Na Anna Nkinda- Maelezo, Lindi
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wazazi na walimu kushirikiana
kwa pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanakwenda shule na kusoma jambo
ambalo litasaidia kupanda kwa kiwango cha elimu mkoani humo.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo
hivi karibuni wakati akiongea na wananchi pamoja na wanafunzi wa
kijiji cha Ruaha waliofika kumsalimia mara baada ya kumaliza mkutano
wake na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi la Ruaha lililopo katika
kata ya Mingoyo wilaya ya Lindi mjini.
Mjumbe
huyo wa Halmashauri Kuu Taifa alisema kiwango cha elimu katika mkoa
huo kiko chini lakini kama wazazi watahakikisha watoto wao wanaenda
shule kwa wakati na walimu wakihakikisha watoto wamefika shule na
kuwafundisha kiwango cha elimu kitapanda kwa kiasi kikubwa.
“Na
ninyi watoto muache tabia ya kupoteza muda kwa kuokota mabibo au maembe
tumieni muda huo kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yenu
kwa kufanya hivyo mtakuwa na maisha mazuri hapo baadaye”, alisema Mama
Kikwete.
Akiwa
katika matawi la Mkwaya, Ruaha na Majengo Mama Kikwete aliwataka vijana
wa CCM kuungana kwa pamoja na kutafuta eneo kubwa la kikundi ambalo
watalitumia kulima kilimo cha mazao ya biashara kama vile ufuta ambao
utawapatia fedha nyingi na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Aidha
Mama Kikwete pia aliwataka kinamama kwenda kupima saratani ya mlango wa
kizazi ambayo inauwa wanake wengi lakini vifo vya ugonjwa huo
vinazuilika kama mgonjwa atakwenda kupima mapema na akigundulika kuwa na
dalili za ugonjwa huo katika hatua za awali ataweza kupata matibabu na
kupona.
Mama
Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini
alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya
kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na
viongozi.
Post a Comment