Serengeti.
"Ni zaidi ya miezi sita tangu nifanyiwe ukatili na mume wangu na mama
mkwe. Nahangaika kuuguza mguu niliokatwa kwa panga kunyunyiziwa maji ya
betri. sijui kama utapona. Kichanga nacho kinasumbua, jamani nimekosa
nini mimi kwa Mungu."Ni
maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio. Maneno ya ya Anna
Sabai (20) mkazi wa Kitongoji cha Manyata Kijiji cha Nyamakendo Kata ya
Mbalibali, wilayani Serengeti, ambaye anapaza sauti kutaka kujua walipo
wanaharakati ambao kwa hali aliyonayo , angeweza kupata msaada kutoka
kwao.Ukatili
aliofanyiwa Anna, mama wa watoto wawili katika ndoa yake na Hamisi
Sabai (20) yenye migogoro na ambayo inazidi kuuweka Mkoa wa Mara kwenye
taswira mbaya kutokana na uwingi wa matukio ya ukatili dhidi ya
wanawake.
Agosti
Mosi, 2013 ikiwa ni siku ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika
mnadani, Anna akiwa na uja uzito wa miezi tisa na akihesabu siku tu kwa
ajili ya kujifungua, aliamriwa na mume wake kwenda kuchunga ng'ombe,
bila kujali hali yake.
"Kwa
kweli nilikuwa na hali mbaya sana," anakumbuka Anna wakati anaongea na
Mwananchi kuhusu ukatili dhidi yake. "Nikiwa malishoni nilikaa chini ya
kivuli huku ng'ombe wakiendelea kula majani. Hali ilivyozidi kuwa mbaya
nilisinzia. Alipokuja mume wangu akanikuta nimelala na hapo hapo akaanza
kunishambulia kwa kipigo, akidai kuwa nilikuwa na mwanamume kutokana na
mapenzi kunoga ndio maana nilisinzia na kuacha ng'ombe wanazagaa."
Anasema
pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake, walipofika nyumbani
mama mkwe wake Bhoke Sabai alizidi kumtia hasira kijana wake akidai kuwa
nilikuwa na mwanaume, natakiwa kupewa kipigo ili iwe fundisho.
"Pamoja
na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea, bado akaona aache fimbo na
akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto," anasema Anna huku akitokwa
na machozi.
"Niliumia
sana... nikatamani kufa, maana hali ilikuwa mbaya. Sikuwa na msaada.
Baadaye akanifungia ndani ili watu wasijue; wala hakuna kwenda
kutibiwa."
Amwagiwa tindikali ili kuzuia damu isitoke
Huku
akiwa amebeba mtoto wake na kutembea kwa shida, Anna anasema ili watu
wasijue unyama aliotendewa, walileta maji ya betri na kumwagia kwenye
kidonda.
"Maumivu
yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua. Nilifikia hatua kama ningepata
kitu cha kujimaliza, ningejiua. Nilikuwa nasumbuliwa na mimba na huku
naumizwa hivi," analalamika. "Jamani wanaharakati wanaotetea wanawake
wako wapi maana nitakatwa mguu hivi hivi."
Anasema
matokeo yake mguu ukaoza kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu na kwamba
ndugu zake hawakuambiwa na mama mkwe wake alikuwa akiendelea kumkejeli
kila wakati.
"Sijaona watu wenye roho ya kikatili kama hao, kwa kuwa walilenga kuniua bila kosa," anasema.
Aokolewa na mama yake mzazi
Anasema
kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani ili majirani
wasijue, kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu, kwa nini afe bila ndugu
zake kumwona. Ndipo bila kutarajia alishtukia mama yake mzazi, Mnanka
Chacha (48) akifika hapo baada ya kutaarifiwa na majirani.
"Nilipomwona
mama nikasema basi sasa hata kama nikifa, niko katika mikono salama kwa
kuwa huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu. Nilijua kama
ningefia mkononi mwa hao huenda maiti ingetupwa kama mbwa. Nilijisikia
ahueni kwa kumuona mama," anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu
Anasema
kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha Hospitali Teule ya Nyerere kwa
ajili ya matibabu na madaktari walipomwona walimwambia kuwa hawana uwezo
tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo. Hivyo wakamwandikia barua kwenda
Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza.
Akosa pesa
Kutokana
na ukata wake, alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi nyumbani kwake
kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema, ili aweze kwenda naye Mwanza kwa
ajili ya matibabu.
Mume achana barua ya rufaa
Katika
kuhakikisha juhudi za kupelekwa hospitali hazizai matunda, akiamini kuwa
mume wake alikuwa ameishajirudi, alimpa barua ya rufaa ili watafute
fedha za matibabu, lakini yeye akaichana na kumuacha asijue la kufanya.
"Alichana
barua ya rufaa ikawa sina namna yoyote ya kwenda kutibiwa Hospitali ya
Rufaa ya Bugando. Ikabidi nikae tu nyumbani nikiangalia mguu wangu
unaoza. Kwa kweli nahitaji msaada kwa watu wanaoguswa maana kula yangu
na hata ya mtoto ni ya shida. Siwezi kwenda zaidi ya hapa," anasema.
Anabainisha
kuwa mumewe alichana barua kwa madai kuwa nimetoa siri polisi na kwa
watu wengine na ndio maana akaamua kumkomoa kwa kuichana ili kupoteza
ushahidi.
CHANZO:http://www.mwananchi.co.tz
Post a Comment