*Fifa yawapa marufuku kwa miezi 14
*Walikiuka usajili wachezaji wadogo
Mabingwa wa Hispania, Barcelona wamepata pigo kubwa baada ya kupigwa marufuku kufanya usajili kwa mwaka mmoja na miezi miwili.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limechukua uamuzi huo kutokana
na
Barcelona kuvunja kanuni za shirikisho hilo kwa kusajili mchezaji wa
kimataifa mwenye umri chini ya miaka 18.
Kwa adhabu hiyo, sasa Barca hawataweza tena kufanya usajili wowote
hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2015, ikimaanisha hawatafanya usajili
majira yajayo ya joto wala dirisha dogo la Januari.
Mbali ya adhabu hiyo, Fifa limewapiga faini Barcelona kiasi cha dola
305,000. Marufuku ya kusajili ni pigo kubwa kwa Barca kwa sababu imekuwa
na msimu mgumu.
Ni klabu ambayo majuzi tu kipa wake namba moja, Victor Valdes aliumia
vibaya na imeelezwa kwamba atakuwa nje kwa miezi saba, ambapo Barca
walishajipanga kuziba nafasi yake mwisho wa msimu, maana pia alitangaza
kwamba angeondoka.
Kadhalika Nahodha Carles Puyol ambaye amekuwa akiumia mara kwa mara
goti, alitangaza kukatisha mkataba wake mwisho wa msimu, akiamini
hangeweza tena soka ya ushindani, ili kuiachia klabu isajili mtu wa
kufaa.
Klabu hiyo iliyotwaa ubingwa wa dunia mara nne, ilikuwa
imeshadhamiria kumsajili golikipa wa Borussia Monchengladbach,
Marc-Andre ter Stegen na wiki iliyopita tu walikubaliana kumsajili
kiungo wa kimataifa wa Croatia, Alen Halilovic.
Barcelona pia imepita kwenye magumu juu ya usajili wa nyota wake,
Neymar, ikidaiwa kwamba palikuwa na ukwepaji wa kodi na kupindisha
taratibu kiasi kwamba Rais wa Barcelona, Sandro Rosell alijiuzulu
Januari na nafasi yake kuchukuliwa na Josep Maria Bartomeu.
Kadhalika hali hii inaiharibia Barcelona machoni pa watu waliokuwa
wakiiheshimu sana, zikiwamo kampuni kubwa na mashirika yaliyojihusisha
nayo, kama Unicef na Qatar Airways.
Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) nalo limeadhibiwa kwa kupigwa
faini ya dola 340,000 na kuonywa kurekebisha mara moja utaratibu wake wa
kuratibu mfumo uliopo wa soka, hasa kuhusu uhamisho wa wachezaji wadogo
wa kimataifa. Wanatakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya mwaka mmoja.
Kanuni za Fifa zinasema kwamba uhamisho wa kimataifa unaruhusiwa tu
ikiwa mchezaji husika ana umri wa miaka zaidi ya 18, vinginevyo lazima
mchezaji husika atimize moja ya vigezo vitatu vya uhamisho.
Vigezo hivyo ni kwa mchezaji kuhamia kwenye klabu ya nchi ambayo
wazazi wake wamehamia ikiwa mchezaji ana umri kati ya miaka 16 -18 ana
uraia tofauti nje ya Umoja wa Ulaya au eneo la kiuchumi la Ulaya.
Atatakiwa kuishi ndani ya uzio wa kilometa 100 kutoka klabu ilipo.
Uchunguzi wa Fifa umegundua wachezaji kadhaa walio chini ya umri wa
miaka 18 waliosajiliwa na kuchezea klabu hiyo kati ya 2009 na 2013
pasipo kutimiza vigezo hivyo.
Post a Comment