Waombolezaji
na wafanyakazi wa kujitolea wameendelea kumiminika huko Kunming mapema
leo baada ya mashambuliaji wa kutumia visu kuua watu 29 kwenye ghasia za
mhemuko.
Wauaji hao, wanne kati yao waliuawa kwa risasi na polisi, walianzisha mauaji yao ya chinja-chinja kwenye Stesheni ya Treni ya Kunming katika Jimbo la Yunnan jana takribani Saa 3 Usiku (Kwa saa za China).
Picha za kutisha zilizosambazwa mkitandaoni zinaonesha miili, madimbwi ya damu na mizigo iliyotelekezwa na kutapakaa sakafuni kila kona ya stesheni hiyo katika kile mamlaka husika zimekiita 'shambulio la kigaidi lililopangwa kikamilifu'.
Leo, hospitali zilifurika wananchi waliofika kujitolea kuchangia damu waathirika huku wengi wao wakiwa katika hali mahututi.
Nje, mishumaa iliwashwa kwa muundo wa moyo wakati taifa lilikabiliana na mshituko kutokana na tukio hilo.
Inaaminika kwamba zaidi ya watu 10 walishiriki katika shambulio hilo. Pia wanne kati ya waliopigwa risasi jana, mmoja alichukuliwa akiwa bado hai. Wengine waliobaki bado wanasakwa vikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya CCTV, Televisheni ya Serikali ya China, washambulizi takribani wawili walikuwa wanawake. Mmoja aliuawa na polisi na mwingine alikuwa ni mwanamke aliyekamatwa. Amepelekwa hospitali kwa matibabu.
Idadi ya waliokufa imefikia 29 mpaka sasa na washambulizi wanne walipigwa risasi na kuuawa na polisi.
Mashuhuda wameelezea wauaji hao walivalia mavazi meusi huku walisambaa stesheni nzima, wakichinja watu wasio na hatia kwa kutumia majambia na mapanga.
Mwanafunzi Qiao Yunao, mwenye miaka 16, alikuwa kwenye stesheni hiyo na kushuhudia mauaji hayo ya kutisha.
Alisema: "Nilikuwa nikitoka nje, na kukimbilia kwenye mgahawa, na watu wengi walikuwa wakikimbili huko kwa ajili ya hifadhi."
"Niliwaona washambulizi wawili, wote wanaume, mmoja akiwa ameshika kisu cha kukatia matikiti maji na mwingine akiwa na kisu cha kukatia matunda. Walikuwa wakikimbia na kuchinja yeyote waliyekutana naye."
Leo polisi wenye silaha walikuwa wakifanya doria kwenye stesheni hiyo ya treni mchana, ambayo ilifunguliwa tena kwa ajili ya shughuli za kawaida.
Wasafishaji wameshaanza kumwaga dawa za kuzuia maambukizi na kusafisha eneo hilo huku maua ya rambirambi yakiwekwa na wapitanjia.
Mmoja, ambaye aliweka rundo la maua ya manjano na kujitambulisha tu kama Guo, alisema: "Hii ni kutoa rambirambi zetu kwa waathirika na kuonesha hatuna hofu tunapokabiliana na ghasia."
Mamlaka za China zimewashutumu kwa shambulizi hilo wanamgambo kutoka mji wa mbali wa Xinjiang, ambako ni makazi ya shinikizo kati ya serikali na Waislamu wanaoshinikiza kujitenga.
Shirika la Habari la nchini humo Xinhua, limevinukuu vyanzo vya habari vya serikali, likisema: "Ushahidi katika eneo la tukio unaonesha kwamba shambulio la kigaidi kwenye Stesheni ya Treni ya Kunming lilifanywa na vikosi vya wanaharakati wanaotaka kujitenga Xinjiang."
Mkoa wa Xinjiang unapakana na Afghanistan, Kyrgyzstan na Tajikistan na serikali ya China imeshutumu mashambulizi kadhaa yanayofanywa na wanamgambo huko.
Mkoa huo ni makao ya sehemu kubwa ya kundi dogo la Waislamu wa Uighur ambao wanachukizwa kwa jinsi mamlaka nchini humo zinavyoshughulikia imani zao.
Mashambulizi mengi yaliyoshutumiwa kufanywa na wanaharakati wa Uighur wanaoshikiza kujitenga yamefanyika mjini Xinjiang pekee, lakini stesheni hiyo iko zaidi ya maili 620 kutoka mji huo.
Hii ni mara ya kwanza kwa wa-Uighur kushutumiwa kwa shambulio kubwa na mbali kutoka yaliko makazi yao. Shambulizi ya kujitoa mhanga Tiananmen Square mjini Beijing, Oktoba mwaka jana pia lilishutumiwa na mamlaka husika kufanywa na kundi hilo.
Post a Comment