Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akimpongeza Askofu Mteule, Alen Legeza Siso, baada ya kumkabidhi Katiba
na Kanuni za Kanisa la Methodist Tanzania, wakati wa Ibada Maalum ya
Kuwekwa Wakfu (kusimikwa) askofu huyo, iliyofanyika kwenye Kanisa la
Imanueli dhehebu la Methodox, Jimbo teule la Pwani na Mashariki lililopo
Bunju Jijini Dar es Salaam, leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwahutubia Waumini wa dini ya Kikristo wa Kanisa la Methodist
Tanzania, wakati wa Ibada Maalum ya Kusimikwa Askofu Mteule Alen Legeza
Siso, iliyofanyika kwenye Kanisa la Imanueli, Jimbo teule la Pwani na
Mashariki lililopo Bunju Jijini Dar es Salaam, leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiagana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Methidist Tanzania, Dkt. Mathew
Byamungu, baada ya Ibada maalum ya kusimikwa Askofu Mteule, Alen Legeza
Siso, (kulia) kuwa Askofu wa Jimbo la Mashariki na Pwani iliyofanyika
kwenye Kanisa la Imanueli, Jimbo hilo lililopo Bunju Jijini Dar es
Salaam, leo.
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Methidist Tanzania, Mathew Byamungu, akimsimika
Askofu Alen Legeza Siso, kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mashariki na
Pwani, Makanisa ya Methodist Tanzania, wakati wa Ibada Maalum ya kuwekwa
Wakfu Askofu huyo iliyofanyika leo Mei 3, 2014, kwenye Kanisa la
Emanueli lililopo Bunju jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Waumini wa Kanisa hilo waliohudhuria Ibada hiyo maalum ya kumsimika Askofu Mteule, Alen Siso.
Baadhi ya Waumini wa Kanisa hilo waliohudhuria Ibada hiyo maalum ya kumsimika Askofu Mteule, Alen Siso.
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Dkt. Mathew Byamungu, akimvisha
pete Askofu Alen Legeza Siso, ya kuashiria kuwa Askofo wa Kanisa hilo,
baada ya kusimikwa rasmi wakati wa Ibada maalum iliyofanyika Kanisa la
Emanueli lililopo Bunju jijini Dar Es Salaam, leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhiri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist
Tanzania, Dkt. Mathew Byamungu, Askofu Mteule wa Jimbo la Mashariki na
Pwani, aliyesimikwa, Alen Siso na baadhi ya wachungaji wa Kanisa la
Emanuel, baada ya ibada maalum ya kusimikwa Askofu, Alen, leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhiri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa katika picha ya pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist
Tanzania, Dkt. Mathew Byamungu, Askofu Mteule wa Jimbo la Mashariki na
Pwani, aliyesimikwa, Alen Siso na baadhi ya wachungaji wa Kanisa la
Emanuel, baada ya ibada maalum ya kusimikwa Askofu, Alen, leo.
Kikundi cha Kwaya cha Msasani, kikitoa burudani wakati wa Ibada hiyo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akisalimina na baadhi ya wachungaji wa Kanisa la Emanueli, Jimbo la
Mashariki na Pwani, wakati alipowasili jimboni hapo kwa ajili ya
kuhudhuria Ibada maalum ya Kusimikwa, Askofu Mteule, Alen Legeza Siso,
jijini Dar es Salaam, leo.
**************************************
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KATIKA IBADA YA
KUSIMIKWA ASKOFU MTEULE ALEN SISO WA KANISA LA METHODIST TANZANIA-
JIMBO TEULE LA MASHARIKI NA PWANI, DAR ES SALAAM, TAREHE 3.5.2014
Mhe. Said Meck Sadiki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Baba Dkt. Mathew Byamungu , Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania:
Alen Siso, Askofu wa Jimbo Teule la Mashariki na Pwani;
Mhe. Jordan Rugimbana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni;
Maaskofu na Wakuu wa Madhehebu mbalimbali mliopo;
Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa mliopo hapa;
Wawakilishi wa Mashirika na Wahisani mbalimbali;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Waumini wote mliohudhuria;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Bwana Yesu asifiwe!
Aawali
ya yote, tuna kila sababu kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ,
kwa kutupa uzima na kutuwezesha kukusanyika hapa siku leo. Tuliopata
kibali hiki, ni upendeleo wa aina yake, wapo wenzetu wengi, wameshindwa
kuiona siku ya leo, wengine wamelala hospitalini wakipigania uhai. Sisi
tuliopata nafasi hii, tuna kila sababu, kumrudishia Mungu sifa na
utukufu.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Kabla
sijaendelea, napenda niseme neno moja; Nimekuwa na bahati kubwa
kusimama chini ya dari ya Kanisa la Methodist Tanzania. Nakumbuka ni
mwaka jana, Aprili 27, mlinialika katika Harambe na Ibada Maalumu ya
kumshukuru Mungu, kwenye Kanisa la Methodist Tanzania, pale Msasani.
Leo hii mmenialika tena katika tukio hili la kihistoria, la kusimikwa
Askofu Mteule Alen Siso. Nawashukuru sana, kwa moyo wa upendo na heshima
kubwa mnayonipa. Sina maneno mazito ya kushukuru, zaidi ya kusema ;
Bwana azidi kuwatunza na kuwapigania !
Nichukue
fursa hii kipekee, kukushukuru wewe binafsi Baba Askofu Mkuu Dkt.
Byamungu, Watendaji wa Jimbo Teule la Mashariki na Pwani, na Uongozi
mzima wa Kanisa la Methodist Tanzania, kwa mwaliko wenu wa leo.
Nimeupokea kwa moyo mweupe, na mikono miwili. Asanteni sana.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu waumini;
Napenda
nitumie nafasi hii, kulipongeza Kanisa la Methodist Tanzania, chini ya
uongozi wako Baba Askofu Mkuu, Dkt. Byamungu , kwa namna mnavyoendelea
kupanuka, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali, kuwaletea
wananchi wake maendeleo.
Kwa
mujibu wa maelezo, Kanisa la Methodist Tanzania, lilianza kutoa huduma
ya kiroho hapa nchini, Juni 12 mwaka 1991. Leo hii lina miaka 23 tu,
lakini tumeona namna lilivyopiga hatua kubwa, kuchangia nyanja
mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Ujenzi
wa hospitali tano mkoani Geita, shule mkoani Arusha, uchimbaji visima
virefu kwa shule na magereza katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na
ujenzi wa Chuo cha Theolojia huko Dodoma na Arusha, ni baadhi tu ya
mambo mengi mema, yanayofanywa na kanisa hili. Kwa niaba ya Serikali,
nawapongeza kwa kazi kubwa mnayofanya. Tutaendelea kuwa karibu nanyi,
kwa kila jambo mtakaloona tunapaswa kushirikiana.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda
nipongeze pia, mchango mkubwa unaotolewa na mashirika na taasisi
mbalimbali za dini hapa nchini, kusaidia juhudi za Serikali kuwaletea
wananchi wake maendeleo. Taasisi na mashirika ya dini, yamekuwa mstari
wa mbele kujenga shule, vyuo, hospitali na huduma zingine mbalimbali
za jamii. Serikali peke yake haiwezi kufanya miujiza.Tunathamini na
kutambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika na taasisi zote za
dini . Nawahakikishia kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana kwa
karibu na mashirika haya, kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yetu.
Wito
wangu kwa mashirika na taasisi za dini; Fanyeni kila linalowezekana,
kuboresha zaidi huduma zenu, ili ziendane na ushindani wa zama hizi.
Hakikisheni mnakuwa na shule bora za kisasa zenye vifaa vya kutosha
kufundishia, kadhalika hospitali zenu ziwe za kisasa , hata visima
mnavyochimba, viwe na ubora wa unaotakiwa. Nawatia shime; Kazi
mnayofanya ni nzuri, endeleeni na moyo huo, na Bwana atazidi kubariki
kazi za mikono yenu.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Napenda
kutumia nafasi hii kuwaasa Watanzania kudumisha amani na mshikamano
wetu, ambao umekuwa tunu kubwa tangu tulipopata Uhuru. Ni juzi tu
tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wetu huku nchi yetu ikiendelea kuwa
kisiwa cha amani na utulivu. Katika hili, nawakumbusha watu wa Mungu
kukesha na kuliombea Taifa letu. Si watu wote wanafurahia mafanikio
haya. Wapo wanaotuombea mabaya usiku na mchana, wanataka waone siku
moja tumefarakana na kupoteza mwelekeo. Naamini watu wa Mungu mkisugua
goti katika hili, kamwe Shetani hatapata nafasi ya kujiinua katika Taifa
letu.
Sisi
katika Serikali, tutaendelea kusimamia kwa nguvu zote, dhamana kubwa
mliyotupa, ya kudumisha Umoja na Mshikamano wa nchi yetu. Naamini kwa
kuwa hata Mungu wetu hafurahii mafarakano na utengano, ataendelea
kusimama upande wa haki kutupigania. Tutaendelea kusimamia misingi ya
utawala wa bora bila kujali rangi ya mtu kabila, dini, jinsia wala
eneo analotoka.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Upendo
ni sharti muhimu sana katika maisha ya kila siku ndani ya jamii.
Nilipozungumza nanyi mwaka jana huko Msasani, nilizungumzia hili,
Napenda kurudia tena katika hadhara hii. Nazungumzia hili kutokana na
mazingira ya mpito ambayo Taifa letu, linapita kwa sasa.
Baba
Askofu Mkuu, ni vigumu nchi yetu kuendelea kuwa na amani kama watu wetu
hawapendani. Ni vigumu watu wetu kuendelea kukaa pamoja kama
hawavumiliani. Ni vigumu nchi yetu kuendelea kuwa ya amani na utulivu,
kama watu wetu hawaheshimiani. Bila Upendo na Kuvumiliana, Taifa letu
litasambaratika.
Tupo
katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Tulianzisha mchakato huu kwa
nia njema ya kuwawezesha Watanzania kupata Katiba, inayoendana na
mazingira ya sasa. Tofauti na ilivyotarajiwa, mchakato huu umeanza
kugubikwa na malumbano huku baadhi ya Wabunge wa Bunge Maalumu la
Katiba, wakitangaza kususa vikao. Kukosekana Upendo, ni moja ya sababu
kuu ya kushindwa kuvumiliana, hata katika mijadala ya Bunge la Katiba.
Ndani ya Biblia takatifu, Kitabu cha Wakorintho wa Kwanza, mlango wa 13, mstari wa 4 hadi 8, kimezungumza vizuri sana kuhusu Upendo; nitanukuu:-“Upendo
huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu, upendo hautakabari, haujivuni,
haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu,hauhesababu
mabaya, haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli, huvumilia
yote, hustahimili yote, upendo haupungui neno wakati wowote… Ukiendelea mstari wa 13, unahitimisha kwa kusema:- “Basi sasa inadumu imani, tumaini , upendo haya matatu; na katika hayo, lililo kuu ni UPENDO.”
Pia Maandiko matakatifu katika Waraka wa Kwanza wa Petro Mtume, mlango wa 4, mstari wa 8 hadi 10, yanasema hivi; nitanukuu:-” Zaidi
ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana kwasababu upendano
husitiri wingi wa dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi pasipo
kunung’unika kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa
kuhudumiana kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.”
Nawasihi
waumini wa dini zote nchini, kuzidi kuombea jambo hili , ili mchato
huo, ufikie hatma njema kama ilivyokusudiwa. Nawakumbusha pia Wabunge
wa Bunge Maalumu la Katiba, watakaporejea Agosti mwaka huu, kujenga
upendo miongoni mwao , wakumbuke kwamba wanawakilisha mamilioni ya
Watanzania. Biblia imetuambia kuwa wakijenga upendo, Watavumiliana, hawatahesabiana mabaya, hawatapenda udhalimu na wala hawatakoseana adabu.
Baba Askofu Mkuu;
Viongozi wa dini mbalimbali mliopo;
Ndugu Waumini;
Jukumu
mlilotupa la kuongoza Watanzania, haliwezi kuwa na tija, kama wananchi
tunaowaongoza, hawatamjua Mungu na kufuata mafundisho yake. Watu wetu
wakimjua Mungu hawatatoa wala kupokea rushwa, hawatauza wala kutumia
dawa za kuleva, hawatajichukulia sheria mikononi, hawataiba wala
kudhulumu, hawatajilimbikizia mali, hawatatega kazini, watakaa mbali na uasherati na
maovu mengine yote. Taifa la wacha Mungu lina amani , upendo, umoja na
mshikamano. Hivyo lina nafasi kubwa ya kusonga mbele. Lakini ni kazi
ngumu sana kuongoza Taifa la watu waliotekwa na ibilisi.
Natoa
changamoto kwa viongozi wa dini zote nchini, kuhakikisha mnawajengea
waumini wenu, misingi ya madili mema. Waumini wenu wakifuata mafundisho
ya Mungu, Taifa litakuwa na raia wema, wachapakazi, maovu ndani ya
jamii yatapungua sana kama si kumalizika kabisa.
Vilevile
nitumie nafasi hii, kuwakumbusha waumini wa dini zote nchini, kuendelea
kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana. Ni wajibu wa kila mmoja wetu,
kuheshimu dini ya mwenzake. Hakuna dini bora kuliko nyingine, dini zote
ni sawa, tofauti yake, ni taratibu za namna ya kuabudu. Tofauti hizi
haziondoi haki yetu ya kuwa watoto wa Baba mmoja Mungu, walio katika
nyumba moja ambayo ni Tanzania. Pendaneni, kwani maandiko matakatifu,
yanatufundisha kuwapenda hata maadui wanaotuudhi.
Kitabu cha Mathayo, mlango wa 5, mstari wa 43 hadi 45 unasema hivi,nanukuu; “Mmesikia
kwamba imenenwa umpende jirani yako, na umchukie adui yako, lakini mimi
nawaambia, wapendeni adui zenu , waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa
wana wa Baba yenu aliye mbinguni, maana yeye huwaangazia jua lake waovu
na wema , huwanyeshea mvua wenye haki na wasio na haki.”
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Nitumie
nafasi hii kukupongeza Baba Askofu Alen Siso, kwa namna Mungu
alivyokuinua, hatimaye leo umesimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Teule
la Mashariki na Pwani. Naamini kuchaguliwa kwako, hakukuja kwa bahati
bali “BWANA AMEKUCHAGUA, NA ANA HAJA NAWE.”
Baba
Askofu Siso, tukio hili kwako, ni ile sauti iliyoandikwa katika Kitabu
cha nabiiIsaya mlango 6 mstari wa 8, ikisema kwamba, nanukuu; “ Kisha
nikasikia sauti ya Bwana akisema, Nimtume nani, naye ni nani
atakayekwenda kwa ajili yenu? Ndipo niliposema. Mimi hapa, nitume mimi.”
Ujumbe huu umeelezwa pia katika Injili ya Luka , mlango wa 12, mstari wa 42 hadi wa 43, nanukuu; Bwana
akasema, ni nani basi aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye
Bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa
wakati wake?”
Baba
Askofu Siso, mistari niliyoisoma hapo juu ni ushahidi kwamba umepokea
utumishi huu kwa Kuitwa na Kuitika. Sisi sote tuliokusanyika hapa leo,
ni mashahidi. Ifanye kazi ya Mungu kwa moyo mmoja. Naamini utakuwa
mchungaji mwema, utakaowachunga kondoo wa Mungu, na kuwarudisha zizini
wale waliopotea.
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Niwaombe
viongozi wote wa kanisa hili, kuanzia wewe Baba Askofu Mkuu, Dkt.
Byamungu, kuzidisha mshikamano miongoni mwenu, na kumsaidia Askofu wetu
mpya, kufanya kazi hii takatifu kwa ufanisi. Zingatieni maneno ya
Mungu kutoka Waraka wa Kwanza wa Petro Mtume, mlango wa 5, mstari wa 2 hadi wa 4, nanukuu ;“Lichungeni
kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa bali
kwa hiyari, kama Mungu atakavyo,si kwa kutaka fedha ya aibu bali kwa
moyo, wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa
kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”
Baba Askofu Mkuu Byamungu;
Askofu Siso;
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Kabla
ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kuwahakikishia kuwa, nimepokea
changamoto zenu mbalimbali mlizosoma kwenye risala yenu. Nimesikia
matatizo yenu ya maeneo ya kujenga miradi. Serikali kupitia mamlaka
zake, itafuatilia kwa karibu masuala hayo, kuangalia namna bora ya
kuyapatia ufumbuzi.
Baada
ya kusema hayo, kwa mara nyingine, napenda kukushukuruni kwa kunialika
mahali hapa siku ya leo. Nazidi kuwasihi sana watu wa Mungu, msichoke
kuliombea Taifa letu, kwani kuna nguvu kubwa ndani ya maombi. Kemeeni
njama zote zenye nia mbaya ya kuvuruga Amani, Umoja na Mshikamano
wetu. Daima, pendeni kusikiliza mema, msivutike kusikiliza maovu .
Nawaachia ujumbe kutoka Kitabu cha Mithali, mlango wa 11, mstari wa 31
hadi 32, unasema hivi; “ Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima, bali
ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali. Midomo ya mwenye haki huyajua
yatakayokubaliwa, bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.”
Mungu awabariki sana. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment