
Idadi ya waliokufa kutokana na mafuriko jijini Dar es Salaam imefikia watu 13 kufikia Jumatatu.
Mkuu wa
mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq amesema idadi hiyo huenda
ikaongezeka baada ya kupata taarifa za matukio ya mafuriko kutoka maeneo
yote ya mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa siku
tatu mfululizo tangu Ijumaa iliyopita, mvua kubwa ziliendelea kunyesha
na kusababisha madhara makubwa vikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu
ya barabara na madaraja, hivyo kukata mawasiliano na mikoa ya jirani ya
Pwani na Morogoro na hata ndani ya mkoa wenyewe.
Karibu maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam yameathirika kutokana na
mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko, huku wakaazi wa maeneo
ya mabondeni wakiathirika zaidi baada ya nyumba zao kujaa maji.
Miundombinu ya barabara na madaraja mbalimbali yanayounganisha jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake pia imeharibiwa.
Mradi
mwingine muhimu wa mabasi yaendayo kasi, DART unaolenga kutatua tatizo
la usafiri jijini Dar es Salaam, nao umeathiriwa na mafuriko hayo ambapo
magari, mashine na mifuko ya saruji imechukuliwa na maji hivyo
kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho za
kukamilisha mradi huo.
Shughuli
za urejeshaji wa miundombinu zimekuwa zikiendelea ikiwa ni pamoja na
matengenezo katika daraja la Mpiji linaloiunganisha mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani.
Hata
hivyo Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania, TMA, yametahadharisha
kuhusu kuendelea kunyesha kwa mvua na kuwataka watu wanaoishi katika
maeneo hatarishi kuhama ili kusalimisha maisha na mali yao.(CHANZO BBC)


Post a Comment