
Rais Jakaya Kikwete
Viongozi wote wa kitaifa na wastaafu waalikwa kumsikiliza Kikwete
Profesa Lipumba aeleza tofauti zao zimezikwa, sasa ni kuchapa kaziSiku
tatu baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu
Joseph Warioba, kutikisa Bunge Maalum la Katiba kwa hoja nzito juu ya
rasimu ya katiba, kesho mji wa Dodoma utarindima tena kwa kufunikwa na
viongozi wakuu wote wa kitaifa waliopo madarakani na waliostaafu.
Ugeni huo umealikwa bungeni kushuhudia
hotuba ya ufunguzi wa bunge hilo la kihistoria itakayotolewa na Rais
Jakaya Kikwete Leo kama sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ya mwaka 2012.
Tukio hilo litahudhuriwa na Makamu wa
Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed
Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Wengine walioalikwa ni wajane wa waasisi, Mama Maria Nyerere na Fatma Karume.
Akizungumza na waandishi wa Habari
jana, Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis Hamad,
alisema kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, amewaalika wageni
mbalimbali ili kushuhudia tukio hilo muhimu la kitaifa.
Khamis aliwataja wageni wengine
walioalikwa kuwa ni pamoja na marais wastaafu kutoka pande zote za
Muungano. Marais wastaafu waliopo ni Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa,
Dk. Salmin Amour Juma na Amani Abeid Karume.
Wengine ni maspika wastaafu, Waziri
Kiongozi mstaafu ambaye hakutajwa jina. Hata hivyo, mawaziri kiongozi
wastaafu waliopo ni Shamsi Vuai Nahodha ambaye ni Mjumbe wa bunge hilo,
Ramadhan Haji Faki na Maalim Seif. Spika Mstaafu ni Pius Msekwa.
Waalikwa wengine ni watendaji wakuu
kutoka pande zote za Muungano, mabalozi wa nchi mbalimbali waliopo
nchini, wawakilishi wa taasisi za kimataifa pamoja na wawakilishi wa
taasisi mbalimbali za ndani ya nchi.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni
taasisi za kidini, wawakilishi wa tasnia ya habari, vyama vyote vya
siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi zisizo za kiserikali, vyama vya
watu wenye ulemavu, taasisi ya elimu, vyama vya Wafanyakazi, vyama vya
wafugaji, vyama vya wavuvi, vyama vya wakulima na wawakilishi toka sekta
binafsi.
Akizungumzia mpangilio wa shughuli
hiyo, Khamis alisema kuwa Bunge litaanza kikao chake majira ya saa 9:10
jioni na baadaye kikao kitaahirishwa saa 9:20 kwa ajili ya kumpokea
Rais.
Khamis aliwataka wajumbe wote wa
Bunge Maalum la Katiba pamoja na waalikwa wote kuwahi kuingia ndani ya
ukumbi kabla Rais hajawasili kwenye viwanja vya Bunge.
Alisema baada ya Rais kuwasili katika
viwanja vya Bunge, atapokewa na Mwenyekiti wa Bunge, Makamu wake,
Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum la Katiba.
Alisema baada ya mapokezi, Rais
ataelekea kwenye Jukwaa maalum kwa ajili ya kupokea salamu ya heshma na
kukagua gwaride Maalum ambalo limeandaliwa na Jeshi la Polisi.
Khamisi alisema kuwa tukio la kukagua
gwaride hilo litakapokamilika, viongozi wataingia bungeni kwa
maandamano maalum kwa ajili ya kwenda kusikiliza hotuba ya Rais ya
kuzindua Bunge hilo.
Alisema viongozi watakaoshiriki
maandamano hayo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na hatimaye Rais
wa Jamhuri ya Muungano ambaye atafuatana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum.
Alisema Rais atakapomaliza kuhutubia, Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba watapata fursa ya kupiga picha ya pamoja na Rais.
Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia Bunge saa 10:00 jioni kwa mujibu wa kanuni ya 75 (1) ya Bunge Maalum la Katiba.
Ingawa maudhui ya hotuba ya Rais
Kikwete hayajajulikana, hotuba ya Jaji Warioba bungeni juzi, imekuwa ni
jambo zito ambalo yamkini yatagusiwa kwa mapana yake.
Miongoni mwa mambo nyeti na yamekuwa
na ubishani mkubwa ambayo yameibuliwa na Tume na kuwekwa kwenye Rasimu
ya Katiba ni pamoja na muundo wa Muungano wa serikali mbili, wakati
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakipinga kwa nguvu zote.
Mambo mengine ni kupunguzwa kwa
kiwango kikubwa kwa madaraka ya rais; kujenga uwajibikaji kwa kuweka
maadili ya viongozi ndani ya katiba; kuimarishwa kwa haki za raia na
kuwandoa mawaziri kuwa wabunge.
Hofu iliyokuwa imetanda mjini Dodoma
ambayo ilisababisha hata Jaji Warioba kushindwa kuwasilisha hotuba yake
Jumatatu, ni suala linaloonekana kama kuviziana na kukosekana kuaminiana
baina ya wabunge wanaotokana na CCM na wale wa upinzani wakishirikiana
na wa kundi la kuteuliwa lenye wajumbe 201.
UKAWA WAMKUBALI JK
Wakati huo huo, Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) umekubali kumpokea na kumsikiliza Rais Jakaya Kikwete
atakapokuwa akizindua Bunge Maalum la Katiba.
Jumatatu iliyopita Ukawa uliongoza
vurugu na kelele bungeni kupinga hatua ya Sitta kumruhusu Jaji Warioba
kuwasilisha Rasimu ya Katiba kabla Rais hajazindua Bunge hilo.
Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim
Lipumba, alisema baada ya tukio la kumgomea Jaji Warioba, viongozi wa
Umoja huo walikutana juzi na kujadiliana na Kamati ya Mashauriano juu ya
suala hilo.
Alisema katika majadiliano hayo
walikubaliana kuwa Jaji Warioba aanze kuwasilisha Rasimu ya Katiba na
apewe muda wa kutosha na pia wabunge wakubali kumpokea na kumsikiliza
Rais atakapokuja kuzindua Bunge kesho.
“Tulikutana tukajadili na
kukubaliana, hivyo katika mkutano wetu wa Ukawa jana (juzi) tulikuwa
tukiwaeleza wajumbe wenzetu yale tuliyokubaliana na viongozi wa Bunge na
baada ya kuwaeleza sote tuliafikiana kuwa tumpokee na kumsikiliza Rais
wakati atakapokuja kuzindua Bunge Maalum la Katiba,” alisema Lipumba.


Post a Comment