SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema lipo katika mpango wa uboreshaji wa vituo vidogo vya usambazaji na upoozaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza na kumaliza adha ya kukatika kwa umeme nchini.
Vituo hivyo ni pamoja na kile kilichopo katikati ya jiji pamoja na kituo cha Kurasini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea Miradi mbalimbali inayofanywa na TANESCO, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Charles Kitwanga, alisema uboreshaji huo unatokana na kuchakaa kwa miundombinu ya umeme hali inayopelekea kukatika kwa umeme mara kwa mara.
“Lengo la ziara ni kuona jinsi miradi inavyotekelezeka na kama Naibu waziri mpya katika wizara hii ni wajibu wangu kutambua kila kinachoendelea ili kuanza kufanya kazi kwa vitendo na ufanisi wa hali ya juu.
“Kwani ni kweli shirika letu limekuwa likikabiliwa na changamoto nyingi katika kufanikisha utekelezaji wake moja wapo ikiwa ni uchakavu wa miundombinu yake na inafikia wakati baadhi hushindwa kusafirisha umeme kwa umbali zaidi na kupelekea umeme kuwa hafifa katika baadhi ya maeneo,”alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imesimama imara katika kuhakikisha hakutakuwa na tatizo la umeme wa mgawo nchini, pindi ifikapo Januari mwaka 2015.
“Hadi kufikia Januari mwakani hakutakuwa na matatizo ya umeme kwani baadhi ya Mitambo ya kufua umeme ya kinyerezi one itaanza kukamilika,”alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Christian Msyani, alisema hadi sasa tayari baadhi ya miradi imeanza kukamilika, ukiwemo wa Kinyerezi one, unaotarajiwa kufua umeme wa Megawatt 150.
“Shirika bado litaendelea kuongeza transforma katika vituo vya kusambaza umeme ambavyo zitaweza kuongeza nguvu za upatikanaji wa umeme hasa katika eneo la Mbagala ambalo lina idadi kubwa ya viwanda,”alisema.
Post a Comment