Rais Jakaya Kikwete ameunda Tume ya Uchunguzi, kuhusu vitendo vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni Tokomeza.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ilisema, Rais
ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi
Sura ya 32.
Kutokana na hatua yake ya kuunda Tume hiyo, Rais Kikwete amemteua Jaji
na Balozi Mstaafu Hamisi Msumi kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Vilevile, Rais Kikwete amewateua Jaji Mstaafu Stephen Ihema na Jaji
Mstaafu Vincent Lyimo kuwa Makamishna. Rais pia amemteua Frederick
Manyanda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kuwa Katibu wa Tume hiyo.
Hatua ya Rais Kikwete kuunda tume hiyo inakuja baada ya Operesheni
Tokomeza Ujangili kusitishwa na Bunge kutokana ukiukwaji wa sheria na
haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Operesheni hiyo iliayoanza Oktoba 2013 na kusitishwa Nobemba 4 mwaka
jana, ndiyo iliyowang’oa mawaziri wanne kwa kushindwa kusimamia vizuri
utekelezaji wake.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo
ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa uteuzi huu ulianza jana, na kutaja
majukumu ya tume hiyo kuwa ni pamoja na kuchunguza na kubaini Operesheni
Tokomeza ilivyoendeshwa.
Majukumu mengine ni kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu
na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza
na kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria,
Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza na kubaini kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote
wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua
zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.
Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote
atakayebainika kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni
Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Post a Comment