa ni marehemu) amepokea mahari kasha yeye
kuozeshwa kimila kwenda kwa mumewe.
Aliishi
kwa mume huyo tangu kipindi hicho na kuzaa naye watoto wanne, lakini
visa na mateso kwa mwanaume vilianza akiwa na watoto wawili. Anasema
mume wake alikuwa akimpiga ndani ya ndoa yao na baada ya kuona mateso
yamezidi aliondoka na kurudi nyumbani.
Anasema
baada ya tukio hilo mumewe alitafuta wazee wa ukoo na kumfuata tena
nyumbani kwao na kumuomba samahani ili wamalize tofauti zao na kurudi
kwa mumewe. Anasema baada ya kumuomba aliridhia na kurudi kwa mumewe
akiwa na watoto wake wawili.
Bi.
Tarafa anasema baada ya kurudi waliongeza idadi ya watoto na kufikia
wanne kwa mumewe huyo. Vipigo na manyanyaso viliendelea na safari hii
mumewe akitamka wazi wazi kuwa anataka kumuacha hivyo arudi nyumbani kwa
wazazi wake tena na watoto wote. Uamuzi huu ndio uliomkera mwanamama
huyu na kuamua kudai haki zake za msingi pamoja na watoto wake.
Mumewe
ambaye kwa sasa anamke mwingine akiwa anaishi naye, alifungua kesi
namba 26/2013 katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi
Oktoba 28, 2013, akitaka mahakama ivunje ndoa yake na mkewe kwamba
amemchoka kutokana na kile kugombana naye mara kwa mara.
Kwa
mujibu wa nakala ya huku ambayo mwandishi wa makala haya anayo, kesi
hiyo iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwenye nakala ya hukumu kwa
jina la B. Stanley; ilitolewa hukumu Novemba 18, 2013 na mahakama
kuvunja ndoa hiyo.
Mahakama
ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili (wa
chini ya miaka saba) kati ya wanne waliozaa na mumewe bila kueleza namna
watoto hao watakavyo pata huduma toka kwa baba yao ambaye tayari
anatengana na mumewe.
Mahakama
hiyo pia katika hukumu yake iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki
kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Kwa mujibu
wa nakala ya hukumu mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe
magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha wote msimu wa kilimo
ulioisha na bati 7 zilizokuwa nyumbani kwao.
Bi.
Tarafa anasema haridhiki na namna ilivyotolewa hukumu ya kuvunja ndoa
yao. Anasema kwanza sababu zilizotolewa na mumewe mahakamani hazina
ukweli wowote na pia hakupewa nafasi ya kujitetea hadi hukumu ya ndoa
yao ikisomwa.
Anasema
pamoja na hayo mahakama imevunja ndoa yao, na kwa sasa hawezi
kung’ang’ania ndoa hiyo irejee lakini anachokitaka ni haki yake pamoja
na watoto ipatikane toka kwa aliyekuwa mumewe. Anasema walichuma mali
nyingi wakiwa pamoja lakini mali hiyo haikuzungumziwa kabisa mahakamani.
“…Inaniuma
sana kwa kitendo ambacho ananifanyia kwa sasa kwani alinikatisha
masomo, kanipotezea muda wangu na kaniongezea mzigo wa watoto wanne na
anataka niende kuishi nao peke yangu nyumbani kwetu,” anasema Bi.
Tarafa.
Anasema
wakati mumewe anafungua kesi ya kutaka mahakama ivunje ndoa yao
aliiongopea mahakama kwamba hawana mali yoyote nyumbani jambo ambalo si
kweli. “…Mume wangu alidanganya kuwa hatuna mali pale mahakamani, mimi
nikaeleza ni uongo kwani tuna ng’ombe zaidi ya 127, buzi 30, nyumba
mbili pale kijijini Isale pamoja na hekari zaidi ya 70 za
mashamba…hawakunisikiliza pale mahakamani. Ukweli ni kwamba tunamali
hizo ambazo tulichuma tukiwa wote,” anasema Bi. Tarafa.
Akifafanua
zaidi anasema walipewa ng’ombe za urithi toka kwa baba yake na Kazuri
zikiwa 65 lakini wamezizalisha hadi kufikia idadi zilipo sasa pamoja na
mashamba na nyumba lakini anashangaa mzazi mwenzake anamdhulumu kila
kitu.
Kimsingi
nakala ya hukumu ya kesi iliyovunja ndoa ina kurasa tatu pekee, ambazo
mwandishi wa makala haya amezipitia na ukweli ni kwamba hakuna sehemu
hata moja imezitaja mali anazozilalamikia Tarafa. Na pia hukumu hiyo
haikuonesha namna/utaratibu wa watoto wanaobaki kwa mama watakavyo
hudumiwa na baba.
Pamoja na hayo, Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Ramadhan Rugemalira anasema mama
huyo anahaki ya kufungua kesi ya madai kuomba mgawanyo wa mali na
matunzo kwa watoto endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa kwa shauri
hilo.
“…Anachotakiwa
kuomba mahakamani kwa sasa ni mgawanyo wa mali, kwamba katika kesi yao
ambayo mahakama ilivunja kuna mali ambazo mahakama haikuzizungumzia
kabisaa lakini na mimi (mke) ninahaki na mali hizo, unaona…ataleta
ushahidi kama ng’ombe hao wapo kama kuna ardà na nini…hivyo huyo
mwanaume ataitwa na kesi kusikilizwa,” anasema Rugemalira katika ushauri
wake akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Anaongeza
kuwa, huenda mtoa hukumu wa mwanzo aliteleza kwa kitendo cha
kutoainisha namna watoto wanaobaki kwa mama watalelewa vipi. Anasema
pamoja na hayo bado mama huyo anahaki ya kufungua madai mengine kudai
haki hizo.
Pamoja
na hayo, kwa kuzingatia Sheria nyingi kama vile Sheria ya Mtoto (2009),
Sheria ya Ndoa (1971), Sheria ya Kanuni za Adhabu (1937) n.k. pamoja na
mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na kusainiwa na taifa, ni vyema sasa
kila mtu, kwa nafasi yake mzazi/mlezi, na hata mamlaka kuwa ustawi na
maendeleo ya mtoto ni jambo lamsingi.
Sheria
ya Ndoa (1971), kifungu 114 kinaeleza uwezo wa mahakama kutoa amri ya
kugawana mali za waliooana na pia kuzingatia masilahi ya watoto na usawa
katika ugawaji. Pia kifungu 136 (1) kinaeleza uwezo wa mahakama
kuzingatia nasaha za maofisa wa ustawi kiushauri. Sheria ya Mtoto (2009)
pia inaeleza maana ya mtoto, lakini pia inatoa agizo la wajibu wa
mzazi/mlezi kwa mtoto au watoto.
Kwa
upande wake Kazuri akizungumzia mali ambazo mke anazilalamikia, yaani
ng’ombe 127, nyumba 2, mbuzi 30 na ardhi hekari 70 anasema mali hizo
alipewa na babayake wakati anaanza maisha hivyo bado ni mali ya babayake
ambaye alidai yupo hai hadi sasa. Uchunguzi uliofanywa umebaini baba
yake na Kazuri (yaani Kazuri Moshi) alifariki dunia tangu Machi 2004 na
mali zake kugawiwa kwa watoto wake.
Hata
hivyo tayari Bi. Tarafa amefungua kesi nyingine mahakama ya mwanzo
akiitaka mahakama igawe mali walizochuma na mumewe kipindi chote na
kuweka bayana majukumu ya namna watoto wa wanandoa hao waliotengana
watapata mahitaji yao kutoka kwa baba yao.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana TAMWA
Post a Comment